Usiache tineja aongozwe na wavumishaji wa mitandao
Wakati wa utineja, wengi hujiuliza maswali makuu kama, “Mimi ni nani?” na “Ninafaa wapi?” Haya si maswali ya kubahatisha, ni sehemu muhimu ya ukuaji wa kisaikolojia. Majibu yake huundwa na familia, tamaduni, walezi na marafiki.
Hata hivyo, katika ulimwengu wa sasa, wavumishaji mitandaoni, na mienendo ya rika kwenye mitandao ya kijamii pia vina ushawishi mkubwa.
Wataalamu wa malezi wanasema wazazi wakishindwa kuunda mazingira salama ya matineja kuchunguza maswali haya, wengine watachukua nafasi hiyo, mara nyingi wakiwa na mitazamo mikali, potofu na hata hatari.
Kwa mujibu wa ripoti ya Observatory on Cyberbullying, Cyberhate and Online Harassment, baadhi ya tabia zinazopigiwa debe na baadhi ya wanaume mashuhuri mitandaoni ni sehemu ya mfumo mpana unaoendeleza ubabe wa kijinsia.
“Intaneti huakisi na kukuza mambo mengi ya maisha ya kila siku mazuri na mabaya, ”asema mtafiti wa vyombo vya habari, Danah Boyd.
Anasema kwamba wavumishaji katika mitandao ya kijamii wanajaza pengo lililopo katika maisha ya matineja wengi hasa wavulana: kiu ya kuthaminiwa, kupewa mwongozo, kupata maana ya maisha, na kujihisi sehemu ya jamii.
“Ili kupambana na athari zao, ni muhimu kuelewa mvuto wao,” asema. Kulingana na wataalamu wa malezi dijitali mitandao ya kijamii ina sifa maalum zinazokutana na udhaifu wa matineja kama upatikanaji wa faragha, mashindano ya umaarufu, na wafuasi wanaopata faida kwa kuvutia umakini wa matineja.
“ Ingawa intaneti haikuzua misimamo mikali, imeifanya iwe rahisi kufikika, kali zaidi, ya kudumu, na ya kibinafsi. Pia imegeuzwa kuwa biashara kubwa inayonufaika na udhaifu wa matineja. Mwisho wa siku, changamoto hizi zinahitaji wazazi, walimu, na jamii kwa ujumla kushirikiana kuwasaidia matineja kupata mitazamo chanya bila kuachia mitandao ifanye kazi hiyo peke yake,”asema Danah.
Kwa hivyo, wazazi wanapaswa kufanya nini hasa?
Uliza vijana ni nini wanaona, kusikia, na kufanya mtandaoni. Sikiliza maneno mapya wanayotumia au mada wanazozungumzia, na udumishe udadisi. Ukiona ishara za misimamo mikali au lugha ya chuki, usipuuzie lakini pia usivamie.
Mvutano unaweza kuongeza mvuto wa “uhuru” unaotumiwa na baadhi ya wavumishaji mtandaoni. Badala yake, eleza misimamo yako kwa utulivu na endelea kushiriki mazungumzo.
Vijana mara nyingi hukutana na maudhui ya aina hii kupitia mitiririko yao ya mitandao ya kijamii bila hata kuyatafuta. Wanahitaji elimu ya vyombo vya habari na uelewa ili kutambua udanganyifu mapema.
Mwisho wa yote asema Danah, mazungumzo haya yanahitaji subira, ushirikiano, na uelewa. Badala ya kuogopa kile vijana wanaona mtandaoni, wazazi na walezi wanapaswa kujenga mazingira salama ya majadiliano, ili kusaidia vijana kujifunza kutambua ukweli, kujiamini, na kufikiri kwa kina katika ulimwengu wa kidijitali unaobadilika kila siku.