Ushauri : Marekebisho ya kisheria yaliyozima udanganyifu katika urithi wa mali
MNAMO Novemba 17 2021, Rais alitia saini Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Urithi ya 2019 na sasa inajulikana kama Sheria ya Marekebisho ya Urithi ya 2021.
Sheria hii mpya ilirekebisha vipengele fulani vya Sheria ya Urithi ya 1981 na kuanzisha mambo mapya.
Lengo kuu la marekebisho lilikuwa kuzuia watu wenye nia ya kujinufaisha kwa udanganyifu kupata sehemu ya mali ya marehemu na hivyo kudhulumu warithi halali wa marehemu.
Vile vile, marekebisho hayo yanabainisha kwa uwazi ni nani anayetambuliwa kama mtegemezi wa marehemu. Pia yanaimarisha ulinzi wa mke au mume, watoto na familia ya karibu katika masuala ya urithi.Kwanza, sheria hii ilirekebisha Kifungu cha 3 cha Sheria ya Urithi ya 1981 kwa kuanzisha tafsiri mpya ya neno “mke au mume”.
Tafsiri hii inaeleza kuwa mke au mume ni mume, mke au wake wanaotambuliwa chini ya Sheria ya Ndoa ya 2014. Sheria hiyo ya ndoa katika Kifungu cha 6 inatambua aina tano za ndoa ambazo tumefafanua katika makala ya awali.
Pili, Kifungu cha 29 cha Sheria ya Urithi ya 1981 kilirekebishwa kwa kufuta cha awali na kukibadilisha na kipengele kipya cha 29, ambacho kinafafanua maana ya mtu anayetegemea marehemu.
Marekebisho hayo yanaeleza kwamba mtu kama huyo ni mke au mume na watoto wa marehemu, awe alikuwa akiwatunza moja kwa moja au la, kabla ya kifo chake.
Pia ni wazazi wa marehemu, wazazi wa kambo, babu na nyanya, wajukuu, watoto wa kambo, watoto walioasiliwa na marehemu, ndugu na dada, iwapo marehemu alikuwa akiwatunza moja kwa moja kabla ya kifo chake.
Marekebisho hayo yanaeleza kuwa mtu yeyote ambaye hajatajwa katika kifungu kipya cha 29 hawezi kutambuliwa kama mtegemezi chini ya sheria hii, isipokuwa mtu huyo athibitishe alikuwa akitunzwa na marehemu kwa kipindi cha angalau miaka miwili kabla kifo chake.
Marekebisho ya Kifungu cha 29 yaliondoa maneno “mke wa zamani” au “wake wa zamani”, kumaanisha kuwa wake waliotalikiwa hawawezi tena kupinga ugavi wa mali ya waume zao wa zamani.
Hili ni badiliko kubwa kwani linahakikisha wake wa zamani hawatakuwa sehemu ya warithi wa mali ya marehemu isipokuwa iwapo walikuwa wakimtegemea marehemu kifedha kwa miaka miwili kabla ya kifo chake.
Zaidi ya hayo, mume wa marehemu sasa anahesabiwa kama mtegemezi wa urithi hata kama marehemu hakuwa akimfaa kifedha kabla ya kifo chake. Hii ni tofauti na msimamo wa awali ambapo mwanamume alihesabiwa kama mtegemezi tu ikiwa mkewe alikuwa akimhudumia kifedha kabla kuaga dunia.