• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
Peter Kenneth ‘aoga’ na kurejea sokoni

Peter Kenneth ‘aoga’ na kurejea sokoni

NA MWANGI MUIRURI 

ALIYEKUWA mwaniaji wa urais 2013 Bw Peter Kenneth amevunja kimya chake, zaidi ya mwaka mmoja na nusu tangu aonekane hadharani akishiriki siasa. 

Bw Kenneth, ambaye 2022 alikuwa anaunga mkono kinara wa Azimio la Umoja kumrithi Rais Uhuru Kenyatta (kwa sasa amestaafu), Aprili 14, 2024 aliitaka serikali ya Rais William Ruto isukume jela wauzaji wa mbolea feki.

Mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuhudumu kama mbunge wa Gatanga pia anaitaka serikali ya Dkt Ruto kuafikia madaktwa ya madaktari wanaoendelea kugoma.

Rais Ruto aliweka bayana kwamba serikali haina pesa kulipa matabibu.

Kwa suala la mbolea, serikali inaonekana kutilia mkazo ripoti za fatalaiza feki.

Akiongea katika Kijiji cha Kirwara, Murang’a alikohudhuria mazishi ya Mzee Kamau wa Chege ambaye alikuwa mfanyabiashara mashuhuri, Bw Kenneth alisema serikali inafaa iwajibikie masuala hayo mawili kwa njia ya dharura.

Kijiji cha Kirwara ni nyumbani kwa kina Kenneth, na alijitokeza katika mazishi hayo kama jirani mwema.

Alisema huu ni wakati wa serikali kuchapa kazi inayoonekana, inayoaminika na inayotoa afueni kwa wananchi pasipo kutoa vijisababu.

Kando na kuhudumu kama mbunge wa Gatanga (2002-2013), Bw Kenneth aidha aliwania ugavana wa Nairobi 2017 na akarambishwa sakafu na Mike Mbuvi Sonko.

Kenneth ambaye pia amehudumia taifa kama Naibu wa Waziri alikuwa akiongea siasa hadharani kwa mara ya kwanza tangu ajitose kwa siasa za kumpigia debe Raila Odinga achaguliwe kuwa Rais wa Tano katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Akiungana na aliyekuwa Rais wakati huo, Uhuru Kenyatta mwanasiasa huyu wa eneobunge la Gatanga alisimama kidete, pamoja na muungano wa mabilionea Murang’a hadi Rais William Ruto akawashinda.

Bw Kenneth alirejelea uratibu wa biashara zake lakini akajitokeza Jumapili akionekana kuwa na msisimko wa kipekee wa kisiasa kinyume na hali zingine ambapo akipoteza kura huwa anakaa kimya na kujitokeza tena uchaguzi mwingine ukiwa umebakisha miezi kadhaa.

Bw Kenneth ni mwanasiasa ambaye katika chaguzi kadha amekuwa akitarajiwa kuchangia pakubwa mkondo wa siasa za kitaifa, mwaka wa 2022 akidokezwa kwamba angeibuka mrithi wa Rais Kenyatta au makamu wa Rais katika serikali ya Bw Odinga.

Hata hivyo, Rais Kenyatta alimpendekeza Bi Martha Karua kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga lakini njama hiyo ikatibuka kwa kishindo hasa Mlima Kenya.

Hata waleo, kunao wanaomuona Bw Kenneth kama mwanasiasa aliye na uwezo wa kuibuka kama mshindani wa hadhi katika uchaguzi mkuu wa 2027 akiwakilisha maslahi ya Mlima Kenya.

Mwandani wake ambaye ni aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi (2017-2022) alisema kwamba “kwa sasa Bw Kenneth anashauriana na wadau na hivi karibuni tutajitokeza kutoa msimamo wa kina kuhusu siasa za hapo mbeleni”.

Alisema kwamba kwa sasa wanaipa serikali muda iwajibikie awamu yake huku wakifuatilia matukio kadha yanayoendelea kutokota akiahidi kuwa “2027 tutakuwa kwa uwanja”.

Katika hotuba yake, Bw Kenneth alisema kwamba ni lazima serikali ya Rais Ruto ijiangazie kama ya kipekee kupitia kuwatupa korokoroni mabwanyenye mafisadi.

“Shida ya nchi hii ni kwamba mabwanyenye wakora huwa hawarushwi jela. Waliouzia wakulima mbolea feki wanafaa kukamatwa, kushtakiwa na kutupwa ndani,” akafoka.

Bw Kenneth alisema kwamba ni uhaini mkuu kwa mtu kuhujumu jasho la mkulima ambaye huchoka akitafutia familia yake riziki na pia kulisha taifa.

Bw Kenneth aidha aliitaka serikali kutafuta pesa na kulipa matabibu ambao wamekuwa katika mgomo.

“Serikali ikarabati bajeti na ipunguze matumizi katika safu zingine ili ipate hazina ya kulipa mishahara inayodaiwa. Watu wasio na hatia wanazidi kuaga dunia kutokana na msimamo mkali wa serikali,” akasema.

Wadadisi sasa wamepata msisimko kwamba huenda Bw Kenneth aoge na arejee sokoni akilenga kuingia Ikulu 2027.

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Makamu Chansela wa Chuo cha Kenyatta aenda likizo ya muda...

Afueni KPLC ikishusha bei ya umeme kwa hadi asilimia 13.7

T L