Pambo

MAPENZI: Uaminifu hupimwa wakati nafasi ya usaliti ipo!

Na BENSON MATHEKA July 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA ulimwengu wa sasa, vishawishi vya kimapenzi vimejaa kila kona.

Kila siku, mwanamume anakumbana na wanawake wa kila aina – vijana zaidi, wa kuvutia zaidi, wa kisasa zaidi, walio tayari kuonyesha mapenzi au hisia zisizo za dhati.

Kila siku utaona mwanamke mwenye umbo linalokuvutia zaidi ya mke au mchumba wako, au anayesema unachotaka kusikia.

Lakini, hilo si jambo jipya.

Ukweli ni kwamba, kila siku ni nafasi ya kumsaliti mpenzi wako – lakini kila siku pia ni nafasi ya kuthibitisha uaminifu wako.Kuna siku mpenzi wako atakuwa na huzuni, yuko mbali, hana muda wako, au hata amekukasirisha.

Katika siku hizo ndipo jaribu linakuja – lakini pia ni wakati ambao tabia yako ya kweli hujitokeza.

Uaminifu haupimwi wakati mambo ni mazuri – hupimwa wakati nafasi ya kusaliti ipo, lakini unaamua kutofanya hivyo.

“Usaliti si ushindi – ni udhaifu,” asema mwanasaikolojia Jane Wamwende.

“Wanaume wengi huamini kuwa kutoka nje ya ndoa au uhusiano ni ishara ya “kuwa mwanaume kamili”. Huu ni uongo mkubwa unaoangamiza familia, kuharibu imani, na kuvunja heshima binafsi,” asema na kuongeza kuwa kumsaliti mke wako au mpenzi wako si ushahidi wa nguvu zako – ni dalili ya kutoweza kujizuia, yaani udhaifu wa maadili.

“Kumbuka thamani ya yule uliye naye,” asema Wamwende.Kulingana naye, mwanamke uliye naye sasa si kwamba hana kasoro.

“Lakini yule mwingine unayemwona kama “bora zaidi” pia ana kasoro zake ambazo hujaziona bado. Usitupilie mbali uaminifu na historia yenu kwa ajili ya raha ya muda mfupi. Mwanamume wa kweli hujua kutunza kile alichonacho na kuheshimu ahadi alizotoa,” ashauri.

Wataalamu wanasema ni kweli wanaume wana udhaifu wa mahitaji ya kimwili na kihisia. Lakini mahitaji hayo ni bora zaidi yanapotimizwa kwa uaminifu.

Ngono isiyo na dhamira hutoa raha ya muda mfupi, lakini huacha maumivu ya ndani yasiyopona kirahisi – kwa upande wako, kwa mpenzi wako na hata kwa familia yako.

“Jifunze kusema hapana, kujiheshimu na kujithamini,” asema mwanasaikolojia Tony Kimani.

“Hata kama hakuna mtu atakayejua, hata kama nafasi ni ya kipekee, jifunze kusema hapana. Mwanaume wa heshima huweza kusimama imara na kusema, “Nina mpenzi, nina mke wangu na simsaliti.”

“Hapo ndipo kuwa mwanamume kweli huonekana,” asema.

Kimani asema kuwa mwanamume mwaminifu kunadhihirisha busara.“Siku hizi, asema, jamii imejaa wanaume wanaoanguka kwa vishawishi vidogo.

Lakini bado wapo wanaume wanaoamua kuwa waaminifu, wanaotambua kuwa mapenzi ya kweli na heshima hujengwa kwa uaminifu wa kila siku.

“Chagua kuwa mmoja wao. Si kwa sababu hujawahi kushawishika, bali kwa sababu uliamua kutomkosea mpenzi wako, hata pale ulipokuwa na nafasi ya kufanya hivyo,” asema Kimani.