Mipaka ni muhimu hata katika masuala ya chumbani
KATIKA ndoa, kila kitu kinapaswa kuwa na mipaka, sio kuzidisha au kupunguza.
Kinachofurahisha mwenzi mmoja kinaweza kukosa kufurahisha mwingine. Kuzidisha jambo linaloleta raha kunaweza kulifanya kuwa chungu. Japo ngono imetajwa kuwa muhimu katika ndoa, wataalamu wanasema inapaswa kuwa kwa kipimo.
“Ni vizuri kushiriki ngono mara nyingi katika ndoa; lakini unapofanya hivyo, hakikisha kuwa ngono siyo kitu cha pekee mnachokipa umuhimu, la sivyo mtakuwa na ndoa dhaifu iliyojaa ngono nzuri,” asema Mike Opande mtaalamu wa masuala ya ndoa.
Anasema japo ni vizuri kufanya mzaha na kuwa mcheshi kimapenzi na mwenzi wako, hakikisha huendi mbali kiasi cha kuwa matusi au kuchukiza, la sivyo mwenzi wako anaweza kuhisi kudharauliwa au kutumiwa.Kama wanandoa, asema Opande, ni vizuri kutozungumza sana kuhusu ngono.
“Lakini hiyo haimaanishi kwamba msizungumze kabisa kuhusu unyumba. Mwenzi wako anahitaji kujua kuwa unatamani kuwa naye kimapenzi,” asema.
Anahimiza watu kujali ikiwa ni sauti na kadhalika wakati wa kushiriki tendo la ndoa, kwani huenda mwenzi wako hatakuwa huru unapofanya hivyo.Mtaalamu huyu anashauri wanandoa kujali wenzi wao wakati wa tendo la ndoa.
Kwa jumla, mshauri huyu anaeleza kuwa mbinu zozote zinazotumika kushiriki unyumba, lazima zizingatie kila mhusika, ili kuhakikisha kuwa si mambo ya kudhalilisha, kuumiza au kuibua hisia zitakazoathiri uhusiano.
Anasema baadhi ya wanandoa huwa wanajipenda sana kuliko wenzi wao.“Ni vizuri mwenzi wako kukufanyia mapenzi kwa mtindo wa ngono unaoupenda; lakini kuwa na haki pia, mfanyie naye mtindo wa ngono anaoupenda,” aeleza Opande.
Hii, asema, inafanya wanandoa kukolezana mahaba.“Kila kitu kinahitaji kuwa kiasi, kukizidisha au kukipunguza kunaweza kuathiri uhusiano wenu. Muhimu kabisa, ni kuwa mbunifu ili kuepuka mazoea yanayofanya ndoa kuwa baridi.”