Pambo

Mali ya mtu mwenye wake wengi hugawanya kwa usawa baina ya familia zote

Na  BENSON MATHEKA April 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIFUNGU cha 40 cha Sheria ya Urithi kinatoa masharti mbalimbali kuhusu urithi wa mali katika ndoa za wake wengi.

Kinasema kuwa mwanamume mwenye wake wengi akifariki, mali yake binafsi na ya familia pamoja na mali zingine zilizosalia zitagawanywa kati ya familia zake.

Mali hiyo hugawanya kulingana na idadi ya watoto katika kila familia, yaani kila mtoto na kila mke aliye hai hupata mgao.

Kama ilivyo katika ndoa za mke mmoja, kila mke katika ndoa ya wake wengi anastahili kupata sehemu yake ya mali binafsi na pia ya familia ya marehemu kikamilifu, pamoja na haki ya kutumia mali zingine zilizobaki maisha yao yote, haki ambayo itaisha iwapo ataolewa tena.

Mamlaka ya kugawa au kutoa sehemu yoyote ya mali kwa watoto wa marehemu hutekelezwa sawasawa na ilivyo katika ndoa ya mke mmoja. Katika ndoa zote, ikiwa mtoto ataona kuwa ugavi wa mali ya marehemu baba yake haujafanywa kwa njia ya haki, anaweza kuwasilisha ombi kortini ili apewe haki yake ya urithi.

Mahakama inaweza kuamua kumpa mlalamishi sehemu ya mali halisi ya urithi, ikiwa ni pamoja na kurekebisha ugavi wowote uliofanywa na ambao aliupinga.

Mjane akifariki au kuolewa tena, mali yote iliyobaki ambayo alirithi kutoka kwa marehemu mumewe hupewa mtoto aliyesalia ikiwa ni mmoja tu, au kugawanywa kwa usawa kati ya watoto wote waliosalia.Katika ndoa zote, ikiwa mrithi wa mali ya marehemu ni mtoto au watoto walio chini ya umri wa miaka 18, mali hiyo itashikiliwa kwa niaba yao.

Ikiwa mtoto wa marehemu amezaa watoto wake mwenyewe (wajukuu wa marehemu) lakini akafariki kabla ya mamake, basi sehemu yake ya mali itapewa watoto wake (wajukuu wa marehemu) au kushikiliwa kwa niaba yao hadi wafikishe umri wa miaka 18.

Urithi usio na wosia ni suala tata linaloathiriwa na masuala mengi ya kijamii na kitamaduni ambayo wakati mwingine yanakinzana na misingi ya sheria.

Sheria ya Urithi inaweka kanuni thabiti za urithi usio na wosia ili kulinda maslahi ya warithi wote na kuhakikisha ugavi wa mali unafanywa kwa haki.

Mfumo huu wa kisheria unapendelea haki za wake na watoto, ukitoa mwongozo wazi wa ugavi wa mali na kushughulikia changamoto ibuka katika urithi wa ndoa za mke mmoja au wake wengi ili kuepusha migogoro.

Sheria za urithi usio na wosia zina jukumu muhimu la kusawazisha kanuni za urithi zinazotambuliwa na tamaduni mbalimbali nchini Kenya.