Pasta Ng’ang’a akataa kualikwa kwa harambee za kuchangisha karo
NA FRIDAH OKACHI
JAMES Maina Ng’ang’a almaarufu Pasta Ng’ang’a wa kanisa la Neno Evangelism Centre, amewakashifu wazazi wanaompa mwaliko wa harambee kuhusu watoto wao wanaojiunga na Kidato cha Kwanza.
Katika video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Pasta Ng’ang’a alionekana kukerwa hadharani kwa kualikwa kwenye harambee ya kuchangisha pesa kwa ajili ya wanafunzi kuenda shule.
“Kuna mtu ameniita. Kuna watu wako na wazimu? Eti ako na harambee ya mtoto anaenda Form 1. Ukizaa tulikuwa na wewe? Rudisha kule ulitoa,” alisema Pasta Ng’ang’a.
Kwenye mtazamo wake, alihisi wazazi hao kufanya upumbavu wa kukosa kujipanga na kutegemea michango, akitoa onyo na kutaka kufahamu iwapo walikuwa pamoja wakati wa kuzaliwa kwa watoto hao.
“Usiniletee huo upumbavu. Mimi nikuchangie mtoto anaenda kujiunga na Kidato cha Kwanza? Kitambo huyu mtoto alikuwa darasa la kwanza hadi 8, tulikuwa wapi na wewe?”
Kwenye mitandao ya kijamii, wafuasi wa kanisa lake walikashifiwa kwa kusikiza matamshi hayo, wakidai kuwa hayana msingi.
Ashley Nicole alidai kuwa iwapo ni mmoja wa wafuasi wake, hataendelea kutoa sadaka kwenye kanisa la Neno Evangelism.
“Na bado huyo mshirika atazidi kuwa mwanachama, na wengine wengi watazidi kuwa washirika na kuwa kwenye kanisa hilo na kuendelea kutoa sadaka,” alisema Ashley Nicole.
Rahema Feisal alikwazika akichangia jinsi mhubiri huyo alipokea pesa wakati wa Krismasi na kuwa mchoyo wakati wazazi wanahitaji kutiwa moyo.
“…Na yeye aliomba za Krismas akapewa. Saa hii amegeuka kuwa mchoyo,” alichangia Rahema Feisal.