Pambo

TUONGEE KIUME: Mwanadada hapendi mistari bila vitendo

Na BENSON MATHEKA May 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUPENDA mwanamke si maneno tu, bali ni vitendo vinavyodhihirisha kile anachoambiwa na mwanamume.

Na mwanamke anathamini kuheshimiwa kwa vitendo. Anapokutana na mwanaume mgeni anayemuita kwa majina ya kimahaba kama ‘mpenzi’, ‘mrembo’, au ‘sweetheart’, humchukulia kwa dharau, kwani huona hiyo ni tabia ya mtu asiye na mipaka, anayetumia maneno hayo kwa yeyote.

Kabla ya kumwambia mwanamke “nakupenda”, mwanaume anapaswa kuelewa uzito wa maneno hayo, maana yake, wajibu unaokuja nayo, na ukweli wake. Mwanamke hapendi kulazimishwa kufungua moyo wake kwa haraka. Anapenda kuchukua hatua kwa hatua, kwa uvumilivu na utulivu — Winnie Kamunde, mtaalamu wa masuala ya mapenzi

Ingawa moyo wa mwanadada unaamini katika mapenzi, anahitaji sababu ya kweli ya kwa nini ampende mtu fulani.Hivyo basi, asema Kamunde, ni kazi ya mwanamume kuthibitisha kwa nini anapaswa kupendwa .

“Kuamsha upendo ndani ya mwanadada anayejithamini, mwenye nia ya kweli si kazi ya siku chache. Kaka, utatoa jasho kabla ya kumuingiza boksi na huyo amekomaa kiakili,” asema.

Kwa mwanadada mpevu, ukweli ni silaha kubwa.

“Mwambie ukweli, hata kama ni mchungu, kwa sababu ukweli huo humfanya akuamini na kukuheshimu zaidi,” aongeza Kamunde.

Mwanamke huchangamkia mwanamume anayemfanya ahisi salama. “Huyu ni mwanaume anayeweza kupatikana akimhitaji licha ya ratiba zake. Mapenzi ya kweli hayafichwi, muonyeshe hadharani kama unavyompenda faraghani,” asema Cidi Wanjiru, mwanasaikolojia na mtaalamu wa masuala ya mahusiano.

Anasema kwamba mwanamke huwa anakita mapenzi kwa moyo wake.

“Ukimtunza vizuri nje ya chumba cha kulala, atajitahidi kukufurahisha ndani ya chumba hicho. Mwanaume mwenye wivu usio na sababu na hofu humchosha mwanamke. Mwanamke anataka mwanaume mwenye ujasiri na uaminifu,” aeleza Wanjiru.

Enzi hizi ambazo wanawake wanapitia au kushuhudia wenzao wakipitia mazito katika mahusiano, kuponya mioyo yao ni kazi ya anayewamezea mate.

“Ikiwa amewahi kukwazwa kimapenzi, si jukumu lako kumhukumu bali kumsaidia kuamini tena katika upendo. Ukweli ni kwamba wanawake wanaogopa kuanza mahusiano ya mapenzi kutokana na waliyopitia awali ya kuvunjwa moyo,” asema Wanjiru.

Kamunde anapendekeza wanaume wasiwe wachoyo wa kumiminia sifa wapenzi wao.

“Mwanamke anapopata sifa zaidi kutoka kwa wanaume wengine kuliko kwako, huumia. Usikose kumpa sifa, heshima na kuthamini mchango wake katika uhusiano wenu na ufanye hivi kwa vitendo,” ashauri Kamunde.

Mshauri huyo anafichulia wanaume siri: “Usibadilike kutoka yule mwanaume mzuri aliyemvutia. Thamani ya mwanaume kwa mwanamke iko pia kwenye uthabiti wa tabia na mapenzi yake.

Mwanamke hutoa kila kitu anapopenda. Usimwache apambane peke yake kuiokoa ndoa au uhusiano wenu. Piganieni penzi lenu pamoja,” aeleza.

Mtaalamu huyu asema mwanamke mwenye upendo wa kweli huleta mabadiliko chanya katika maisha ya mwanaume, huzidisha amani, upendo, baraka na ukuaji wa maisha kwa ujumla.

[email protected]