Peter Kenneth aishauri serikali iachane na ushuru wa thamani ya gari
NA MWANGI MUIRURI
ALIYEKUWA mwaniaji wa Urais Bw Peter Kenneth amesuta pendekezo la serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto la kutaka kuanza kutoza ushuru wa magari kwa kati ya Sh5,000 na Sh100,000.
Hii ni baada ya pendekezo hilo kuzindua ushuru wa asilimia 2.5 ya thamani ya gari.
Bw Kenneth alisema kwamba ushuru huo una maana kwamba bei ya bima kwa magari itaongezeka hadi asilimia 7.5 kwa kila gari kutoka kiwango cha sasa cha asilimia tano(5).
“Acha niwapee ushauri bila malipo kama mtaalamu na mwekezaji katika sekta ya bima. Mwaka wa 2006 serikali kupitia mawaidha ya kitaalamu, ilitupilia mbali ushuru wa magari na badala yake ikalenga wamiliki wote wa magari katika utumizi wa mafuta,” akasema Bw Kenneth.
Akiongea katika kikao cha Baraza la Wazee Kaunti ya Kiambu mnamo Alhamisi Bw Kenneth alisema “hii serikali ingekuwa na washauri waliokomaa, wangeielekeza kudumisha tu ushuru wa mafuta kwa kuwa ndio unaoweza kunasa magari yote yanayohudumu bila kulikosa hata moja”.
“Hata matingatinga ya kubeba miwa ambayo huwa huwa hayalipii bima pamoja na malori yanayohudumu ndani ya matimbo maeneo ya mashinani, lazima yanywe mafuta,” akasema.
Alisema ulazima huo wa kunywa mafuta ndio mtego wa uhakika wa kunasa magari kujumuika ndani ya ulipaji ushuru.
Bw Kenneth aidha alisema kwamba ushuru wa bima uko na mwanya wa kukaidiwa kupitia wamiliki kuhepa bima za ujumla na badala yake kukata Ile ya abiria pekee.
“Kwa mpigo, pendekezo hili la serikali ni butu na litaishia wengi kukwepa na pia kuhujumu uwezo wa uchumi kuunda nafasi za kazi, hivyo basi kuweka serikali kwa shinikizo zaidi,” akasema.
Kuhusu suala la bei ya mafuta kupanda ikiwa ushuru huo utaelekezwa kwa wanunuzi, Bw Kenneth alisema hiyo sio hali.
“Kwa sasa ushuru huo umependekezwa. Ina maana kwamba hiyo ni gharama ya asilimia 2.5 kwa wamiliki wa magari katika awamu mbili za ununuzi magari na ukataji wa bima. Kwa kuwa mafuta ni kwa kipimo cha lita, utapata kwamba nyongeza ya asilimia 0.5 itazua lengo sawa na lile la asilimia 5.0,” akasema.
Alisema kwamba pendekezo la kutoza ushuru wa 0.5 lina umaarufu kuliko la kupendekeza asilimia 5.0.
Bw Kenneth alisema kwamba ni lazima sekta za kiuchumi zitozwe ushuru lakini sio kiholela.
“Hili ni suala la kitaalamu na busara lakini ilivyo kwa sasa, linatekelezwa kiholela,” akasema.