Pasta James Ng’ang’a ajisafisha dhidi ya madai ya unyakuzi ardhi
KIONGOZI wa Kanisa la Neno Evangelism Centre, Pasta James Ng’ang’a amewasuta baadhi ya viongozi serikalini ambao alidai wanamsingizia kunyakua kipande cha ardhi kulikojengwa kanisa hilo.
Alisema Alhamisi kwamba ardhi hiyo, iliyoko katika makutano ya barabara za Haile Selassie na Uhuru Highway, ni mali ya kanisa lake na kwamba aliinunua kutoka kwa Benki Kuu ya Kenya (CBK) kwa Sh42 milioni mnamo 2004.
“Ardhi inamilikiwa kwa njia halali na Kanisa la Neno Evangelism Centre na niliinunua miaka 20 kutoka benki ya CBK kwa Sh42 milioni na nikapewa hatimiliki. Kwa hivyo, wale wanaotumia jina la serikali kudai kuwa nilinyakua ardhi hiyo, wanaipiga vita kanisa wala sio mimi na ningependa kuwahakikishia hapa leo kwamba hawatashinda,” akasema Pasta Ng’ang’a.
Mchungaji huyo alisema hayo baada ya kufika mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Ardhi kujitetea dhidi ya madai kuwa ardhi kulikojenga kanisa ni ardhi za Shirika la Reli Nchini (KRC) zilizonyakuliwa na watu binafsi.
“Nilianza kuhubiri Mombasa kabla ya kuja Nairobi. Huku nikihubiri jijini, niliona bango kutoka CBK lenye maandishi kuwa kipande cha ardhi kinauzwa. Nilipouliza walinitaka ninunue na bei ya Sh32 milioni lakini wakaniambia nilipe asilimia 10 kwanza kisha pesa zilizosalia nikamilishe malipo baada ya siku 90,” akaeleza.
Baadaye, akasema aliambiwa kuwa bei ya ardhi hiyo sasa ilipandishwa hadi Sh42 milioni hali iliyomlazimu kukopa pesa zaidi kutoka Benki ya Equity.
“Tulitia saini makubaliano na benki ya Equity ikanisaidia kulipa pesa hizo kupitia mkopo. Nilimaliza kulipa mkopo huo mnamo 2008 na nikapewa hatimiliki chini ya jina Neno Evangelism Centre,” akafafanua
Alikuwa akiwaambia wabunge wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na Mbunge wa Mugirango Kaskazini Joash Nyamoko.
Ng’ang’a alieleza kuwa stakabadhi alizoonyeshwa za lililokuwa baraza la jiji la Nairobi zilionyesha kuwa ardhi yenye Nambari ya Usajili 209/9640 awali ilikuwa mali ya benki ya Kenya Finance Bank Ltd iliyosambaratika.
“Kulingana na sheria CBK ndio sasa ilichukua mali ya benki hiyo na ndio ikaamua kuuza ardhi hiyo,” mchungaji huyo akasema.
Ng’ang’a alisema kuwa alishangaa alipopokea barua kutoka kwa Shirika la Reli nchini mwaka 2020 ikimjulisha kuwa asasi hiyo ilitaka kutwa ardhi yake.
“Niliwambia kuwa nilinunua ardhi hiyo kutoka CBK na nikapewa hatimiliki.,” akaeleza.
Aliongeza kuwa baadaye aliitiwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi James Macharia na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Huduma za Jiji (NMS) Meja Jenerali Mohammed Badi waliotaka kujua jinsi alivyopata ardhi hiyo.
“Niliwaonyesha stakabadhi zote na wakasema kuwa hawakuwa na baadhi ya stakabadhi hizo katika rekodi zao,” akaongeza Ng’ang’a akiwaeleza wabunge hao kwamba hakupata muda wa kuleta stakabadhi hizo “kwa sababu nilipata ujumbe wa kutakiwa nifike mbele yenu leo asubuhi.”
Baadaye Bw Nyamoko alimpa mchungaji huyo siku 14 kuwasilisha stakabadhi zote kuhusu umiliki wa ardhi hiyo.
Mapema mwezi huu wa Machi, Tume ya Maadili na kupambana na Ufisadi (EACC) iliorodhesha ardhi hiyo (Nambari ya usajili 209/9640) na nyingine nambari 209/12361 ambayo pia inamilikiwa na Ng’ang’a kama miongoni mwa ardhi za shirika la KRC zilizonyakuliwa na watu binafsi.
Vipande vingine ni ardhi nambari 209/12492 na 209/9641 vilivyoko kando ya barabara ya Haile Selassie ambazo zilinuiwa kwa matumizi na shirika la KRC.