Sheria: Ukipewa talaka hauwezi kurithi mali ya marehemu mumeo au mkeo
KUMEKUWA na visa vya watu kuzozania mali ya watu wanaoaga dunia au mali kutajwa kuwa ya marehemu na hivyo kuzua mgogoro ambao kisheria haufai.
Makala ya leo yanalenga kufafanua mahitaji ya mume au mke kurithi mali ya marehemu lakini nitaanza kwa kurejelea haki ya kurithi mali kwa uwazi zaidi.
Kwanza, marehemu hana haki ya kumiliki mali na ndio sababu watu wanashauriwa kuacha wosia wakieleza wanavyotaka mali yao isimamiwe au kugawa na wanaopaswa kunufaika.
Mtu hukoma kumiliki mali akifariki.
Baada ya kifo, mali hupitishwa kwa warithi wake au serikali, kulingana na hali.
Wosia huwasilisha matakwa ya mwisho ya mtu kuhusu mali na wanaopaswa kunufaika baada ya kifo chake. Wosia unaonyesha jinsi mali ya mtu huyo itakavyogawanywa baada ya kifo chake, ukibainisha ni nani atasimamia mali hiyo ikiwa ni pamoja na fedha,hadi itapogawanywa.
Katika wosia wake, marehemu anaweza kutaka mali yake ihifadhiwe kwa watu waliokuwa wakimtegemea au igawe kwa watu wa familia yake, kikundi, au itolewe kama hisani.
Pale ambapo marehemu anakosa kuacha wosia, ni mumewe au mkewe na watoto (ikiwa wapo) au jamaa wa karibu walio hai huku wazazi wakipatiwa kipaumbele wanaorithi mali hiyo.
Hata hivyo, mtu aliyekuwa akimtegemea marehemu anaweza kuomba mahakama arithi sehemu ya mali iwapo anaamini kupuuzwa iwe katika wosia au mali inaporithiwa.
Sheria inafafanua watu waliokuwa wakitegemea marehemu kuwa mke au wake wa zamani na watoto wa marehemu.
Kwa mujibu wa kifungu 160 cha Sheria ya Urithi,watu wanaoweza kurithi mali ya marehemu ni mke au wake zake, mke au wake wa zamani, watoto wa marehemu ikiwa walikuwa wakitunzwa marehemu kabla ya kifo chake; wazazi wa marehemu, wazazi wa kambo, babu, wajukuu, watoto wa kambo, watoto ambao marehemu aliwachukua katika familia yake kwa kama wake, kaka na dada, na kaka na dada wa kambo, waliokuwa wakitunzwa na marehemu kabla ya kifo chake.
Iwapo marehemu alikuwa mwanamke, mtu wa kwanza kunufaika na mali yake ni mumewe ikiwa alikuwa akitunzwa naye kabla ya tarehe ya kifo chake.
Hata hivyo, mtu hawezi kurithi mali ya marehemu, kama mke au mume, ikiwa alikuwa ameachana na marehemu au ndoa hiyo ilikuwa imevunjwa kwa njia halali wakati wa uhai wa marehemu.
Kwa hiyo, ili kuzingatiwa kurithi mali ya marehemu kwa misingi ya ndoa, ushahidi wa ndoa unapaswa kuthibitishwa kwamba ilikuwepo pindi kabla ya kifo cha marehemu. Ushahidi huo unaweza kuwa kwa njia ya cheti halali cha ndoa.