Umuhimu wa kuzingatia habari sahihi katika malezi
KATIKA kasi ya ulimwengu wa sasa unaotegemea vyanzo tofauti vya habari, wazazi mara nyingi hutegemea mtandao kutafuta ushauri kuhusu malezi ya watoto.
Mada kama matumizi ya vifaa bebe na athari zake kwa maisha ya watoto ni maarufu sana katika mijadala mtandaoni.Utafiti mpya uliochapishwa katika jarida la Journal of Children and Media, unaonyesha kuwa wazazi wanapokabiliana na changamoto za kulea watoto katika enzi ya kidijitali, kuelewa jinsi vyombo vya habari vinavyowasilisha habari ni muhimu kama ujumbe wenyewe.
Wazazi hutegemea sana mtandao kwa ushauri – tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 75 hadi 98 ya walezi hutumia mtandao kufanya maamuzi kuhusu malezi. Hata hivyo, uwasilishaji usio sawa wa matokeo ya tafiti unaweza kupotosha mitazamo.
Wataalamu wanasema wazazi wanaotegemea chanzo kimoja au mitandao ya kijamii huweza kupata taarifa zile zile mara kwa mara, hivyo kukosa mitazamo tofauti.
Ili kufanya maamuzi bora, wazazi wanaweza kuchukua hatua madhubuti za kuchanganua taarifa wanazokutana nazo.Kwa mfano, badala ya kusema tu ‘matumizi ya vifaa bebe ni mabaya,’ dadisi ujue iwapo kuna mazingira yanayoweza kuwa na athari tofauti.
“Tumia vyanzo tofauti: Usitegemee tovuti moja au akaunti moja ya mitandao ya kijamii. Tumia vyanzo vingi, hasa vile vinavyotoa maoni ya wataalam,” asema Profesa Erin O’Connor, mtaalam wa malezi dijitali akiandika katika jarida la Psychology Today.
Anashauri wazazi kuhoji kila habari wanayopata kuhusu malezi dijitali kabla ya kuitumia au kuipuuza.“Hoji habari au maelezo ya kushangaza unayopata ukisaka habari kuhusu malezi. Vichwa vya habari vya kushtua vinalenga kuvutia macho, lakini baadhi havina maelezo ya kumfaa mwanao,” asema.
Anapendekeza wazazi watafute utafsiri wa tafiti za wataalam. “Ingawa zinaweza kuwa ngumu kuelewa, tafsiri sahihi zinasaidia wazazi kuimarisha malezi ya watoto wao,” aeleza.
Vyombo vya habari vina ushawishi mkubwa katika kuunda mitazamo ya malezi – na kwa hivyo vina jukumu kubwa. Vyombo vinavyotanguliza kuonekana kuliko usahihi ni hatari na vinaweza kusambaza taarifa potovu au zisizokamilika.Kwa bahati nzuri, baadhi ya vyombo vya habari tayari vinafuata maadili kwa kuchambua kwa kina na kuhimiza uwazi katika taarifa zao.
Kuwa na ujuzi wa kuchambua taarifa kutoka kwa vyombo vya habari kunasaidia wazazi kubaini habari za kuaminika.