Pambo

NASAHA ZA NDOA: Mume hutaka utiifu na kudumisha siri ndani ya penzi

Na BENSON MATHEKA March 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANAMUME hutaka mkewe kumheshimu akitarajia mambo kadhaa kutoka kwake.

Mbali na utiifu, mume hutarajia mkewe kutomlinganisha na wanaume wengine na kutotangaza hadharani udhaifu wake au kushindwa kutimiza majukumu yake yakiwemo ya chumbani.

“Makosa ya wanawake wengi ni kuanika udhaifu wa waume wao hata kwa wanaume wengine. Kufanya hivi ni kutomheshimu mumeo na ni kosa ambalo anaweza kuhisi vigumu kukusamehe,” asema mshauri wa masuala ya ndoa, Brian Kibe.

Mwanamke anayefahamu maana ya heshima na manufaa yake kwa ndoa hawezi kumfokea mumewe hadharani au hata faraghani bali huwa anatafuta mbinu za kumrekebisha.

“Wanaume ni viumbe wa ajabu. Hata kama mume amekosa, usimkaripie iwe faraghani au hata mbele ya watu. Kufanya hivyo ni kumkosea heshima na matokeo yake ni hasi kwa ndoa yako,” aeleza Kibe.

Mwanamke anayedumisha heshima kwa mumewe, aeleza, huwa hadharau mafanikio na mchango wake katika jambo lolote bali anautambua na kumtia shime.

Kwa vyovyote vile, usiwahi kufanyia mzaha maumbile ya mumeo au utendakazi wake chumbani.

“Kwa mwanamume, ni kilele cha kukosa heshima kwa mwanamke kutania uume au nderemo zake chumbani. Mwanamke mjanja huwa anaepuka kauli yoyote hasi kuhusu uwezo wa mumewe chumbani,” aeleza Kibe.

Hakuna mwanamume anayetaka kukumbushwa na mkewe jinsi alivyomsaidia kwa pesa kuashiria alimkwamua akiwa na shida.

“Huu ni ukweli mchungu kuhusu wanaume. Hata ukimuokolea jahazi mumeo usiwe unamkumbusha mara kwa mara jambo hilo. Mwanamume huchukulia kwamba unamkosea heshima unapomkumbusha ulivyomsaidia ilhali anawajibikia majukumu yake kwako na kwa familia. Kama mke, epuka hili,” aeleza Kibe.

Mwanasaikolojia Sharon Kemunto anakubaliana na Kibe akisema wanaume huchukulia kukumbushwa walivyookolewa jahazi na wake wao kama dharau.

“Ukisaidia mumeo, sahau na matokeo yatakuwa atachukulia unamheshimu. Ukimkumbusha, anahisi unamdharau,” asema Kemunto. Mwanasaikolojia huyo anasema wanawake wanakosea waume wao heshima kwa kutomakinika wanapozungumza nao na kuzama katika mitandao ya kijamii.

“Kuna dharau mambo leo inayozua tafshani katika ndoa. Mumeo akizungumza nawe, makinika, weka kando chochote unachofanya umsikilize kwa makini. Ukiwa naye chumbani, mpe sikio lako, weka kando mitandao ya kijamii na atachukulia kwamba unamheshimu,” aeleza.

Mbaya zaidi, asema Kemunto, ni mwanamke kuzoea kukataa kumpa mumewe haki yake kwa kusingizia ugonjwa na uchovu au hata wanapotofautiana, na kuwaburudisha wanaume wengine kimapenzi.