Talaka haihusu wanandoa kuachana pekee, mali pia huzingatiwa
TALAKA nchini Kenya si suala la kuvunja ndoa pekee, bali pia linahusisha haki za kifedha, makazi na ugavi wa mali kati ya wanandoa.
Kwa mujibu wa sheria, mwenzi mmoja anaweza kupewa posho la kifedha baada ya talaka iwapo atathibitisha kuwa hawezi kujitegemea kimaisha.
Hata hivyo, uamuzi wa mahakama hutegemea hali ya kila kesi.
Katika kuamua masuala ya posho na mali, mahakama huzingatia mambo kadhaa, ikiwemo muda ambao ndoa ilidumu, kipato na majukumu ya kifedha ya kila mwenzi, kiwango cha maisha walichoishi wakati wa ndoa, pamoja na mwenendo wa wanandoa husika.
Lengo ni kuhakikisha haki na usawa, bila kumpendelea yeyote.
Katika miaka ya hivi karibuni, maamuzi ya mahakama yameanza kufafanua wazi sheria za talaka, hasa kuhusu ugavi wa mali ya ndoa.
Uamuzi wa kihistoria katika kesi ya JOO dhidi ya MBO, iliyosikilizwa na Mahakama Kuu mnamo Januari 2023, uliweka bayana kuwa wanandoa hawana haki ya moja kwa moja ya kugawana mali ya ndoa kwa asilimia 50 kila mmoja.
Mahakama ilisisitiza kuwa ugavi wa mali unapaswa kuzingatia mchango wa kila mwenzi, iwe ni wa kifedha au usio wa kifedha kama vile malezi ya watoto na kazi za nyumbani.
Uamuzi huu ulilenga kuzuia hali ambapo mtu anaweza kupata mali bila mchango wowote, jambo ambalo linakiuka haki ya umiliki wa mali inayolindwa na Katiba.
Aidha, Mahakama ilieleza kuwa Sheria ya Mali ya Ndoa ya mwaka 2013 haitumiki kwa kesi za ndoa zilizovunjika kabla ya mwaka 2014, huku ikithibitisha kuwa kifungu cha Katiba kinachozungumzia usawa wa wanandoa kinatumika kulingana na mchango uliothibitishwa, si ugavi wa lazima wa nusu kwa nusu.
Katika kesi nyingine ya MWM dhidi ya JMM iliyowasilishwa mwaka 2023, Mahakama Kuu ilionyesha umuhimu wa kulinda mali ya ndoa kesi ya talaka ikiendelea.
Mahakama ilitoa amri ya muda kumzuia mmoja wa wanandoa kuuza au kuhamisha mali inayodaiwa kuwa ya ndoa hadi kesi isikizwe na kuamuliwa kikamilifu.
Uamuzi huu uliimarisha msimamo kwamba mahakama iko tayari kuingilia kati ili kuzuia dhuluma au hasara isiyorekebishika.
Mwaka 2024, katika kesi ya MWK dhidi ya JKK, mahakama ilisisitiza kuwa umiliki wa kweli wa mali ya ndoa hauamuliwi na jina lililoandikwa kwenye hati ya umiliki pekee.
Mali iliyosajiliwa kwa jina la mume ilibainika kununuliwa kwa juhudi za mke pekee, na mahakama ikaamua kuwa mume alikuwa akishikilia mali hiyo kwa niaba ya mke. Hivyo, aliamriwa kuhamisha umiliki.
Hivi majuzi zaidi, kesi ya WW dhidi ya JMM ya mwaka 2025 ilionyesha kuwa mahakama inalinda haki ya makazi ya wanandoa hata kabla ya talaka kuamuliwa.
Mahakama ilitoa amri ya muda kuzuia uuzaji wa nyumba ya ndoa na ikaagiza wanandoa waendelee kuishi humo kwa mpangilio maalum hadi kesi itakaposikilizwa kikamilifu.
Kwa jumla, maamuzi haya yanaonyesha mwelekeo mpya katika sheria za talaka nchini Kenya, ambapo msisitizo uko kwenye haki, mchango halisi na ulinzi wa maslahi ya kila mwenzi.