PATA USHAURI WA DKT FLO: Ni lazima upasuaji kuondoa koili/kitanzi?
Na DKT FLO
Mpendwa Daktari,
Kwa wiki kadha sasa nimekuwa nikikumbwa na maumivu ya mgongo na nashuku kwamba ni kitanzi/koili ninayotumia kuzuia mimba. Juma lililopita nilienda katika kituo cha afya ili kiondolewe lakini mhudumu wa afya hangeweza kukiona. Kwa hivyo alinituma kwa mwanajinalokojia ambapo baada ya kupigwa picha ya ‘scan’, koili ilionekana lakini bado walishindwa kuiondoa kwani nyuzi/kamba hazikuonekana. Alipendekeza nifanyiwe upasuaji kuondoa lakini sijashawishika, na hivyo naomba maoni yako.
G.H., Mombasa
Mpendwa G.H.,
Koili huwekwa kwenye uterasi huku nyuzi zake zikining’nia kwenye lango la uzazi. Nyuzi hizi hutumika kuvuta koili hii ikihitajika kuondolewa. Koili ikisonga au ikiwa haipo sehemu inayotakikana, huenda ukakumbwa na maumivu ya tumbo na mgongo au kuvuja damu. Ikiwa mwanajinalokojia atakufanyia uchunguzi na akose kuona nyuzi hizo, anaweza kutumia kijibrashi kidogo kujaribu kuzitafuta na kuziweka vyema. Ikiwa hili halitafaulu, basi picha za ‘ultrasound’ zitapigwa kutafuta ilipo. Kuna hatari kubwa ya kushika mimba ikiwa haiko mahali inapaswa kuwa. Ikiwa baada ya majadiliano yako na mwanajinakolojia bado unataka koili isalie mle, basi waweza kukaa nayo hadi muda wa kuiondoa utimie. Hata hivyo, ni jambo la busara kuiondoa kwa sababu inakuletea matatizo. Hii itafanywa kwa kufungua njia ya uzazi na kuiondoa kupitia upasuaji wa tumbo iwapo imesonga kupitia ukuta wa uterasi na kuingia tumboni.
Mpendwa Daktari,
Nilishiriki ngono na binti mmoja mwezi mmoja uliopita na sasa anasema kwamba ana mimba. Nashuku iwapo mimba hiyo ni yangu kwani tulitumia kinga, na mbali na hayo, niligundua kwamba mimba hiyo ni ya wiki nne na siku nne. Nitafanya vipi uchunguzi wa DNA kabla ya mtoto huyu kuzaliwa?
K, Nairobi
Mpendwa K,
Inawezekana kwa uchunguzi wa DNA kufanywa mama akiwa mjamzito, ambapo chembechembe za DNA za kijusi hutenganishwa na za mama, mimba ikiwa na umri wa kati ya wiki 15 na 20. Ikiwa matokeo sio ya kawaida, basi uchunguzi wa ‘amniotic fluid’ au ‘chorionic villus’ sampling kuthibitisha waweza kufanywa, ambapo sampuli inachukuliwa kutoka kwa tishu zinazozingira kijusi kinachoendelea kukua. Taratibu hizi zinahusisha mwili wa mama kuingiliwa ambapo zaweza chochea mimba kutoka, na hivyo ni vyema kusubiri hadi mtoto atakapozaliwa. Ili uchunguzi huu kufanywa, unahitaji ridhaa ya mama na pia unaweza kuhitaji idhini ya kisheria. Katika baadhi ya uchunguzi utahitaji utaratibu wa kimatibabu.
Kando na hayo unapaswa kuelewa kwamba wahudumu wa afya huhesabu umri wa ujauzito kuanzia siku ya mwisho ya hedhi kushuhudiwa. Kwa mfano, ikiwa mtu alishika mimba majuma manne yaliyopita, lakini alishuhudia hedhi zake wiki mbili kabla ya hili kutokea, basi mimba hii itahesabiwa kuwa ya wiki sita. Hii inamaanisha kwamba hauwezi shuku uwezekano wa kwamba wewe ndiye baba wa mtoto huyu kwa msingi wa tarehe hizi. Zaidi ya yote, uthabiti wa kondomu hutegemea sana na jinsi ilivyotumika.
Mpendwa Daktari,
Mume wangu ana uvimbe kwenye titi lake la kushoto. Awali haukuwa ukisababisha maumivu lakini hivi majuzi amekuwa akishuhudia uchungu. Mbali na hayo, siku kadha zilizopita, titi hili lilianza kutoa majimaji. Anaona aibu ya kuzungumzia suala hili hasa ikizingatiwa sehemu iliyoathirika. Je, yaweza kuwa ni kansa ya matiti?
Anita, Nairobi
Mpendwa Anita,
Uvimbe kwenye titi waweza kuwa wa kusababisha kansa au la. Njia ya kipekee kujua kwa hakika ni kwa kupigwa picha za ‘scan’ na kwa sampuli ya uvimbe huu kuchukuliwa na kufanyiwa uchunguzi wa tishu au seli (biopsy). Ni jambo la busara kwa uchunguzi kufanywa upesi ili matibabu yafaayo yaanze. Wanaume pia wanaweza pata kansa ya matiti.