Martha ashauri wanawake kuepuka ndoa zilizo na dalili za fujo
NA MWANGI MUIRURI
SAFARI ya mwanamitindo Martha Wanjiku,23, katika ndoa haikudumu kwa sababu ilikaa mwaka mmoja tu kati ya 2021 na 2022 na akatoka akiwa na mtoto mmoja.
Bi Wanjiku kutoka Kaunti ya Murang’a anasema alikuwa hajakomaa akili vile na kwamba aliingia kwa uhusiano huo kwa ule msukumo tu wa ujana maji ya moto.
“Mwanzoni nilimpenda sana mtoto huyo wa watu ambaye alikuwa ndiye mume wangu,” asema Bi Wanjiku.
Kulingana na Bi Wanjiku miezi mitano ya kwanza hali ilikuwa shwari na mapenzi yalikuwa yamenoga hadi akashika ujauzito.
“Lakini kuanzia mwezi wa sita, nilianza kuona mume wangu akibadilika polepole na kuanza fujo zisizo na maana. Hata pasipo kuongeleshwa na yeyote, unampata amekasirika. Lakini nikiwa karibu kujifungua, alitangaza kwamba angenichapa,” asema.
Bi Wanjiku anasema kwamba hakubishana na wala hakuonyesha ishara yoyote ya kupandwa na hasira.
“Nilisubiri aende madukani alikozoea nami nikapanga virago vyangu na nikatoka. Nilirudi kwa mamangu mzazi na nikamwambia nilikuwa nimeamua kutamatisha maisha yangu ya ndoa. Mamangu aliniuliza sababu ya kufanya uamuzi huo na nikamjibu kwamba mwili wangu si ngoma la sebene,” akasema.
Bi Wanjiku anasema kwamba anaweza akavumilia madhila yote ya dunia isipokuwa matusi na vita.
Anapuuzilia mbali watu wenye mtazamo kwamba kutandikwa kwa ndoa ni njia mojawapo ya kuonyeshwa mapenzi.
Pia, anasema kwamba yeye hajui kutoa maneno makali wala kuhusika na ghasia na hakuwa tayari kufundishwa namna ya kukumbatia hali hizo mbili za uhuni.
Bi Wanjiku anasema kwamba “mimi nilifanya uamuzi kwamba Mungu ndiye hujalia wanaomwamini boma la kudumu lakini hakuna pale kwa maandiko wala kwa ufunuo ambapo imerekodiwa boma la fujo na matusi ni baraka kutoka kwa Mungu”.
Bi Wanjiku anasema kwamba ilimjuzu kuanza maisha yake upya na hata akajiondoa kwa mamake mzazi.
“Nilikodisha nyumba yangu ambapo kwa sasa namlelea mtoto wangu msichana,” asema akiongeza kwamba bado anamtambua babake mtoto huyo kama “damu ya mtoto wangu lakini kuna ile mipaka hatuwezi tukavuka”.
Anadokeza kwamba hawezi akamruhuru mumewe wa zamani akuje kumvurugia maisha yake na mtoto wake kwa msingi kwamba yeye ndiye baba mzazi wa mtoto huyo.
“La muhimu hapo ni kudumisha heshima,” asisitiza.
Ushauri wake kwa wanawake ni wakome kuingia kwa ndoa kama njia moja ya kusaka uthabiti wa kimaisha.
“Ukiingia kwa ndoa eti unahepa kuwa maskini ama upate pa kupata mlo na makazi, wewe utakuwa umejitoa kafara kwa utumwa. Ingia kwa ndoa ikiwa kwa uhakika moyo wako umeamua kupenda. Ikiwa ni uthabiti wa pato unasaka, jitume kivyako jinsi ambavyo huyo mwanamume unayedandia amejituma na kuwa na chake,” ashauri.
Aidha, Bi Wanjiku anaonya wanawake wenzake dhidi ya kuwa na tamaa ya kujipa vya bwerere akisema huko ndiko visa vya kisasi hutokana na kujiangazia kama mashambulio yanayosababisha vifo na ulemavu.
“Heshimu mali ya wengine na pia uzingatie kutimiza mikataba uliyoweka na wengine pasipo kuwa na tamaa au ujanja. Jiheshimu pia ukiwa mwanamke na uelewe kuna mambo hufai kukumbatia kama vile uraibu wa pombe na dawa za kulevya. Jitume kujiwekea akiba na uwekeze. Pombe na mihadarati achia wajinga,” asema.
Pia, anasema mwanamke yeyote anayejithamini humwogopa Mungu na kuheshimu sheria za nchi kando na kuwa na heshima kwa wote.
Lakini cha mno, anakushauri wewe unayelenga kuingia kwa ndoa au tayari uko ndani, “usivumilie fujo na matusi, jitoe mapema ukajipe amani”.
Soma Pia: Uchunguzi kuhusu mshukiwa wa mauaji ya Starlet Wahu wakamilika
Anasema kwamba anasubiri mume ambaye atajileta kwake akiwa na nia njema akifahamu kwamba sio chombo cha nyumbani anajipa bali ni mshirika wa kuinuana katika hali zote za kimaisha, lengo likiwa kuimarika kama washirika.
“Na ni lazima huyo mwanamume kwanza ampende mtoto wangu. Huyo ni lazima umpende kwa asilimia 100. Hata heri mimi unipende asilimia 50 lakini umheshimu na umpende malaika huyu wangu. Sijashindwa kumlea na amani na furaha yake sio suala la mjadala,” asema.