Pambo

PAMBO:Jifunze sanaa ya kupanga mume

Na BENSON MATHEKA May 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA safari ya ndoa au mahusiano ya kudumu, wanawake mara nyingi hujifunza mbinu nyingi za kutunza nyumba, kulea watoto, au hata kufanya kazi kwa bidii.

Lakini kuna kipengele kimoja muhimu kinachopuuzwa na wengi- sanaa yakupanga mume.

Hili halihitaji  ujanja au hadaa.  Linahitaji hekima, heshima, na mapenzi ambayo hujenga uhusiano imara na wa kuridhisha  pande zote mbili.

“Kupanga mume kunamaanisha kumfahamu, kumthamini, na kumgusa kwa njia ambazo humfanya kuwa karibu nawe kimwili, kihisia, na kiakili,” asema mtaalamu wa mahusiano na mshauri wa wanandoa, Veriane  Kiruki

Ngono, asema, si haki tu ya ndoa, bali ni njia ya mawasiliano ya kina kati ya wanandoa. “Wakati mwingine, mwanamume huhitaji tu kuguswa ili apone kiakili. Kumpa mapenzi kwa hiari, kwa joto la upendo na bila masharti, kunamweka katika hali ya utulivu na furaha. Usisubiri aanzishe kila mara – unapoanza wewe, anakuheshimu zaidi,” aeleza.

Hakuna mwanaume anayetaka kurudi nyumbani na kukaribishwa kwa lawama, kelele au mashambulizi ya maneno. Nyumba iwe hifadhi yake ya amani, mahali ambapo anahisi salama na anapenda kurudi. Mazungumzo ya busara, subira na hekima ni silaha kubwa ya mwanamke mwerevu.

Kiruki asema kama vile  wanawake hupenda kuulizwa walivyolala au jinsi siku yao ilivyokuwa, vivyo hivyo waume nao wanahitaji hilo. “Maswali madogo kama, “Ulikula vizuri?” au “Kazi iliendaje leo?” yanamaanisha mengi zaidi ya unavyodhani,” asema.

Kulingana na  wataalam, mwanaume mwenye mawazo huwa na wakati mgumu kupanga mambo yake. Msaada mdogo kama kumsaidia kupanga mavazi, kupanga ratiba yake au kumkumbusha ahadi fulani kunaweza kumwondolea mzigo mkubwa wa akili.

“Unamjua kwa undani – changamoto zake, maamuzi yake magumu, na ndoto zake. Sala zako ni silaha ya nguvu. Mwombee kwa moyo, na mwambie unamwombea. Hili linamgusa hata kama hakuonyeshi mara moja,” asema mshauri wa masuala ya ndoa Kenn Kiambi.

“Usimwache mumeo abebe mzigo wa kifedha peke yake. Kama unaweza kuchangia, fanya hivyo. Kama si kwa pesa, basi kwa kupunguza gharama zisizo za lazima, kusaidia kupanga bajeti, au kuwa mbunifu kwenye matumizi ya familia,” aeleza.

Mwanaume pia hupitia vipindi  anavyojiona kuwa hafai au kuchoka.  “Katika kipindi kama hiki, mthibitishe kwa maneno yenye heshima na mapenzi: ‘Najivunia kuwa na wewe’, ‘Ninaamini unaweza’. Haya ni mafuta ya moyo wake,” asema Kiambi.

Anasema uaminifu si wa kimwili tu – bali pia wa hisia. “Epuka siri zisizokuwa na maana, zungumza kwa uwazi na mume wako, na mpe amani ya moyo. Usaliti ni sumu inayovunja kabisa uaminifu na usalama wa moyo wa mwanaume,” aeleza.

Mwanaume anapopata nafasi ya kuzungumza, asema Kiruki, huwa ni fursa ya dhahabu. Hivyo,  usimkatize, usimchekelee, na usitumie udhaifu wake dhidi yake baadaye. Kuwa ngome yake ya usiri na faraja.

“Na usipuuze nguvu ya tabasamu lako. Ni dawa ya uchovu wake, ni alama ya kukaribishwa nyumbani, na ni mwanga wa moyo wake. Tabasamu linaweza kubadilisha siku nzima kuwa nzuri,” ashauri.

Busu si kwa wapenzi wapya tu. Katika ndoa, busu ni muhuri wa upendo unaoendelea. Mbusu asubuhi, kabla ya kulala, wakati wa shukrani – kila mara kuna nafasi ya kuonyesha upendo bila maneno.

Mambo mapya huleta msisimko katika uhusiano. Tembeeni sehemu mpya, pikeni pamoja, angalieni sinema, chokozaneni, chekeni hadi mjilize. Hii huimarisha uhusiano na kuongeza ukaribu wenu.

Kupanga mume, asema Kiambi, si sawa na kumbadilisha, bali ni kumwezesha kuwa bora zaidi kwa msaada wako. Ni kumpenda kwa vitendo, kwa hekima na kwa moyo wa kweli. Katika dunia yenye msukosuko, kuwa kimbilio lake .na atakuwa ngome yako.