Pigo kwa Gachagua mwaniaji akimruka pap
Chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kimepata pigo kubwa katika kampeni za ubunge wa Mbeere North baada ya mgombea wake Duncan Mbui kujiondoa ghafla.
Bw Mbui alitangaza kujiondoa kwake kupitia mitandao ya kijamii. ‘Nimekuwa nikifuatilia kwa makini yanayoendelea ndani ya chama cha DCP na nimefikia uamuzi kuwa chama hiki kimegeuka kuwa klabu ya wanachama wachache ndani ya kile kinachoitwa Muungano wa Upinzani,’ aliandika.
Aliongeza:’Klabu hiyo imeingilia na kuamua kuwa DCP haipaswi kuwasilisha mgombea katika eneo la Mbeere North – uamuzi ambao naona kama juhudi za wazi za kuua ndoto yangu na ya familia ya KivuiKivui (kauli mbiu ya kampeni yake inayoashiria nyundo). ‘Kutokana na hayo, nimeamua kuwania kwa tiketi ya mgombeaji huru. Nimekuwa huru daima na nitashinda nikiwa huru.’
Mchanganuzi wa siasa Bw Wahome Thuku alitaja hatua ya Mbui kama uthibitisho wa mshikamano ndani ya upinzani unaolenga kusimamisha mgombea mmoja kukabiliana na yule wa Rais William Ruto.
‘Hatua hii imewatia hofu serikali na washirika wake,’ alisema.
Akizungumza katika eneo bunge la Mathioya, Kaunti ya Murang’a, Alhamisi, Bw Gachagua ambaye amekuwa kimya kuhusu Mbui, alisisitiza kuwa DCP itasimamisha wagombeaji katika chaguzi ndogo zote 27 zitakazofanyika Novemba 27.
Awali, DCP ilikuwa imemtangaza Mbui, ambaye kwa sasa ni MCA wa wadi ya Evurore katika Bunge la Kaunti ya Embu, kuwa mgombea wake. Timu yenye ushawishi mkubwa ikiongozwa na Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji, Seneta wa Nyandarua John Methu, Seneta wa Kiambu Karungo Thang’wa na Mbunge wa Kajiado North Onesmus Ngogoyo ilitumwa kumtambulisha rasmi.
Hata hivyo, baada ya wiki kadhaa za mvutano kati ya kiongozi wa Democratic Party (DP) Justin Muturi na Bw Gachagua kuhusu kiti hicho, inaonekana kuwa Naibu Rais huyo wa zamani amekubali kuachia chama cha Muturi kusimamisha mgombeaji wa upinzani.
Kiti hicho kilisalia wazi baada ya Rais Ruto kumteua aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo, Bw Geoffrey Ruku, kuwa Waziri wa Huduma za Umma. Ruku alichaguliwa kwa tiketi ya DP, na baadaye kuchukua nafasi ya kiongozi wa chama chake (Muturi) alipofutwa kazi kutoka wadhifa huo na Rais.
Katika uchaguzi wa 2022, ushindani ulikuwa mkali ambapo Ruku alipata kura 17,069 dhidi ya Muriuki Njagagua (UDA) aliyepata 16,422. Patricio Njiru wa Jubilee alipata 2,390 huku Njuki Ngari wa DEP akipata 1,873.
Bw Muturi aliapa kuwa DP ilikuwa na nia ya kurudisha kiti hicho kupitia uchaguzi mdogo na alikataa katakata kutoa nafasi kwa DCP kubeba bendera ya upinzani. Kwa upande wake, Bw Gachagua alisisitiza kuwa DCP ilikuwa chama cha kitaifa chenye mizizi ya Mlima Kenya na alikuwa tayari kujaribu nguvu zake kwenye ulingo wa siasa.
Mbui alichaguliwa kuwania kiti hicho kupitia DCP, lakini Muturi alimteua MCA maarufu wa Muminji na mwanamuziki maarufu Newton Kariuki, anayefahamika kwa jina la kisanii Karish Mwana M-Embu.
Bw Muturi alisema:’Nchi hii ni ya mfumo wa vyama vingi na hatuwezi kukubali kurudishwa kwenye mfumo wa chama kimoja tuliopinga miaka 33 iliyopita.’
Aliongeza kuwa DP pia inapanga kushiriki katika chaguzi zote ndogo – hatua iliyoweka mazingira ya makabiliano kati ya vyama hivyo viwili.
Wachambuzi wa kisiasa wanasema hatua ya kujiondoa kwa Mbui ni pigo kwa Gachagua ambaye alihitaji ushindi huu kudumisha hadhi yake kama mwelekezi wa siasa za Mlima Kenya kuelekea 2027. Mbali na DP, vyama vingine ndani ya muungano wa upinzani ni pamoja na People’s Liberation Party ya Martha Karua na Party of National Unity ya Peter Munya.
Vingine vinavyowania ushawishi wa Mlima Kenya ni Jubilee inayoongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, Usawa kwa Wote ya Mwangi wa Iria, Tujibebe Wakenya ya Waziri wa ICT William Kabogo, The Service Party ya Mwangi Kiunjuri, The National Democrats ya Thuo Mathenge na Umoja na Maendeleo Party ya Kawira Mwangaza, pamoja na UDA ya Rais Ruto.
Kwa mujibu wa mchambuzi wa siasa za Kaunti ya Embu Bw Malila Munywoki iwapo Mbui na Kariuki wote wangeng’ang’ania kusalia kwenye kinyang’anyiro, mgombea wa UDA angepata faida ya wazi. Lakini kama upinzani utaungana, basi kutakuwa na pambano halisi.’