• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Picha za Lamu usiku zamdondosha mate mke wa afisa wa Unesco

Picha za Lamu usiku zamdondosha mate mke wa afisa wa Unesco

NA KALUME KAZUNGU

UFICHUZI wa Afisa Mshauri wa Utamaduni wa Ukanda wa Afrika Mashariki katika Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) Nagaoka Masanori kwamba yeye humsikiliza na kuzingatia maoni ya mkewe, umegeuka kuwa gumzo mitaani, hasa miongoni mwa wanawake.

Wakati wa ziara yake ya hivi majuzi katika mji wa kale wa Lamu kuzindua vitabu vya lugha asili ya Kibajuni, Masanori alifichulia washiriki wa sherehe hiyo kwamba kuna siku alipiga picha kisiwa cha Lamu usiku mmoja na akamtumia mkewe kupitia WhatsApp.

Sababu yake ya kutuma picha hiyo, alisema, ni kuchochewa na urembo wa kisiwa cha Lamu ambacho humeremeta metumetu taa zikiwaka usiku.

Masanori, akiwa ameabiri mashua usiku kuvuka kutoka uwanja wa ndege wa Manda kuingia mjini Lamu, alipendezwa na mandhari yaliyokoleza mng’ao wa taa za rangi aina mbalimbali ambazo ziliwaka na kuupamba mji vyema.

Ni kutokana na hilo ambapo alichomoa simu yake na kupiga picha kisiwa na mji wa kale kwa ujumla na kisha akamtumia mkewe picha hizo kupitia njia ya WhatsApp.

Afisa Mshauri wa Utamaduni wa Unesco – Kanda ya Afrika Mashariki, Nagaoka Masanori. PICHA | KALUME KAZUNGU

Punde mkewe Masanori alipoona jinsi picha hizo zilivyovutia, alimuuliza mumewe ni wapi hasa alipokuwa kwa wakati huo.

Masanori alisema mwanzo mkewe alidhani hapo si Kenya kabisa bali ni nchi fulani yenye maeneo tulivu na mazuri kwa matembezi ya wapendanao na familia.

“Nilipomueleza mke wangu kuwa hicho ni kisiwa cha Lamu nchini Kenya, aliniambia kuwa yeye na watoto wetu, walipendezwa sana na taswira ya Lamu na kwamba nipange mara moja jinsi watakavyoandamana na mimi kuja Lamu kujivinjari,” akasema Bw Masanori.

Aliongeza kwamba mkewe akisema ni hivyo.

“Bosi wangu wa nyumba, ambaye ni mke wangu akishasema, siwezi kupinga hilo,” akafafanua.

Aidha Masanori alifichua mpango wake wa kuzuru tena eneo la Lamu kufikia mwezi ujao, kwa wakati huo akitazamia kuandamana na mkewe na wanawe anaowapenda.

“Kwa sababu bosi amenena basi sina budi. Na ndio sababu mwezi ujao ninarudi tena hapa Lamu na familia yangu, tuje kufurahia haya mandhari ya Lamu pamoja,” akasema Masanori huku umma ukiangua kicheko na kupiga makofi ya kumpongeza.

Masanori aidha aliwashauri wakazi wa Lamu kuenzi mila na tamaduni zao ili kuendelea kulifanya eneo hilo kuwa la kipekee ulimwenguni.

Pia alisisitiza haja ya wenyeji na wageni kuhakikisha mji wa kale wa Lamu, ambao ni miongoni mwa maeneo yanayotambuliwa na Unesco kuwa sehemu zinazolinda na kudhibiti ukale wake, yaani Unesco World Heritage site, kulinda hadhi hiyo.

Mji wa Kale wa Lamu uliorodheshwa na Unesco kuwa eneo linalotambuliwa kwa kuhifadhi tamaduni na itikadi zake mnamo 2001.

Afisa wa Unesco Nagaoka Masanori (kulia) akimkabidhi cheti mmoja wa wakazi Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kutokana na usemi na mapenzi aliyoonyesha Bw Masanori na jinsi alivyoweka wazi jinsi anavyomthamini mkewe, akina mama kisiwani Lamu sasa wanawarai wanaume waliooa na wale walioko kwenye uchumba au mahusiano kuiga afisa huyo wa Unesco kupitia kuzidisha mapenzi kwa wanawake wao.

Bi Khadija Salim alisema ni jambo jema kumuona mwanamume wa hadhi kubwa kama Bw Masanori akimtambua na hata kumzungumzia mkewe hadharani bila kujali.

Alilamika kwamba wanaume wengi, hasa katika ulimwengu wa sasa, wana mazoea ya kuwabeza na hata kuwaficha wake wao, hatua aliyoitaja huvunja moyo wapenzi husika.

“Wanaume wengi hupendelea uhusiano au hata ndoa zao ziwe za siri. Nafurahia kuona wanaume wakijivunia wake zao kama alivyodhihirisha Dkt Masanori. Natumai tabia yake ni mfano bora utakaoigwa na wanaume wengine hapa Lamu na Kenya kwa ujumla,” akasema Bi Salim.

Kauli yake iliungwa mkono na Bi Mwanasaumu Athman aliyeshikilia kuwa ni vyema kwa wanaume kujivunia walichonacho badala ya kukiweka chini ya maji.

Bi Athman alisema kumtambua mwenza wako hadharani ni suala linalokoleza ladha ya ndoa

“Ni mwanamke yupi hapendi kutambuliwa na mumewe hadharani? Wanaume wanakosa kuzingatia hii siri. Wajue wanapotutambua kama vile Dkt Masanori alivyomtambua mkewe, hilo tu linaongeza mapenzi chumbani. Wanaume wachanuke,” akasema Bi Athman.

  • Tags

You can share this post!

‘Kanuni za ushemeji’ anazofaa kuzingatia...

Vita dhidi ya pombe vyageuka ujenzi wa mnara wa Babeli

T L