Mambo ya chumbani ni ‘takatifu’, usiyaanike kwa watu
KUNA mambo ya kulinda katika ndoa. Hasa, usifichue mengi kuhusu maisha ya chumbani ya ndoa yako kwa marafiki zako.
Huenda wakadharau ndoa yako, kukufanya uifananishe na ya wengine, au wakupatie ushauri usiofaa.
Katika ndoa, masuala ya chumbani huwa takatifu na yanafaa kuwa hivyo.
Ili kukoleza raha, usiwe mtu wa kufurahia shughuli chumbani peke yako, isiwe tu kupata raha kwako pekee, mpe mwenzi wako raha.
Watu wanavuruga shughuli chumbani kwa kuwa na ubinafsi. Mkipeana raha mtanogesha mapenzi na kufanya ndoa kunawiri.“Muhimu kabisa, usitumie ngono kama silaha ya kumwadhibu mwenzi wako ili kupata kile unachotaka.
Hivi ni vita ambavyo vitageuka kuwa vibaya na kuporomosha ndoa,” asema Grace Kamau, mtaalamu wa masuala ya ndoa.Anasema watu wanajikosesha raha kwa kuendelea kusononeka kimya badala ya kubadilisha uzoefu wa shughuli chumbani na wenzi wao.
“Usitumie tendo la ndoa kuficha mambo. Kuzingatia burudani bila kusuluhisha matatizo kunaleta udanganyifu na kudhoofisha ndoa yako,” aeleza.Watu wana uwezo tofauti wa kuburudishana na ni makosa makubwa kulinganisha mume au mke wako na mpenzi wako wa zamani.
“Usilinganishe uwezo wa tendo la ndoa wa mwenzi wako na wa mpenzi wako wa zamani au hata mpango wa kando. Kama huyo ex wako angekuwa mzuri, ungemuoa au kuolewa naye lakini uliolewa au kumuoa mwenzi wako kutokana na sifa alizonazo. Zika yaliyopita na uyasahau, jifunze raha mpya na mwenzi wako,” asema.
Kamau anakosoa watu wanaodhani wanajua wenzi wao wanavyopenda kufanyiwa chumbani akisema huwa wanaenda kinyume na kanuni zilizothibitishwa.
“Usidhani unajua jinsi mwenzi wako anavyopenda kufurahishwa, muulize usikie kutoka kwake. Acha kuwa mjua yote. Ni sawa na kumparamia bila kumuandaa ukisema anafaa kuwa tayari kukuhudumia wakati wowote. Kwa kufanya hivi, unamuumiza na anaweza kukuchukia,” asema.
Usiwe mkali kwa mwenzi wako. Hii inafanya watu kupoteza hamu ya tendo la ndoa. Tumia maneno matamu. Usiache kurushia mwenzi wako mistari sawa na siku zenu za mwanzo. Usiwe mkali unaposhika sehemu zake za raha ukisema ni mali yako.
“Ukimsinya mwenzi wako basi usitarajie makubwa chumbani. Kumbuka msemo kwamba ya sebuleni yabaki huko, yasitue chumbani.Ukiendelea kuumiza hisia za mkeo, hatachangamka kukupa mwili wake,” aeleza Kamau.
Anaongeza kuwa hufai kuudhihaki mwili wa mwenzi unayetarajia kuufurahia. Ukidhihaki sura yake, ukubwa wake, basi usitarajie fataki chumbani. “Tumia mwili wa mwenzi wako kwa heshima na hiyo itamfanya akuchangamkie na mtakuwa na nyakati zisosahaulika.”