• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
PATA USHAURI WA DKT FLO: Nina maumivu tupu ya nyuma

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nina maumivu tupu ya nyuma

Na DKT FLO

DKT Flo,

Ninaitwa Duncan kutoka Kaunti ya Nyamira. Tangu mwaka wa 2013 nimekuwa nikikumbwa na maumivu katika tupu yangu ya nyuma. Nimefanyiwa uchunguzi wa ‘haemorrhoids’ lakini nikapatikana niko salama. Nilipewa tembe za ‘Anusol’ za kuingiza mle. Tatizo hili lilitulia kwa muda lakini limekuwa likirejea kila mara. Mwaka uliopita nilipewa krimu hiyo hiyo kupaka na kama kawaida tatizo hilo lilisha. Hata hivyo tangu mwanzo wa mwaka huu shida hiyo imerejea tena. Nifanyaje kupata tiba ya kudumu? Naomba ushauri.

Duncan

Mpendwa Duncan,

Uchungu katika sehemu hii waweza kusababishwa na;

  • Anal Fissure: Kupasuka kwa safu ndani ya tupu ya nyuma kutokana na kupitisha kinyesi kikubwa au kigumu.
  • Hemorrhoids: Kufura kwa mishipa ya damu iliyochomoza katika sehemu ya rektamu na tupu ya nyuma
  • Anal Fistula: Shimo/tundu linalojitokeza katika safu ya ndani ya tupu ya nyuma hadi kwenye ngozi, na ambalo hasa hutokana na maambukizi na mwishowe kusababisha usaha.
  • Mkazo wa misuli
  • Jeraha
  • Kuvimba kwa safu ya ndani ya tupu ya nyuma na rektamu
  • Maambukizi
  • Kuendesha au tumbo kuvimba
  • Kidonda katika safu ya ndani ya rektamu
  • Kansa (ni nadra sana)

Kutokana na sababu kwamba tatizo hili linajirudia, itakuwa vyema kwako kumuona Daktari wa upasuaji (surgeon) ili ufanyiwe uchunguzi wa kina katika mfumo wa gastrointestinal tract unaohusika na mmeng’enyo wa chakula ili kupata virutubisho, na kuondoa uchafu uliosalia kama kinyesi.

Hasa tiba hutegemea na nini hasa kinachosababisha hali hii.

Dawa kama vile ‘Anusol’ huwa na viungo vya kutuliza uchungu na hivyo kukabili ishara. Aidha, zuia tumbo kuvimba (constipation) kwa kunywa maji mengi na kuhusisha viwango vya juu vya nyuzi (fibre) katika lishe yako. Pia, fanya mazoezi, weka ratiba ya saa fulani ya kwenda haja kubwa kila siku na badala ya karatasi ya shashi tumia ‘baby wipes’ kujipangusa. Unapooga, kwa dakika 20 kaa kwenye beseni iliyo na maji yaliyopashwa moto ili kutuliza tishu iliyo na jeraha. Mbali na hayo, kuna vijalizo vya nyuzi ambavyo hufanya kinyesi kuwa chepesi na hivyo kukusaidia kwenda haja kubwa kwa urahisi ambayo unaweza kutumia.

******

Dkt Flo, nimekuwa nikishuhudia maumivu makali katika sehemu ya chini ya tumbo baada ya kufanyiwa utaratibu wa kushawishi uavyaji mimba (Induced abortion) majuma mawili yaliyopita. Tatizo laweza kuwa lipi?

SC

Mpendwa SC,

Maumivu makali ya tumbo yaweza kuwa kutokana na maambukizi, kutoavya mimba vikamilifu, kupasuka au kuharibika kwa viungo vya uzazi. Hii yaweza kusababisha maambukizi ya kuhatarisha maisha na/au kuvuja damu. Unahitaji uchunguzi wa dharura na mwanajinakolojia. Uchunguzi huu utahusisha sehemu nyeti na hata picha ya ‘ultrasound’. Uchunguzi zaidi waweza fanywa ikiwa ni pamoja na ule wa damu, mkojo, vile vile kubaini iwapo kuna masalio kwenye uterasi. Hospitalini utapewa kiua vijasumu, tembe za kutuliza maumivu miongoni mwa matibabu mengine kulingana na nini hasa watakachopata.

******

Nina umri wa miaka 27 na hivi majuzi nilitambua kuwa nina virusi vya HIV. Sina uhakika niliambukizwa lini na hivyo sijui nani hasa aliyeniambukiza. Nina hofu sana kwamba nitakufa hivi karibuni na sitaki watu wajue kuhusu hali yangu, wala kuanza kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi hivi (ARVs) kwa sababu sionyeshi ishara za kuwa mgonjwa.

Fatuma, Nakuru

Mpendwa Fatuma

Japo virusi vya HIV ni maambukizi ya kudumu, sio mwisho wa maisha iwapo yatakabiliwa vyema. Ni vyema uanze kutumia ARVs haraka iwezekanavyo hata ikiwa hauhisi kuwa mgonjwa. Kuna uchunguzi kadha ambao hufanywa kubaini kiwango cha kingamwili, vile vile hali yako kiafya, kabla ya kuanza kutumia dawa. Sababu ya matumizi ya dawa hizi ni kuimarisha mfumo wa kingamwili na kuzuia maambukizi na matatizo mengine ambayo yaweza kutokana na virusi vya HIV. Wakati mwingi huenda hali ya ndani ya mwili wako sio nzuri japo nje waonekana sawa. Kutumia dawa kutakusaidia kuishi maisha ya kawaida na pia kutapunguza uwezekano wako wa kusambaza virusi hivi kwa mtu mwingine. Unahitaji kula vyema na kufanya mazoezi. Kuna vikundi vya kutoa ushauri na kuhimizana wakati huu. Vituo vya kutoa ushauri nasaha hospitalini vitakusaidia kupata matibabu na kupata usaidizi mwingine unaohitaji.

You can share this post!

Watu kadha waugua kipindupindu Mandera

Askari jela wawili wakamatwa kwa kuficha kokeni chooni

adminleo