Peter Munya ajipata njia panda ugenini Jubilee
Na MWANGI MUIRURI
WAZIRI wa Biashara na Viwanda Peter Munya ambaye analaumiwa pakubwa na baadhi ya wanasiasa wa Mlima Kenya kwa kutekeleza sera ‘zinazosaliti wafanyabiashara wa Mlimani’ sasa amejipata kikaangoni na anapigana kufa kupona kujitakasa nembo ya ‘msaliti’.
Akiwa mwanachama wa chama cha PNU na ambacho hakiko ndani ya Jubilee, Munya anachukuliwa kama ‘adui’ wa chama na sera za kisiasa kuhusu urithi wa Ikulu ifikapo mwaka 2022 hivyo basi kulengwa.
Hali yake imegeuka kuwa vibonde ambapo wandani Wa Naibu Rais Dkt William Ruto sasa wamechukulia hatua yake ya kujihusisha na chama cha PNU akikifufua na kukitafutia ufadhili kama ushahidi wa “waziri msaliti kwa sera na kwa siasa.”
Hatua ya Rais Uhuru Kenyatta ya wiki jana kujitokeza nyanjani kushughulikia wafanyabiashara wa Nyamakima jijini Nairobi kufuatia kuzuiliwa kwa shehena zao za bidhaa za uagizaji inatajwa kama ushahidi mwingine dhidi ya ‘usaliti’ wa Munya ambapo akiwa waziri husika ndiye alifaa kuwasaidia wafanyabiashara hao.
Hata hivyo, kulingana na mkuu wa wafanyakazi na pia aliye mwenyekiti wa ufanikisho wa miradi katika Ikulu Nzioka Waita, Rais aliamua kujipeleka mwenyewe nyanjani ili kutangamana na wafanyabiashara waliokuwa na malalamishi ya muda, lakini sio kwa msingi wa kuelewa Munya ni ‘msaliti’.
“Wafanyabiashara hao walikuwa wakiteta kuwa shehena zao 270 ambazo walikuwa wameagiza kutoka ng’ambo zikiwa zimejaa mali ya uchuuzi zilikuwa zimezuiliwa kwa msingi wa kukagua bidhaa ghushi na pia za magendo,” akasema Waita.
Alisema wafanyabiashara 40, 000 wakiwa na mali ya Sh50 bilioni walikuwa wameathirika kwa kipindi cha mwaka mmoja, akisema kuwa rais alikuwa akipokezwa jumbe za malalamishi na wabunge na pia wafanyabiashara.
“Baada ya kilio chao kuzidi licha ya mikutano kadhaa ya wadau, ndio Rais aliamua kujipeleka katika eneo la shida na kwa sasa ametoa mwelekeo ambao umewaacha wote katika sakata hiyo wakiwa na tabasamu,” akasema Bw Waita.
Lakini wa mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua anapinga akisema kuwa Rais alitekeleza ziara hiyo ya kivukio cha nchi kavu cha Embakasi baada ya kupokezwa malalamishi tele na wadau kuwa “Waziri Munya anahujumu umaarufu wa Rais.”
Alisema kuwa Waziri Munya amejiunga na mrengo ndani ya serikali ambao unalenga kusambaratisha umaarufu wa Rais Kenyatta kwa lengo pana la kujiweka pema katika siasa za urithi wa 2022 ambapo hupinga Naibu Rais, Dkt William Ruto.
Alitaka Bw Munya afutwe kazi na wadhifa wake upewe ‘mwingine wa Mlima Kenya’ ambaye ataelewa kuwa “wapigakura wa Mlima Kenya ndio wanahisa wakuu katika hii serikali.”
Mbunge wa Starehe, Charles Njagua alisema, “Tumekuwa tukikita kambi katika afisi ya Bw Munya lakini amekuwa akitupigisha kona na hivyo basi kumwangazia Rais kama aliyefeli kuchunga masilahi ya watu wa Mlima Kenya.
“Kuna wengi ambao wanaangusha Rais na sasa inaonekana tumepata bahati kuwa Rais ameonekana kupevuka macho na sasa kuna ishara atatembeza mjeledi kwa wote wazembe na wasio na manufaa kwa masilahi pana ya siasa za Rais,” akasema Njagua.
Viongozi wa makanisa hawakuachwa nyuma; Mhubiri Paul Mwai wa Jesus Winner Ministries akisema mwelekeo wa Rais unatokana na maombi yao ya kumwombea Rais awaone na awatambue na kisha awatenge maadui wa umaarufu wake hasa Mlima Kenya.
Hata hivyo, akijitetea, Munya aliambia Taifa Leo sio yeye ambaye hufanya maamuzi ya biashara ya uagizaji na mikakati ya kiusalama ya kuzingatiwa.
“Hii ni kazi ya vitengo vingi serikalini na ambapo maamuzi lazima yawe ya kuafikiana katika mikutano,” akasema Munya.
Akaongeza: “Mimi nikiwa waziri siwezi nikasaidia baadhi ya waagizaji kukwepa ulipaji ushuru, kuingiza bidhaa za magendo na pia kujumuisha vifaa vya kiujambazi katika shehena hizo kwa msingi wowote, uwe ni wa kisiasa au vinginevyo.”
Bw Munya alisema wakati Rais alijitokeza Embakasi na kusema shehena hizo ziachiliwe, hakusema hata zile ambazo zimekiuka sheria za ushuru na za usalama wa ndani ziachiliwe.
