Shauri yako ukiachilia mpenzi mwenye sifa hizi
KATIKA dunia ya sasa ambapo mapenzi yamejaa mashindano ya nani ana pesa zaidi, nani ana sura na umbo nzuri zaidi, au nani ana gari ya kisasa, mtu asiyemezea vitu ulivyonavyo, anayekupenda jinsi ulivyo ni zawadi ya thamani isiyo na kifani.
Usimpuzie mtu kama huyu katika mapenzi.
“Huyu si mtu wa kuangalia “CV” yako ya maisha elimu, kazi, au familia. Huyu ni mtu anayekupenda jinsi ulivyo, pamoja na mapungufu yako. Anakusikiliza bila kukuhukumu, anakuombea bila kukuambia, na anakuinua bila kutaka sifa, asema Dkt Sue Johnson, mtaalamu wa saikolojia na mahusiano.
“Mapenzi ya kweli ni yale yanayotoa mazingira salama ya kihisia ambapo mtu anaweza kuwa yeye mwenyewe bila hofu ya kuhukumiwa.”
Katika mahusiano, mtu wa aina hii ni nguvu unayoihitaji unapolegea, mwanga wa kukuongoza unapopotea, na kioo kinachokukumbusha thamani yako pale unapovunjika moyo.
“Huyu ni mtu anayekutambua zaidi ya majina uliyoitwa na dunia. Anakuhimiza usikate tamaa, anakukumbusha kwa upendo uwezo wako wa ndani, na huamini katika ndoto zako hata wakati wewe umeanza kuziweka kando,” asema Sue.
Brene Brown, mtafiti maarufu wa ujasiri wa kihisia, anasema: “Kila mtu anastahili mtu ambaye anaweza kukaa naye katika giza, bila kulazimisha kuleta mwanga, bali kuwa mwanga wa karibu tu.“
Huyu ni mtu ambaye unahisi huru kuwa mkweli kwake, unaweza kumwambia unaposhindwa bila aibu, na kushiriki naye mafanikio yako bila woga.
Katika mapenzi, watu kama hawa huwa si wa muda mfupi. Wao ni msingi wa mahusiano ya kudumu. Watu ambao hawakimbii wakati wa dhoruba, bali hukufunika kwa sala, kukutia moyo, na kuhimiza mabadiliko ya kweli. Wao ni wale wanaosema, “Sioni tu ulipo sasa, bali naona kule unaweza kufika.”
“Usimpuzie mtu kama huyu,” asema Brene. Badala yake, mpe nafasi ya kukuonyesha kuwa mapenzi ya kweli bado yapo. Jifunze pia kuwa mtu wa aina hii, anayependa kwa kina, anayesamehe kwa haraka, na anayejenga badala ya kubomoa.
“Mtu mwenye mapenzi ya kweli anakupenda kwa sababu ya mwanga anaouona ndani yako, si kivuli kinachokuzunguka,” asema Sue, akinukuu msemo maarufu kuhusu mahusiano ya mapenzi.
Katika mapenzi ya kweli, mwonekano wa nje huja na kuondoka. Lakini mtu anayekupenda kwa moyo, kwa maono na kwa maombi, ni wa kudumu.
“Usimpuzie mtu huyu. Anaweza kuwa ndiye msaada wa hatima yako, na pengine, wewe pia unapaswa kuwa huyo kwake.”
Katika dunia inayotufundisha kupanda juu kwa kutumia, kuporomosha na kugandamiza wengine, kuwa mtu wa kuinua mwenzako ni tendo la kishujaa. Na kama umebahatika kuwa na mtu wa aina hii maishani mwako mshike vizuri.
Kuna watu wanaokuja kwa maisha yako kwa muda, wengine kwa maslahi, lakini mtu anayesimama nawe katika kila hatua, hata ukiwa chini kabisa, ni zawadi ya nadra.
“Watu wa aina hii hawapatikani mitaani au kwenye mitandao ya kijamii. Wanapatikana katika mazungumzo ya kina, katika hali ngumu, na katika safari ya maisha yenye changamoto,” asisitiza Brene