Wanawake Lamu wadai ladha ya ndoa ni ‘kuwakalia chapati’ waume
NA KALUME KAZUNGU
WANAWAKE katika Kaunti ya Lamu wametoa ushauri kwa wanaume wanaotawaliwa na kasumba ya taasubi ya kiume na kuwaambia ladha ya ndoa ni pale mabibi wanakuwa katika mstari wa mbele kwa kutoa ushauri.
Wanasisitiza kuwa hatua hiyo husaidia kupunguza presha na migogoro ya kinyumbani.
Isitoshe, wanasema ni kupitia wanawake kusikilizwa na waume kwa dhati, ama kwa lugha rahisi, wanaume kukubali ‘kukaliwa chapatti,’ ambapo ladha ya ndoa itaongezeka vilivyo.
Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake la Lamu Women Alliance (Lawa) Raya Famau, aliwakosoa wanaume wanaojibeba na kukataa kabisa kusikiliza ushauri kutoka kwa wake wao, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni sawa na kumkandamiza mwenza katika ndoa.
Bi Famau aliweka wazi kuwa ilmradi kuna heshima na mipaka ya mwanamke kwa mumewe, haoni sababu ya kwa nini hao wanaume wasiridhike wanapotawaliwa na wake kwa uzuri.
Alibainisha kuwa wale wanaotilia shaka suala la mwanamke ‘kukalia chapati’ mwanamume wake ni wale ambao wanatawaliwa na taasubi ya kiume tu.
Bi Famau anaamini kuwa punde mwanamume anapokuwa mtu wa kusikiliza wosia wa mkewe, kuukumbatia na kisha kuchanganya na ushauri wake mwenyewe kama kiongozi wa nyumba, mara nyingi hiyo ndoa hufika mbali.
“Kwa nini mwanamume umdhalilishe na kutomsikiliza mkeo? Usipomsikiliza mke wako mnayeishi pamoja na hata kulala pamoja chumbani, basi utamsikiliza nani katika ulimwengu huu? Hawa wenzetu wanaume wakubali ‘tuwakalie chapati’ kwa heshima na taadhima, bora tu sisi wanawake nasi tusifikie kiwango cha kuwapanda vichwa waume wetu,” akasema Bi Famau.
Naye Bi Khadija Alwy alichacha kuwa wanaume walio kwenye ndoa wakikubali kutawaliwa na mabibi wao, ni njia bora ya kuifanya ndoa kuwa na raha hata zaidi.
Bi Alwy aliwakosoa wale wenye fikra kuwa mwamume kukaliwa chapati ni sawa na kukosa usemi mbele ya bibi au hata mchumba wake.
“Sisi wanawake, hasa wa Uswahilini tumefunzwa jinsi ya kumdhibiti mume ndoani kwa kumpa maneno matamu, kujipamba na kuremba chumba kiasi kwamba mwanamume huyo anapoingia chumbani si rahisi kutoka wala kufikiria kwingine. Tukiwadekeza hawa waume wetu, hawatakuwa na budi kutusikiliza hata kiushauri. Hilo kamwe halimaanishi tumewakalia chapati kama wengine waonavyo. Kimtazamo wangu, mwanamume kukaliwa chapati ndio siri kuu ya ndoa tamu,” akasema Bi Alwy.
Mwanaharakati na mtetezi wa masuala ya kijinsia kisiwani Lamu Hindu Salim, alitaja kuwa mara nyingi nyumba huendeshwa na wanawake ambao pia wanapaswa kupewa nafasi ya kuwatawala waume.
Bi Hindu aidha anawashauri wanawake kuwa makini wakati wanapojaribu kutafuta kusikilizwa na wanaume, akisema dini yenyewe ya Kiislamu imeweka wazi nafasi ya mwanamume na mwanamke.
Alisema wanawake wengi wanaopewa nafasi kubwa au sauti na waume wao wameishia kukiuka maadili ya dini na hata kutenda dhambi kwa kutowatambua, kuwaheshimu na kuwasikiliza waume hao.
“Si vibaya kwa mwanamke kuwa na nafasi, iwe ni ya sauti au maamuzi katika nyumba lakini tunapofanya hayo pia tusisahau nafasi aliyopewa mwanamume kwenye ndoa. Mwanamume kivyovyote vile ndiye kiongozi wa nyumba, iwe ni wewe bibi ndiwe husema, kukimu familia au uwe na cheo kikubwa namna gani. Si lazima kila unalosema kama mwanamke lifuatwe. Punde unapoenenda kinyume na nafasi uliyopewa kama mwanamke katika Qur’an au dini, basi wewe utajikosesha pepo. Tuweni makini,” akashauri Bi Hindu.
Kwa upande wake aidha, Imamu wa Msikiti wa Jamia Mjini Mokowe, Ustadh Mohamed Bwanamkuu aliweka wazi kuwa mwanamume kukaa vizuri na mkewe ni jambo bora na muhimu kwani lahitajika hata kulingana na mafundisho ya dini ya Kiislamu na hata nyinginezo.
Bw Bwanamkuu alisisitiza kuwa ni raha kwa mwanamume kutangamana kwa njia nzuri na mkewe kwani hata Mtume Muhammad (S.A.W) asema “bora wenu ni yule bora wenu kwa mke wake.”
Bw Bwanamkuu anaeleza kuwa kauli ya mwanamume ‘kukaliwa chapati’ inajiri wakati mume anapokosa kuwajibikia majukumu ya nyumba, ikiwemo kuikimu familia kwa chakula, mavazi, elimu na kila kitu kipasacho kufanywa.
“Tusisahau kuwa wanaume ndio wasimamizi wa wanawake katika nyumba. Binadamu haiwezekani kuugeuza mpango huo kwamba bibi awe ndiye msimamizi au kichwa cha nyumba. Haya ya kukaliwa chapati hutokea tu wakati wanaume wanapokuwa wazembe au watepetevu. Mwanamume hutoi chochote ambapo bibi ndiye anatekeleza majukumu hayo. Yaani unakuwa mwanamume bwege. Hilo halifai. Lazima tuwe kichwa cha nyumba, ikiwemo kuwajibikia majukumu yatupasayo kama wanaume,” akasema Bw Bwanamkuu.