Pambo

Sheria zinazowalinda wajane dhidi ya ubaguzi, unyanyasaji

Na  BENSON MATHEKA April 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAJANE wengi nchini wanapitia maisha magumu, ubaguzi, umaskini na kukosa haki. Baada ya kumpoteza mume baadhi hukumbana na hali za kutamausha ikiwemo kufukuzwa katika nyumba zao za ndoa, kunyimwa malezi ya watoto, au hata kushutumiwa kwa kusababisha kifo cha waume wao.

Kwa wengine, hasa wanaotoka jamii zinazofuata mila zilizopitwa na wakati, wanalazimishwa kuolewa tena kupitia mila ya “urithi wa mjane” – tendo la kutwaliwa na ndugu wa marehemu kama mke – bila hiari yao.

Ripoti ya World Widows Report 2015 inakadiria kuwa kuna wajane 8 milioni nchini Kenya. Wengi hawana ulinzi wa kisheria wala njia rahisi za kupata haki, hasa vijijini ambako mila bado zinatamalaki kuliko sheria.

Katiba ya Kenya inalinda haki za kila mtu – wakiwemo wajane. Kifungu cha 27 (Sura ya 4 – Haki za Kimsingi) kinasema watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanapaswa kulindwa kwa usawa.

Pia, Katiba inapiga marufuku ubaguzi wowote – ikiwemo kwa misingi ya jinsia au hali ya ndoa.Kifungu 45 (3) kinasema kuwa wanandoa wote wana haki sawa wakati wa ndoa, ndani ya ndoa, na hata ndoa inapovunjika.

Hivyo, mke ana haki sawa na mume katika mambo yote ya ndoa. Sheria ya Ndoa (2014) inasisitiza kuwa ndoa zote lazima zisajiliwe. Ndoa iliyosajiliwa inampa mjane utambuzi wa kisheria kama mke halali wa marehemu – jambo muhimu kwa yeye kupata haki zake baada ya kifo cha mume, hasa kuhusu mali ya ndoa.

Sheria ya Mali ya Ndoa (2013) inaeleza mali ya ndoa ni nini, na inatoa ulinzi kwa mjane kuhusu umiliki wa mali hiyo. Inasema wazi kuwa mume na mke wana haki sawa katika ununuzi, matumizi, usimamizi na hata uuzaji wa mali ya ndoa.

Kwa hivyo, baada ya mume kufariki mjane hapaswi kufukuzwa wala kunyimwa mali aliyochuma pamoja na mumewe.Sheria ya Urithi ndiyo sheria inayosimamia ugavi wa mali ya mtu aliyefariki.

Iwapo mume hakuacha wosia, mjane ana haki ya kupata mali iliyomo nyumbani (vitu vya matumizi ya kibinafsi na familia), na pia “haki ya matumizi” ya sehemu ya mali iliyosalia. Hii ina maana kuwa anaweza kuendelea kutumia na kufaidika kutokana na mali hiyo ili kudumisha hali ya maisha aliyozoea.

Pamoja na kuwepo kwa sheria hizi, changamoto zinazokabili wajane bado ni tele.Sheria nyingi hazitekelezwi ipasavyo hasa maeneo ya mashambani ambako watu hawajui haki zao na mila bado zinatawala.

Aidha, baadhi ya vifungu vya sheria vina kasoro. Mfano ni uamuzi wa hivi karibuni wa Mahakama Kuu uliobatilisha kifungu cha Sheria ya Urithi kilichobagua wajane wa kike.

Kifungu hicho kilisema haki ya mjane wa kike kutumia mali ya marehemu inafika kikomo iwapo ataolewa tena, lakini hakikuathiri mjane wa kiume anayetumia mali ya marehemu mkewe na ameoa tena.