TUONGEE KIUME: Tendo la ndoa kila siku linachosha
KATIKA maisha ya ndoa, ni kawaida kwa wanandoa kupitia vipindi tofauti vya kihisia na kimwili.
Moja ya mambo ambayo mara nyingi huibua maswali na wasiwasi katika uhusiano wa ndoa ni kupungua au kukosekana kwa hamu ya kufanya mapenzi.
Hili si jambo la ajabu wala la aibu, bali ni hali ya kawaida inayoweza kutokea kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kiakili, kihisia, au hata kimwili.
Katika jamii nyingi, kuna dhana potofu kuwa kupungua kwa tendo la ndoa ni dalili ya kupungua kwa mapenzi. Hili si kweli. Mtu anaweza asiwe na hamu ya kufanya mapenzi lakini bado anampenda mwenzi wake kwa dhati.
“Mtu hawezi kuwa na hamu ya kufanya mapenzi kila wakati, lakini hiyo haimaanishi kuwa hapendi mwenzi wake. Mapenzi yanategemea hisia na kwa binadamu yeyote zinaweza kukosa,” asema Frederina Akech, mtaalamu wa masuala ya ndoa na mahusiano ya mapenzi.
Anasema kuwa mapenzi ya kweli hayawezi kupimwa kwa mara ambayo wachumba wanafanya tendo la ndoa.
“Ni zaidi ya tendo, ni ukaribu wa kihisia, heshima, na kujaliana,” asema na kuongeza mtu anaweza kupatia mwenzi tendo la ndoa kila siku bila hata heshima na iwe ni kujitesa.
Anasema kupungua kwa hamu ya kufanya mapenzi kunaweza kuchangiwa na mambo mbalimbali, kama vile msongo wa mawazo na shughuli nyingi za kila siku, mabadiliko ya homoni hasa kwa wanawake baada ya kujifungua au wakati wa hedhi, matatizo ya kiafya kama kisukari, shinikizo la damu, au msongo wa mawazo, ugomvi au kutoelewana, uchovu wa mwili au ukosefu wa usingizi.
“Kwa hivyo, ni muhimu kwa wanandoa kuelewa kuwa hali hii haipaswi kuchukuliwa kama tishio kwa ndoa, bali kama changamoto inayohitaji mawasiliano, uvumilivu, na msaada wa pamoja,” asema Akech.
Kulingana na mtaalamu masuala ya ndoa Joan Kiama ni vigumu kwa mwenzi mmoja kuelewa hali ya mwenzake ikiwa hakuna mawasiliano ya wazi.
“Kukaa kimya kuhusu hisia, au kulazimisha tendo la ndoa bila kuzingatia hali ya mwenzako, kunaweza kuharibu uhusiano. Wakati mwingine mtu huhitaji kuwa peke yake binafsi, kutafakari, kutulia na kujijenga upya. Hivyo basi, kuna haja ya mtu kuelewa kuwa mwenzi wake si roboti ya kimapenzi, bali binadamu mwenye hisia, mahitaji ya kiakili na wakati mwingine anahitaji kupumzika,” asema Kiama.
Mtaalamu huyu anasema mafanikio ya ndoa hukitwa katika uwezo wa mume na mke kufundishana, kusikilizana, na kuwa tayari kujifunza kila siku namna ya kuboresha uhusiano wao.
Hivyo basi, asema Kiama, kukosa hamu ya kufanya mapenzi si mwisho wa ndoa.
“Ni changamoto inayoweza kushughulikiwa kwa mawasiliano, uvumilivu na uelewano. Badala ya kuhukumu au kujihisi kunyimwa haki, wanandoa wanapaswa kujenga utamaduni wa kuzungumza kwa uwazi, kuonyeshana mapenzi kwa njia tofauti, na kuthibitishiana kuwa upendo wao ni wa kweli, hata kama si kila wakati watakuwa na hamu ya kuburudishana kimwili. Tendo la ndoa sio ugali eti ukikosa kila siku utakufa,” asema.