• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
PATA USHAURI WA DKT FLO: Nini husababisha masikio kuziba?

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nini husababisha masikio kuziba?

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, kila baada ya miezi sita masikio yangu huziba na ninapoenda hospitalini huambiwa kwamba yamejaa uta. Kisha hupewa dawa ya kutia mle na yanarejea hali ya kawaida. Nini kinachosababisha hali hii?

Asante, Ken

Mpendwa Ken,

Masikio huzalisha uta kila siku ambapo bidhaa hii husaidia kulinda sikio kwa kunasa na kuzuia vumbi, vijidudu na bidhaa zingine ambazo huenda zikaingia mle na kuliharibu. Kwa kawaida, sikio hujisafisha kwani uta huu husafiri hadi kwenye lango la sikio na kuanguka au kuondolewa wakati wa kuosha mwili. Kwa watu wengine, kutokana na sababu zisizoeleweka, masikio yao huzalisha uta kupita kiasi. Uta huu waweza kukusanyika na kuwa mgumu na hivyo kuziba mfereji wa sikio. Hii yaweza kusababisha masikio kuziba, mhusika kupoteza uwezo wa kusikia, kelele na maumivu kwenye masikio. Uta huu huondolewa kwa kutumia dawa ambayo huwekwa mle kwa matone na hivyo kuufanya kuwa mwepesi kisha kuondolewa na daktari kwa kutumia taratibu zinazofahamika kama suctioning au curettage. Mkusanyiko wa uta waweza kutokea tena kwa sababu mfereji huu unazidi kuuzalisha.

 

Mpendwa Daktari,

Miguu yangu huvimba kila wakati ninapoenda safari ndefu na hivi majuzi tatizo hilo lilianza kunikumba hata ninapokaa kwa muda mrefu afisini. Kwa kawaida uvimbe huu hupungua au kutokomea kabisa ninapoamka, lakini hurejea baadaye jioni. Shida ni nini?

Lucy, Nairobi

Mpendwa Lucy,

Miguu kuvimba kunatokana na mkusanyiko wa majimaji miguuni kwa sababu ya mzunguko duni wa damu. Damu inapotoka moyoni husukumwa na misuli ya moyo na kutiririka kupitia mishipa midogo ya damu, ambapo mbadilishano wa oksijeni na virutubisho hutokea. Kutoka hapo, damu huanza safari ndefu kurejea moyoni. Ikiwa mtiririko huu ni kutoka kwa miguu kurejea moyoni, kuna matatizo mawili: mtiririko huu unaenda dhidi ya mvutano (gravity) hivyo moyo hausukumi damu inavyostahili. Mwili unategemea mnyweo wa misuli ya miguu kusukuma damu kurejea moyoni. Kwa hivyo ikiwa hausongi ili kuwezesha misuli ya miguu kunywea, huenda kukawa na mkusanyiko wa majimaji miguuni mwako. Ili kukabiliana na tatizo hili, usikae chini kwa zaidi ya dakika 45 bila kusimama na kutembea. Aidha, unaweza kufanyisha miguu yako mazoezi ukiwa katika safari ndefu. Ukiwa unapumzika au kulala, kwa kutumia mto, inua miguu yako uwekelee juu ya mto. Aidha, waweza kutumia stokingi maalum za kufinya misuli ambazo zaweza kusaidia kupunguza au kuzuia miguu kuvimba.

 

Daktari,

Jina langu ni Evelyn na nina miaka 26. Miaka michache iliyopita niliamua kutokula nyama kutokana na sababu zangu za kibinafsi. Hata hivyo, katika siku za hivi majuzi nimekuwa nikikumbwa na maumivu ya kichwa na kisunzi. Nilienda hospitalini kisha nikaambiwa kwamba kiwango changu cha damu kiko chini ambapo nilishauriwa nianze kula nyama ili isaidie kuniongezea damu. Aidha, nilipewa tembe za vijalizo. Je, kuna mbinu ambayo naweza kutumia kuimarisha afya yangu pasipo kula nyama au kutumia dawa?

Evelyn

Mpendwa Evelyn,

Kila kikundi cha chakula kina umuhimu. Madini ya chuma ni kirutubisho muhimu kinachohusika na shughuli za kuzalisha damu. Ikiwa haupati madini haya ya kutosha, basi kiwango chako cha damu (himoglobini) kitapungua. Kutokana na sababu kuwa himoglobini husafirisha oksijeni katika tishu za mwili, kiwango chake kikipungua, basi mwili wako unaanza kukumbwa na matatizo ya upungufu wa oksjeni, na hivyo kusababisha maumivu ya kichwa, kisunzi, kuzimia na hata moyo na figo kusitisha shughuli zao. Ikiwa una upungufu wa madini ya chuma, basi bali na chakula, unapaswa kutumia vijalizo vya madini ya chuma ili mwili wako uweze kuzalisha himoglobini upesi, na hivyo tishu za mwili wako ziache kukumbwa na ukosefu wa oksijeni. Mwili wako hufyonza virutubisho vya chuma upesi kutoka kwa nyama zaidi ya vyakula vingine. Kutokana na sababu kuwa umeamua kutokula nyama, basi itakubidi upate virutubisho hivyo kutoka kwa vyakula vingine vilivyo na virutubisho hivi kama vile maharagwe, dengu, soya, mboga za kijani, matunda yaliyokaushwa kama vile zabibu kavu na nafaka zilizoimarishwa kama vile unga wa ugali.

  • Tags

You can share this post!

MAZINGIRA NA SAYANSI: Vipodozi vyarembesha ila pia hatari...

SHANGAZI AKUJIBU: Nimegundua mke wangu alitoroka kwa mumewe!

adminleo