Pambo

Ukimnyima mume haki ya ndoa waweza ‘kupandishwa cheo’

June 2nd, 2024 2 min read

NA WINNIE ONYANDO

KATIKA jamii yetu, ndoa ni taasisi takatifu inayojengwa kwa misingi ya upendo, uaminifu na mawasiliano ya wazi.

Sehemu muhimu ya uhusiano huu ni kushiriki mapenzi, ambayo huwaleta wanandoa pamoja kihisia na kimwili.

Hata hivyo, kuna wanandoa wengine ambao huwanyima wenzao kitendo cha ndoa.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na Shirika la Mawakili Wanawake nchini (Fida) mwaka wa 2008, wanandoa hasa wanawake wanawanyanyasa waume wao kingono kwa kuwanyima haki zao za ndoa.

Japo ripoti hiyo ilitolewa miaka kadhaa iliyopita, tabia kama hizi bado zinaendelea katika jamii.

Baadhi ya wanawake siku hizi hutumia mbinu hiyo kuwanyanyasa waume zao hasa baada ya kutofautiana.

Hata hivyo, ni muhimu kuelewa kwamba kama mke, una wajibu wa kumtosheleza mume wako.

Kutomtosheleza kunaweza kusababisha migogoro na hata kusambaratisha ndoa yenu.

Kumbuka kuwa unapoanza kumnyanyasa mume wako kwa kumnyima ngono, unamfungulia mlango kuanza mahusiano ya nje na hata unaweza ‘kupandishwa cheo’ kuwa mke wa kwanza yeye akitafuta wa kumridhisha chumbani.

Kwanza kabisa, ni muhimu kuelewa kwamba ngono ni ishara ya upendo na inawaunganisha kihisia katika ndoa.

Kukataa mara kwa mara kushiriki mapenzi na mume wako kunaweza kumfanya mwanaume ahisi kutengwa na kukosa thamani.

Hii inaweza kumfanya mume kutafuta faraja na kuthaminiwa kwingineko, mara nyingi kwa kuanzisha mahusiano ya nje ya ndoa.

Pili, kukataa kushiriki mapenzi na mume wako kunaweza kuzorotesha mawasiliano na kuongeza mvutano ndani ya ndoa.

Wakati mahitaji ya kimwili na kihisia hayatoshelezwi, hasira na vita zinaweza kutokea.

Hivyo, ni vyema wanandoa kujadili waziwazi hisia na mahitaji yao ili kuepuka matatizo na mvutano usiofaa.

Tatu, kushiriki mapenzi kunasaidia kuimarisha upendo na uaminifu katika ndoa. Mapenzi yakiwekewa kipaumbele na kushughulikiwa kwa heshima, huleta wapendanao karibu kihisia na kimwili.

Wanawake wanapaswa kuelewa kwamba kukataa kushiriki mapenzi na waume zao kunaweza kudhoofisha uhusiano na kusababisha matatizo makubwa.

Hata hivyo, ni muhimu pia kutambua kwamba ngono inapaswa kuwa kitendo cha hiari na heshima kwa pande zote mbili.

Kama kuna sababu yoyote inayomfanya mwanamke ajisikie kutokuwa tayari au kutotaka kushiriki mapenzi, basi ni muhimu ajadili hili na mume wake kwa uwazi. Mawasiliano ya wazi yanaweza kusaidia kutatua changamoto na kupata suluhisho bora kwa wote.

Kwa kumalizia, ningependa kusisitiza kwamba wanawake hawapaswi kukataa kushiriki mapenzi na waume zao bila sababu za msingi na mawasiliano ya wazi.

Kukataa mara kwa mara kunaweza kusababisha waume kuanza kutafuta uhusiano wa nje, hali ambayo inaweza kudhoofisha ndoa na hata kuisambaratisha ndoa yenu.

Ni muhimu kwa wanandoa kushughulikia mahitaji ya wanaume wao kimwili na kihisia kwa heshima na upendo ili kuimarisha ndoa zao.