Pambo

MWANAMKE BOMBA: Pesa, hadhi zisifanye umdharau mumeo

May 28th, 2024 2 min read

NA WINNIE ONYANDO

JUZI, nilimsikia msichana mmoja akisema kuwa hawezi kuolewa na mwanaume aliye na mapato ya chini wakati yeye analipwa mshahara mkubwa.

“Nina pesa, nakutana na watu mashuhuri na ninaishi maisha mazuri. Mbona niolewe na mtu ambaye hana gari au yule ambaye ana mapato ya chini? Mtu kama huyo atanisaidia na nini,” msichana huyo alisema.

Kando na hayo, msichana huyo alisema kuwa hawezi kuacha kazi yake ya uanahabari kwa sababu ya mwanaume.

“Nathamini sana pesa zangu. Siwezi kukubali kudhulumiwa na mwanaume. Kando na hayo, sina muda wa kuanza kumdekeza mwanaume ilahali nina kazi ya kufanya.”

Maneno yake yalinifanya niwaze. Ni wasichana au wanawake wangapi nchini au duniani ambao huanza dharau pindi tu wanapopata pesa au kupandishwa cheo kazini.

Kwa kweli, japo pesa ni sabuni ya roho, haufai kumdharau mume wako na kukosa kutekeleza majukumu yako kama mke nyumbani.

Katika maisha ya sasa, ni jambo la kawaida kuwaona wanawake wakifanikiwa kazini na kupandishwa vyeo.

Hii ni hatua nzuri na inapaswa kusherehekewa kwani inawapa wanawake uhuru wa kifedha na nafasi ya kuchangia maendeleo katika jamii.

Hata hivyo, ni muhimu kwa wanawake kukumbuka kuwa pesa na hadhi hazipaswi kuwa sababu ya kumdharau mwanaume unayeishi naye.

Kwanza, hela na madaraka ni vitu vya muda tu. Leo unaweza kuwa na kazi nzuri na kipato kikubwa, lakini kesho hali inaweza kubadilika.

Upendo na heshima katika ndoa ni mambo yanayodumu milele.

Mume wako, ambaye amekuwa nawe katika dhiki na furaha anastahili heshima na upendo wako bila kujali hali yako ya kifedha au hadhi yako katika jamii.

Pili, mafanikio yako hayapaswi kuwa kipimo cha thamani ya mume wako.

Kumbuka kuwa kila mmoja ni wa maana hasa katika ndoa.

Mume wako anaweza kuwa na kazi duni, lakini mchango wake katika familia na jamii ni kubwa.

Tatu, kumdharau mume wako kwa sababu ya pesa au hadhi ni sawa na kudharau upendo na kujitolea kwake.

Mume wako amekuwa nawe katika kila hatua na safari yako ya mafanikio. Heshimu mchango wake na uonyeshe shukrani kwa yale yote anayofanya kwa ajili yako na familia yenu.

Ni muhimu kuelewa kwamba ndoa ni ushirikiano.

Hivyo, usimdharau mwenzako.

Mwanamke anayemheshimu mume wake hujenga mazingira ya upendo, ushirikiano na uelewano katika familia yake.