Makala

Askofu aliyepokea Sh20 milioni za Ruto atakiwa kuziwasilisha kwa EACC au ashtakiwe

Na CHARLES WASONGA March 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA wanne sasa wanamtaka Askofu Mkuu wa Kanisa la Jesus Winners Ministry, lililoko Roysambu, Nairobi kuwasilisha kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Sh20 milioni zilizotolewa na Rais William Ruto kama mchango kwa kanisa hilo, la sivyo wamshtaki mahakamani.

Kupitia barua aliyoandikiwa Askofu huyo na kampuni ya mawakili ya ‘Ndegwa and Ndegwa’, Mabw Kennedy Kariithi Gachenge, Lempaa Soyinka, Fanya Mambo na Peter Kuiria wanadai kuwa pesa hizo zilipatikana kwa njia ya uhalifu kwani asili yake haikufichuliwa.

“Wateja wetu wanaamini kuwa Sh20 milioni ulizokabidhiwa na Bw William Ruto mnamo Machi 2, 2024 ni mali ya wizi au ni mali ambayo haijulikani ilivyopatikana. Ni pesa ambazo zilitolewa na mtu ambaye mnamo Desemba 30, 2024 aliorodheshwa kama mtu wa pili mfisadi zaidi duniani na shirika la Organised Crimes and Corruption Reporting Project –OCCRP, barua hiyo ikaeleza.

Kampuni hiyo, ambayo mkurugenzi wake ni Wakili Ndegwa Njiru, ilisema kulingana na kipengele cha 230 cha Katiba ikisomwa pamoja na sheria ya Tume ya Mishahara (SRC), mshahara wa Rais Ruto ni Sh1,443, 750 kila mwezi na “haiwezekani kwamba angetoa kiasi cha pesa kinachodizi mapato yake yanayojulikana pasina kufichua alikozitoa.”

“Aidha, haiwezekani kwamba Bw William Ruto aliweza kukusanya Sh20 milioni kutokana na mishahara yake kila mwezi kwa misingi ya muda mfupi ambao amehudumu afisini,” barua hiyo ikasema.

Kulingana na Bw Ndegwa, licha ya suala hilo kuvutia hisia za wananchi alitoa pesa hizo, ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Kenya, hajatoa “maelezo ya kuridhisha” kuhusu asili ya pesa hizo.

“Kwa hivyo, tumeshawishi kuwa wewe kama Askofu Mwai unahifadhi pesa chafu,” barua hiyo ikasema.

“Kwa hivyo, endapo utaendelea kukaa na pesa hizo na ukatae kuziwasilisha kwa EACC inavyohitajika kisheria na endapo mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) atachelea kutekeleza wajibu wake kwa kutochukua hatua inayohitajika kushughulikia suala hili, ujue kwamba mawakili wetu wametuagiza tukufungulie mashtaka kama mtu binafsi kwa lengo la kukomboa pesa hizo,” barua hiyo ikasema.

Kampuni hiyo pia ilisema itamshtaki Askofu Mwai “ili kuzuia suala kama hilo kutokea tena.”

Mnamo Jumapili wiki jana, Rais Ruto alitoa mchango wa Sh20 milioni kwa kanisa hilo la Jesus Winner Ministry alipojumuika na waumini kwa ibada.

Kiongozi wa taifa aliahidi kutoa Sh100 milioni katika harambee “ambayo nitahudhuria pamoja na marafiki zangu.”

Hatua hiyo iliibua kero miongoni mwa Wakenya waliohojia hatua ya Rais Ruto kuyapa kipaumbele masuala ambayo hayana manufaa ya moja kwa moja kwa Wakenya.

Kupitia jumbe kadhaa katika mitandao ya kijamii, Wakenya walitaka kujua ikiwa Rais amebatilisha marufuku aliyoweka dhidi ya watumishi wa umma kushiriki harambee baada ya maandamano ya vijana wa Gen Z mwaka jana.

Itakumbukwa kwamba mnamo Novemba mwaka jana Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini walimsuta Rais Ruto kutokana na mwenendo wake wa kutoa mamilioni ya pesa kama michango makanisa “ilhali Wakenya wanaathiriwa na makali ya kuzorota kwa uchumi”.

Mnamo Novemba 18, uongozi wa Kanisa Katoliki, jimbo la Nairobi, lilirejesha Sh5.8 milioni ambazo Rais Ruto na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja walitoa kusaidia kanisa lao lililoko mtaa wa Soweto.