• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Ndoa ikikataa imekataa, Akothee ashauri wanawake

Ndoa ikikataa imekataa, Akothee ashauri wanawake

NA FRIDAH OKACHI

MWANAMUZIKI Esther Akoth Kokeyo almaarufu Akothee, amewashauri wanawake dhidi ya kusalia kwenye ndoa ambazo huwa tayari zimeonekana haziwezi kudumu.

Kwenye ujumbe aliopakia katika majukwaa ya mitandao ya kijamii, Akothee alisikitika kuwa wanawake wengi wamekuwa wakipoteza maisha sababu ikiwa ni kushikilia kisichowezekana.

Hata hivyo aliwashauri walioolewa kuwa tayari kujiondoa kwa ndoa zao, mara zikianza kuyumbayumba.

“Uchungu wa mwanamke kumpoteza mume kwa mwanamke mwingine au kwa ulimwengu, unahitaji uchunguzi wa kina. Lakini itachukua miaka, hivyo maoni yangu ni kwamba kadri unavyoondoka mapema, ndivyo inavyokuwa bora kwako,” akasema Akothee.

Akothee,43, alisema ni vyema mwanamke arudi nyumbani kwa wazazi wake akiwa hai kuliko kupoteza maisha wakati anapigania ndoa yenye matatizo.

“Nimeona wanawake wakipoteza maisha kwa jina la kupigania ndoa zao zifanye kazi. Afadhali aje nyumbani ndani ya matatu na sio juu ya matatu. Rudi nyumbani na jina Esther Akoth Kokeyo badala ya ‘mwili unawasili kesho,” akashauri.

Mama huyo wa watoto watano alisema kuwa wanawake wengi wamewapoteza waume zao duniani, akimaanisha kuwa wapo hai ila hawatekelezi majukumu yao.

“Wanawake wengi wana waume waliokufa katika miili ilio hai… Maumivu ya kufiwa na mume ni ya kuumiza sana, lakini angalau unapata hitimisho unapopita na kumuona pale kando ya nyumba,” aliendelea.

Mfanyabiashara huyo anafahamika na wengi kuwa kwenye mahusiano au ndoa tano. Ndoa ya mwisho ni ile aliyofunga pigu za maisha na Denis Schweizer almaarufu ‘Omosh’ na kuachana naye baada ya miezi miwili.

Kwenye ukurasa wake mapema mwaka 2023 alimshukuru bintiye Rue Baby aliyekuwa akifuatilia maisha yake baada ya harusi na kumfuata kila alipokuwa akienda bila kufahamu.

  • Tags

You can share this post!

Kibarua cha kukabiliana na janga la ulevi Mlima Kenya

Super Eagles wa Nigeria watamla ndovu Cote d’Ivoire...

T L