Pambo

Tusifumbie macho ukweli kwamba wapo kinadada wanaotumia ndoa kama kitega uchumi

Na PAULINE ONGAJI December 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HIVI majuzi mwanasoka Achraf Hakimi kutoka Morocco, anayechezea klabu ya kabumbu ya Paris Saint Germain, nchini Ufaransa, alituzwa taji la kambumbu.

Ushindi huu ulinikumbusha tukio la miaka kadhaa iliyopita ambapo mwanasoka huyu aligonga vichwa vya mtandaoni, baada ya mkewe, Hiba Abouk, kumtaliki.

Lakini bibi huyo alipigwa na butwaa baada ya ombi lake la kutaka kugawiwa nusu ya mali ya mumewe kugonga mwamba, ilipobainika kwamba Hakimi hakuwa na chochote kwani mali na pesa zake zote alikuwa ameziandikisha kwa mamake.

Ni kisa kilichoibua mjadala mkali mtandaoni huku washauri na wataalam wa mahusiano wa kweli na uwongo wakichipuka kila mahali kudadisi kisa hiki.

Hasa nakumbuka kaka huyu mmoja kutoka Nigeria aliyeonekana kukerwa sana na hatua ya mwanasoka huyo, huku akimshutumu kwa kutomuamini mkewe.

“Hatupaswi kumshabikia Hakimi kwa kumhadaa mkewe. Ikiwa haumuamini kwa nini umuoe?” aliuliza.

Nakubaliana naye kwamba kama wanandoa mnapaswa kuaminiana kwa mambo yote ya uhusiano wenu, lakini kumbuka kwamba kuna baadhi ya watu ambao wamebobea kwa kuficha tabia zao kamili, ambazo huanza kujitokeza baada ya ndoa.

Kunao wanaosema kwamba kumficha mkeo mali ni upumbavu na nakubaliana nao, lakini je ikiwa umegundua kuhusu pupa yake baada ya kumuoa?

Hayo kando, ni mara ngapi hata humu nchini umesikia visa vya wake kuwaua waume wao na kuachwa na mali kuambatana na sheria? Hata kuna waume wanaowaua wake wao na kusalia na mali.

Kisha kama Waafrika kidogo tunapaswa kujitenga na hizi itikadi za kigeni zinazokulazimu kuvunja mwunganisho na jamaa zako baada ya kuoa au kuolewa.

Hebu fikiria hasa katika muktadha wa zamani ambapo kwa mfano mali na rasilimali za familia zingeuzwa ili mtoto mvulana mkubwa aende shuleni.

Kisha, baada ya kusoma na kupata ajira kubwa kaka anaoa na kulazimika kuvunja uhusiano hata na wazazi wake waliomlea na sasa kumakinika na mtu ambaye amekutana naye tu!

Pia, tusifumbie macho ukweli kwamba kuna wanawake wanaotumia ndoa kama kitega uchumi na kamwe hawajui kutia bidii ila kunyemelea mali ya mwanamume.

Kuna wanaume wanaopoteza kila kitu kwa wanawake hata baada ya kufanya kazi kwa miaka na vikaka.

Hiyo kamwe sio haki.

Wanasoka kama vile Tendai Ndoro na Emanuel Eboue, wameishia kusalia kwa uchochole baada ya kupokonywa kila kitu na wanawake ambao ni wake wao.

Ikiwa una kaka, una mtoto wa kiume au umewahi shuhudia mwanamume akinyang’anywa jasho lake kwa msingi wa ndoa, utaelewa hatua ya dume huyu na wala sio kuropokwa na kumtusi kiholela.