PATA USHAURI WA DKT FLO: Mbona nachemua sana kila asubuhi?
Na DKT FLO
MIMI huchemua sana kila asubuhi na kila ninapokumbana na vumbi na harufu kali. Sikumbuki ni lini hasa nilipoanza kushuhudia haya, lakini nadhani ni tokea utotoni. Nimetumia dawa nyingi lakini tatizo lingalipo. Je, kuna namna naweza kupata suluhu ya kudumu ili kukabiliana na tatizo hili? Tafadhali naomba usaidizi.
Mwangi
Mpendwa Mwangi,
Yaonekana kana kwamba unakumbwa na tatizo linalofahamika kama ‘allergic rhinitis’. Hii inamaanisha kwamba mwitiko wa kingamwili yako kwa viumbi, harufu kali na baridi uko juu. Hivi vinaitwa vichocheo na vinasababisha mshtuko kwa mfumo wako wa kupumua, na hivyo kumfanya mhusika kuchemua na wakati mwingine pua kuziba na kutokwa na kamasi. Kwa kawaida hii huwa kwenye mfumo wa jeni wa mhusika, kumaanisha kwamba tatizo hili laweza kupitishwa kutoka kwa mzazi hadi kwa watoto, na hivyo haliwezi kukabiliwa. Inahusishwa pia na hali zingine za mzio kama vile upele, kikohozi, kuashwa sehemu ya macho (allergic conjunctivitis) na maradhi ya pumu. Mtu anaweza kukumbwa na hali moja kati ya hizi au zote kwa pamoja. Hali hii haiwezi kutibiwa, lakini yaweza kudhibitiwa kwa kujiepusha na vichocheo kama vile baridi, vumbi, harufu kali, chavua na moshi, vile vile kutumia dawa za kukabiliana na mzio (anti-allergy medicines). Vinyunyizi vya pua (Nasal sprays), pia vyaweza kutumika kudhibiti hali hii.
Je, madaktari huafikia vipi uamuzi kuhusu muda wa kutumia dawa? Kwa nini nisiache kutumia dawa pindi ninapoanza kupata nafuu?
Samantha
Mpendwa Samantha,
Hili ni tatizo ambalo limekithiri. Dawa unazopendekezewa na daktari na muda wa kuzitumia huambatana na dalili unazoonyesha, nguvu za ishara hizi, ugonjwa ambao umegundulika, vile vile historia yako kiafya. Muulize daktari wako ikiwa dawa zako ni za kupunguza ishara pekee, kwa mfano dawa za kukabiliana na maumivu, na iwapo unaweza koma kuzitumia pindi ishara fulani zimekabiliwa. Ikiwa umepewa kiua vijasumu (antibiotics), lazima ukamilishe dozi uliyopendekezewa. Hii ni kwa sababu kiua vijasumu hukabiliana na visababishi vya maradhi kama vile bakteria, virusi, kuvu na vimelea. Dozi hutolewa kuambatana na kiwango cha dawa kitakachotolewa na kwa muda upi ili kuangamiza visababishi hivi. Ikiwa dozi ni kidogo au inatumika kwa muda mfupi kinyume na mapendekezo ya daktari, basi visababishi hivi hubadilika na kupata nguvu zaidi za kupigana na aina hiyo ya dawa, kumaanisha kwamba sasa haiwezi kufanya kazi tena mwilini mwa mhusika.
Mpendwa Daktari,
Mwanangu ana umri wa miaka 11, na amekuwa akiumwa na kichwa kila mara hasa shule zinapofunguliwa, vile vile akicheza michezo ya video kwa muda mrefu. Amekaguliwa na madaktari mara kadha na hata kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu ambapo matokeo yameonyesha kwamba hana tatizo. Shida iko wapi?
Mama mwenye wasiwasi
Mpendwa mama mwenye wasiwasi,
Hii yaonekana kana kwamba ni tatizo la kuona. Hebu chunguza ikiwa mwanao anajikaza kuona vitu hasa vilivyo mbali. Pia, muulize mwalimu wake ikiwa ameshuhudia hilo kwa mwana wako. Anapaswa kufanyiwa uchunguzi na daktari wa macho kutambua iwapo anahitaji miwani au matibabu. Unaweza kumuomba mwalimu wake amsongeze kwenye kiti cha mbele darasani karibu na ubao. Aidha, anapaswa kupunguza muda anaotumia kwenye skrini kama vile televisheni, kompyuta, simu. Vilevile anapaswa kunywa maji mengi.