Akasema kati ya shehena 270 ambazo zimezuiliwa, ni 134 pekee ambazo zimeidhinishwa kuachiliwa.
Munya alitaja madai kuwa anahujumu Rais kuwa “semi ovyo za kisiasa.”
Haki
Alisema kuwa kuhudhuria hafla za PNU ni haki yake ya kimsingi ya kujiamulia mrengo wa kisiasa katika demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa.
Aidha, alisema kuwa katiba humzima tu kujihusisha na siasa za moja kwa moja akiwa waziri lakini sio kuwa rafiki Wa wanasiasa na vyama vyao.
Akijitetea hivyo, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro anamkumbusha kuwa yuko katika baraza la mawaziri katika serikali ya Jubilee wala sio ya PNU.
“Huwezi kuwa katika harusi hii lakini misa za ndoa unafanyia kwa boma la jirani,” akasema Nyoro.
Kimafumbo, anasema kuwa ‘mpango wa kando’ ndani ya siasa ni usaliti ambao unafaa kuzimwa kupitia Munya kutemwa nje ya serikali akimtaja kama “mzigo kwa serikali na Jubilee.”
Munya anajulikana vyema kwa ueledi wake wa kisiasa, hasira za mkizi za ghafla na uwezo wa kujipanga upya kisiasa.
Hivi majuzi Wakenya wamemuona akipigana kufa kupona kuhifadhi wadhifa wake wa ugavana wa Meru baada ya kuchaguliwa 2013 lakini mawimbi ya Jubilee yakivurumishwa na Kiraitu Murungi yakamsomba.
Baada ya ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta kubatilishwa na mahakama ya Juu na kuamrishwa Wakenya warudi kwa debe Oktoba 26, 2017, Munya kwa hasira akatangaza kuwa alikuwa amejiunga na National Super Alliance (Nasa).
Alikuwa awali amekataa katakata kujiunga na Jubilee na ndipo akafufua chama cha Mzee Mwai Kibaki cha Party of National Unity (PNU).
Aliwania nacho na ndipo akagongwa ndipo hadi sakafuni na Murungi na akainuka akiwa analia alichezewa ngware, hivyo basi kujiunga na Nasa ili akimbizane na haki yake ya kutambulika kisiasa.
Taharuki iliyowaingia UhuRuto kufuatia hatua hiyo ya Munya iliwaelekeza hadi Meru ‘kumchumbia’ Munya na ndipo wakamwahidi kuwa wangemkumbatia ndani ya serikali ya kitaifa iwapo wangeishia kuwa washindi.
Leo hii, Munya ni waziri wa masuala ya Afrika Mashariki, wadhifa ambao sio mgeni nao kwa kuwa alihudumu katika afisi hiyo katika utawala wa Mwai Kibaki.
Mzawa wa eneo la Muthaara mwaka wa 1970, Munya anaonekana kubeba ndoto za vijana wa Meru ambapo anapendwa si haba bali kura zikawa hazitoshi kumnusuru kuanguka ugavana.
Ujasiri wake ulimpata akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) nchini na ambapo hakuchelea kusuta serikali ya Uhuru Kenyatta mara kwa mara akitetea ugatuzi.
Amezoea kukumbana na changamoto kwa kuwa aling’atuliwa gavana mwaka wa 2014 lakini akakimbia mahakamani kukata rufaa na akanusurika katika mahakama ya juu zaidi.
Januari 1995 alikuwa katika chuo cha Brussels nchini Ubelgiji ambapo alikuwa amefadhiliwa na ubalozi wa taifa hilo na ambapo alipata hati ya uzamili kwa sheria za kimataifa.
Aliishia katika chuo cha Georgia, Amerika ambapo alipata hati ya pili ya uzamili katika taaluma hiyo.
Mwaka wa 1993 alikuwa katika chuo kikuu cha Nairobi kwa shahada yake ya kwanza kuhusu uanasheria.
Ni mwanafunzi wa uanasheria katika kampuni ya Kamau Kuria na Kiraitu akiwa ni mwanafunzi wa zamani wa shule ya upili ya Chogoria na pia ile ya Meru.
Mwaka wa 2002 aliunda kampuni ya uansheria akishirikiana na mshirika na ikapewa jina Kimayo & Munya Advocates.
Ni katika kipindi cha 2000 na 2002 ambapo alikuwa mhadhiri wa somo la sheria katika Chuo Kikuu cha Moi.
Amekuwa mhadhiri pia katika taasisi za Kenya School of Professional Studies (KSPS) na Kenya School of Monetary Studies (KSMS).
Katika uchaguzi wa 2007, alichaguliwa kuwa mbunge wa Tigania Mashariki na ambapo alimenyana na mawimbi ya kiusalama akishutumiwa na vitengo vya kiusalama kwa madai ya kuwa mchochezi wa makabiliano katika mpaka kati ya Isiolo na Meru.
Alijipa mashiko ya kuepuka lawama kwa kuwa aliteuliwa kuwa naibu waziri wa usalama wa ndani ya Oktoba 2006 na Desemba 2007.
Ni mtoto wa Mzee Jackson Munya M’Rukunga na Mama Grace Mwakithi na ambapo ni mume wa Phoebe Munya na baba wa Karauni na Nkio Munya.