• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Mtaalamu atoa vidokezo muhimu kuhusu salamu za ma-ex

Mtaalamu atoa vidokezo muhimu kuhusu salamu za ma-ex

NA FRIDAH OKACHI

MWANAMUZIKI wa kufokafoka kutoka mtaa wa Kibra Stephen Otieno Adera almaarufu ‘Stivo Simple Boy’ alikataa kumsalimia mpeziwe wa zamani Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy aliyemtembelea ghafla bila idhini.

Miongoni mwa Waswahili, upo msemo kuwa salamu haigombwi. Nao Waislamu wanafundishwa kwamba ni lazima kujibu salamu. Haya kando, turudi kwa hawa wapenzi wa zamani (ma-ex) wawili.

Vishy na Stivo walikuwa kwa mahusiano ya miaka mitatu. Wawili hao waliachana mwaka 2022. Tangu wakati huo, 2024 imekuwa mara ya kwanza kwao kukutana.

Katika video, Stivo alionekana kutofurahia mazingira hayo ya kujiwa ghafla na Vishy.

Tukio hilo lilijiri wakati Vishy aliingia kwenye nyumba ambayo Stivo alikuwemo na baadhi ya marafiki zake.

Vishy alionekana akionyesha nia yake ya kutaka kumsalimia Stivo.

“Leo nimejileta mwenye kukupa salamu zangu,” alianza Vishy.

Hata hivyo, alikatishwa tamaa huku Stivo akiwa amesalia bila kuitikia, akikunja mikono yake na kutotambua uwepo wake.

“…Njoo unikumbatie. Je, Atieno (ni mpenzi wa sasa wa Stivo) alikuambia usinisalimie?” akauliza Vishy.

Marafiki wa Stivo walishangazwa na kilichokuwa kinaendelea na mmoja wao akataka kufahamu sababu iliyofanya Vishy kufika kumpa salamu.

“Kama ni salamu mbona unalazimisha?” aliuliza rafiki mmoja huku mwingine akisikika akiwa anacheka.

Mtaalamu wa masuala ya ndoa na mahusiano, Bi Mumbi Ngugi, anasema kuwa wakati wa kuvunjika kwa mahusiano kwa wapenzi au wanandoa, wakati mwingine waliokosana huwa na hisia za ugumu na misimamo mikali.

Kuhusu tukio la Stivo kususia salamu za aliyekuwa mpenzi wake Vishy, alisema kuna baadhi ya wapenzi wa zamani ambao huwachukua muda mrefu kukubali yaliyotokea au kuwasamehe wapenzi wao wa zamani na hivyo hukataa chochote kuwahusu, ikiwemo salamu.

“Iwapo Vishy alimpa salamu mpenziwe wa zamani na akakataa, haikuwa na haja ya yeye kusisitiza zaidi. Wakati mwingine, unamzidishia machungu na kumpa kumbukumbu ambazo huenda pengine anajaribu kusahau,” akasema Bi Mumbi.

“Vishy anamchukulia rafiki wa zamani kuwa rafiki yake. Kuachana hakumaanishi kuwa rafiki au mpenzi wa zamani atakuwa adui yako. Mawasiliano ya kawaida na kujumuika pamoja kama kikundi ni sawa lakini kuwepo na mipaka ambayo inapaswa kuheshimiwa pia ni muhimu,” akaongezea mtaalamu huyo.

  • Tags

You can share this post!

Mwanafunzi mwenye ndoto ya urubani aomba msaada wa karo

Kamwene: Makau Mutua amkinga Kalonzo dhidi ya makombora ya...

T L