Ukiwasilisha kesi ya talaka kuwa tayari kuthibtisha mumeo au mkeo alitenda kosa
Talaka nchini Kenya hutegemea kuthibitisha kosa. Hii inamaanisha kwamba sheria inaruhusu kuvunjwa kwa ndoa ikiwa mtu anayeomba talaka ataweza kuthibitisha kuwa mwenzi wake ametenda kosa chini ya sharia ya ndoa.
Katika makala hii tutaangazia mazingira tofauti ambayo talaka inaweza kutolewa nchini Kenya.
Kwanza, sababu kuu zinazotumika kuvunja ndoa za kikristo, kijamii na kitamaduni nchini Kenya ni:Uzinifu unaofanywa na mmoja wa wenzi wa ndoa, ukatili wa kimwili au kiakili unaofanywa na mume au mke dhidi ya mchumba wake au dhidi ya watoto wao, kutelekezwa na mke au mume kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu kabla ya kuwasilisha kesi ya talaka na kuvunjika kwa ndoa kiasi kwamba hakuna matumaini ya kurekebishwa.
Kwa mujibu wa sheria za Kenya, ndoa inachukuliwa kuwa imevunjika kabisa iwapo mmoja wa wanandoa ametenda uzinifu, mume au mke ni mkatili kwa mwenzake au kwa mtoto wa ndoa, amempuuza kwa makusudi mwenzake kwa angalau miaka miwili, wanandoa wametengana kwa muda wa angalau miaka miwili, mmoja wa wenzi amemtelekeza mwenzake kwa muda wa angalau miaka mitatu na mume au mke amehukumiwa kifungo cha maisha au kifungo cha miaka saba au zaidi gerezani.
Ndoa inaweza kuchukuliwa kuvunjika kiasi cha kutorekebishwa iwapo mmoja wa wanandoa anathibitishwa kuwa na matatizo makubwa ya afya ya akili, na hili linapaswa kuthibitishwa na madaktari wawili, mmoja wao akiwa ni daktari wa magonjwa ya akili.
Wenzi waliooana kwa ndoa ya kijamii hawawezi kuomba talaka ikiwa hawajaishi pamoja kwa angalau miaka mitatu.
Mahakama inaweza kuelekeza mgogoro wowote ulioibuka katika ndoa ya aina hii kupelekwa kwa upatanisho. Upatanisho huu ni wa hiari lakini unakubaliwa kisheria.
Hii ina maana kuwa, mara baada ya mahakama kuelekeza mgogoro huo kwa upatanisho, na wanandoa wakikubali, wanatarajiwa kurejea mahakamani ndani ya siku 60 wakiwa na ripoti kutoka kwa mpatanishi.
Baada ya upatanisho, wanandoa wanaweza kuamua kusuluhisha tofauti zao au kuendelea na mchakato wa talaka.
Sababu za ziada za kuomba talaka katika ndoa za kitamaduni zinaweza kujumuisha sababu nyingine yoyote inayotambuliwa na mila na desturi za jamii wanayotoka wanandoa.
Kwa mfano, ikiwa mmoja wa wanandoa amekamatwa kwa kosa kama vile wizi au ujambazi, hii inaweza kuwa sababu ya kuomba talaka, kwa kuwa baadhi ya jamii huamini kwamba tabia kama hiyo inaweza kurithiwa na watoto na kuwafanya kuwa wahalifu au watu wasiofaa katika jamii.
Wanandoa walio katika ndoa ya kitamaduni wanaweza kupitia mchakato wa upatanisho wa jamii yao au utatuzi wa migogoro kwa njia ya kitamaduni kabla ya mahakama kutoa uamuzi wa talaka.
Katika jamii nyingi, wazee hujaribu kuwapatanisha wanandoa kabla ya talaka kuidhinishwa. Iwapo upatanisho kama huu unakosa kufanikiwa, wazee wanaweza kuruhusu ndoa ivunjwe.
Mtu anayesimamia mchakato wa kutatua mgogoro wa kitamaduni huandaa ripoti ya mchakato huo kuwasilishwa mahakamani.