Usimfuate fuate mwanao akiingia utu uzima
Katika maisha ya kila siku, wazazi wengi hupitia changamoto ya kuona watoto wao wanapokua na kuwa watu wazima huku uhusiano nao ukibadilika ghafla.
Wale waliokuwa wakitegemea ushauri na msaada wa wazazi kila siku sasa huanza kujiondoa taratibu, na mara nyingine huenda kimya kabisa. Hali hii huwavunja moyo wazazi wengi.
Wazazi wengi wameelezea hisia za uchungu kwa kusema watoto wao huwatenga wakiwa watu wazima. Wanajikuta wakingoja kwa hamu ujumbe wa maandishi au simu ambayo haiji. Wengine hutuma ujumbe mmoja baada ya mwingine kwa watoto, bila majibu.
Lakini swali kuu ni hili: Je, ni jukumu la mzazi kuendelea kumfuata mtoto wake mtu mzima kwa kila hali?
Watoto wanapofikia utu uzima, asema Dkt Jefffrey Bernstein wanajifunza kusimama kwa miguu yao. Wanakumbana na changamoto za maisha—ajira, ndoa, watoto, na mengineyo—na mitindo yao ya kuwasiliana inaweza kubadilika. Wanapoanza kuwa mbali kihisia au hata kimawasiliano, haimaanishi hawawapendi wazazi wao.
Mara nyingi, wazazi huchukulia ukimya wa mtoto kama ishara ya kukataliwa au kutothaminiwa. Hili linaweza kuumiza sana, lakini ukweli ni kwamba watoto hao huenda wanapitia hali zao binafsi, na si lazima iwe ni kosa la mzazi.
Badala ya kuwa na presha ya kuwasiliana kila mara, mzazi anaweza kuonyesha upendo. “Tuma ujumbe mmoja wa pole na wa upole kwa wiki; sema “Nipo hapa wakati wowote utakapohitaji”. Hii hujenga hali ya kuaminiana bila kumchosha mtoto,” asema
Vivyo hivyo, ni muhimu kutambua kwamba upendo hauimaanishi kumsaidia kila mara au kumtatulia kila shida. Kuwa mzazi wa mtu mzima kunamaanisha kumwamini mtoto wako kwamba ana uwezo wa kukabiliana na changamoto zake.
“Kama mzazi, unapomfuata fuata mtoto kila mara kumtumia pesa, kumshinikiza kuzungumza, au kumkumbusha makosa ya zamani huenda ukamfanya ajihisi kutotosha au hata kuchoshwa. Badala yake, jenga mipaka yenye afya.
“Ni muhimu kuelewa kuwa kimya kutoka kwa mtoto mtu mzima mara nyingi ni nafasi anayojipa ili apumue, apange maisha, au ashughulikie mambo yake. Kama mzazi, usikimbilie kuhisi kuwa wewe ni tatizo kwa hali yoyote. Ukijifunza kutulia na kuwa na subira, unajilinda kisaikolojia,” aeleza Dkr Jeffrey katika makala aliyochapisha kwenye jarida la Psychology Today.
Tumia muda huo kujipeleleza. Je, unaumia kwa sababu mtoto amenyamaza, au kwa sababu unahisi hujatimiza wajibu wako? Kwa hali zote, jibu sahihi si kumfuata zaidi, bali kubadilisha namna unavyoshughulikia hali hiyo.
Upendo wa kweli wa mzazi, aeleza ni ule unaoacha nafasi ya mtoto kukua, kufeli, kuanza tena, na kurudi nyumbani kwa hiari yake mwenyewe. Wakati mwingine, kumpa nafasi mtoto ni njia bora ya kumkaribisha nyumbani.