Pambo

Ushauri:Sababu za talaka ni sawa kwa ndoa aina zote nchini Kenya

Na BENSON MATHEKA March 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NDOA ni taasisi takatifu inayounganisha watu wawili wa jinsia tofauti kwa upendo, heshima na uaminifu. Hata hivyo, sio ndoa zote hustawi na hivyo wanandoa wakaamua kutengana rasmi kupitia talaka.

Katika Sheria ya Ndoa ya Kenya 2014 kuna sababu kuu zinazokubalika kuvunja ndoa, ambazo zinatumika kwa aina nne kati ya tano ya ndoa zilizoidhinishwa kisheria; ndoa za Kikristo, Kijamii au Kiraia, Kihindu na Kitamaduni.Uzinifu ni mojawapo ya sababu kuu za talaka katika ndoa nyingi.

Wakati mmoja wa wanandoa anahusiana kimapenzi na mtu mwingine nje ya ndoa, uaminifu huvunjika na mara nyingi husababisha kutoaminiana na maumivu ya moyo ambayo huifanya ndoa isambaratike.

Unyanyasaji wa kimwili, kihisia, au kiakili ni sababu nyingine inayoweza kuibua talaka.
Ikiwa mmoja wa wanandoa anateseka kutokana na dhuluma za mume au mke wake, anaweza kuomba talaka kwa misingi ya usalama wa kimwili na afya ya akili.

Sheria inatambua kuwa ikiwa mmoja wa wanandoa amemwacha mwenzake kwa muda wa miaka mitatu bila sababu za kimsingi au bila makubaliano, ndoa hiyo inaweza kuvunjwa.

Kuachwa kunahusisha mume au mke kuondoka nyumbani na kutoonyesha nia yoyote ya kurudi au kusaidia familia.

Tabia zisizo za kawaida na zinazokiuka maadili zinaweza pia kuleta talaka. Hizi zinajumuisha tabia kama vile uraibu wa dawa za kulevya, ulevi kupindukia, uhalifu au vitendo vinavyohatarisha maisha ya mke au mume.

Ikiwa wanandoa hawawezi tena kuelewana au kuishi pamoja kwa amani, mahakama inaweza kutangaza ndoa hiyo imevunjika kabisa.
Moja ya masharti yanayothibitisha hilo ni kutengana kwa miaka miwili au zaidi bila matumaini ya kurudiana.

Mbali na sababu zilizoainishwa hapo juu, ndoa za Kihindu zinaweza pia kuvunjwa ikiwa mmoja wa wanandoa anaacha imani ya Kihindu na kujiunga na dini nyingine.

Pia ubakaji, ushoga au kushiriki mapenzi na mnyama ni sababu ya kuvunja ndoa.

Vile vile, vitendo vinavyokiuka maadili vinaweza kuwa msingi wa kuomba talaka.Talaka hufuata mchakato wa kisheria ambapo mmoja wa wanandoa anawasilisha ombi la kutaka talaka mahakamani.

Kisha upande wa pili unapata nafasi ya kujibu ombi hilo. Ikiwa hakuna upinzani, mahakama inatoa cheti cha muda cha talaka, ambacho hutangazwa kuwa rasmi baada ya siku 30 na hivyo ndoa kuwa imevunjwa kisheria.

Sababu za talaka zilizoainishwa katika Sheria ya Ndoa 2014 zinafanana katika ndoa za Kikristo, Kiraia, Kihindu na Kitamaduni.
Hata hivyo, ndoa za Kiislamu zinafuata sheria za dini ya Kiislamu.

Katika jamii ya sasa, ambapo changamoto za ndoa zinaongezeka ni muhimu wanandoa kuelewa haki zao kisheria na kutafuta ushauri kabla kufanya uamuzi wa mwisho wa kuvunja ndoa.