Tija ya kusimama na mchumba wako nyakati za hali ngumu
KATIKA maisha ya ndoa au uhusiano wa kimapenzi, si kila siku huwa ya furaha na tabasamu. Kuna nyakati ambapo hali huwa ngumu, majaribu huzuka, na mioyo hushikwa na mashaka. Katika nyakati hizo, jambo moja dogo linaweza kuleta tofauti kubwa: hakikisho kutoka kwa mpenzi wako.
Hakikisho ni ile sauti ya upole inayomwambia mwenzi wako, “Bado niko hapa. Nakupenda. Sikutoroki.” Na mara nyingi, hakikisho linahitajika si kwa sababu mtu hajui, bali kwa sababu anahitaji kusikia tena. Kumhakikishia mwenzi wako kunaweza kuokoa na kuimarisha uhusiano wenu.
“Watu wengi huachwa na wapenzi wao wanapopoteza chanzo cha mapato iwe ni kazi, biashara au fedha. Wengi huingiwa na hofu ya kuachwa. Kwa upendo, mhakikishie mtu wako, mwambie mapato yake si sababu ya wewe kuwa naye. Ni yeye unayethamini. Katika hali hiyo, hakikisho huwa tiba ya hofu isiyoelezeka,” asema Judy Kwamboka, mwanasaikolojia na mtaalamu wa masuala ya mahusiano.
Anasema kila uhusiano hupitia migogoro. Lakini hata mnapogombana, ni muhimu kumwambia mwenzi wako kuwa tofauti zenu hazibadili msingi wa upendo wenu.
“Mwambie ingawa tumetofautiana kwa sasa, bado ni wewe niliyechagua. Na bado niko hapa.”Mabadiliko ya mwili, aeleza Kwamboka, huja kwa sababu nyingi kama vile ujauzito, ugonjwa, ajali au hata umri.
Katika nyakati hizo, mwenzi wako anaweza kuhisi kutovutia au kukosa thamani. Hapo ndipo unapohitajika kumwambia kwako, yeye angali sawa na mabadiliko hayabadili namna unavyompenda.Watoto wanapofanya makosa, mzazi mmoja anaweza kuonekana kana kwamba ndiye wa kulaumiwa.
“Usimwache ahisi hivyo peke yake. Mwambie: “Hili si kosa lako. Tuko pamoja. Hatutakata tamaa na watoto wetu.”“Kuna wakati mchumba wako anahisi wivu au kutokuwa salama kutokana na mahusiano yako na marafiki au familia. Huu si wakati wa kumlaumu mchumba wako, bali wa kumtoa hofu. Mwambie wewe si wa kushindana na yeyote. Nafasi yako moyoni mwako haijaguswa,” asema Kwamboka.
Kulingana na mtaalamu wa masuala ya mapenzi Jane Muthoni, kila mtu hufanya makosa. Lakini makosa hayo yasipokabiliwa kwa upendo, huweza kuvunja kabisa uhusiano. “Ukiumia, sema ukweli wako lakini pia ongeza hakikisho: Ndiyo, nimeumizwa. Lakini sijakata tamaa. Bado nakutaka.Hilo peke yake huweza kumfanya ajutie kwa dhati na kubadilika,” asema Muthoni.
Kuna nyakati mchumba wako atauliza maswali yanayohitaji hakikisho: “Bado unanipenda?” “Bado nakuvutia?” Maswali haya yasiwe chanzo cha kero. Ni mlango wa ukaribu zaidi. Yajibu kwa moyo wako wote, anasema.Mshauri huyu anatahadharisha watu dhidi ya kukemea wachumba wao wakijikwaa wakati wa shughuli chumbani.
“Si kila wakati wa shughuli chumbani huwa kamilifu. Kuna nyakati mambo hayaendi kama ilivyotarajiwa. Badala ya kumkosoa au kumbeza, mpe mwenza wako hakikisho: Sawa. Haimaanishi kuwa hatupendani.Mahusiano ya kweli yanajengwa katika uelewano, si ukamilifu.Katika kila ndoa au uhusiano, asema Muthoni, hakikisho ni kama mbolea kwenye mmea wa upendo.
Hauhitaji kusubiri matatizo ndipo uanze kusema, “Ninakupenda.Sema hivyo kila wakati. Sema hasa wakati ambapo moyo wa mchumba wako unaumia. Mhakikishie yeye ndiye wako na wewe ni wake,” asema.