Polisi anayetumia ucheshi kulainisha raia
NA WANDERI KAMAU
NI nadra sana kupata polisi ambaye hutumia ucheshi anapotangamana na raia.
Kwa kawaida, polisi wengi wanajulikana kwa kuwa wakali sana wanapoingiliana na raia.
Sifa hiyo ndiyo imewafanya wengi kuogopewa na raia—wakati mwingine hata wakionekana kuwa maadui.
Hata hivyo, polisi mmoja amejitolea kubadilisha dhana hiyo, kwa kutumia ucheshi kila mara anapoingiliana na raia.
Polisi huyo ni Inspekta Evans Ikomol, anayehudumu katika Kaunti ya Bomet.
Kwenye mahojiano ya kipekee na ‘Taifa Leo Dijitali’, Bw Ikomol alisema kuwa aligundua siri ya kudumisha uhusiano mzuri na raia alipojiunga na Idara ya Polisi karibu miaka 20 iliyopita.
“Katika maeneo yote ambayo nimehudumu, huwa ninajaribu kuhakikisha kuwa nimebadilisha dhana ambayo raia huwa nayo dhidi ya polisi. Kwa kufanya hivyo, wengi hugeuka kuwa marafiki wakubwa wa polisi, kwa kutupa habari muhimu ambazo hutusaidia sana,” akasema Bw Ikomol.
Tangu ajiunge na idara hiyo, baadhi ya maeneo ambayo amehudumu ni Pokot Magharibi, Turkana, Trans Mara, Molo na sasa, Bomet.
Alisema kuwa mbinu hiyo imemsaidia sana—pamoja na polisi wenzake—kukabili uhalifu na wizi wa mifugo, hasa katika maeneo kama Turkana na Pokot Magharibi.
“Katika maeneo hayo, wananchi wengi huwa wanawajua wahalifu, kwa mfano wale ambao huwa wanashiriki katika wizi wa mifugo. Hata hivyo, uhusiano mbaya ambao umekuwepo baina yao na vikosi vya usalama kwa muda mrefu, ndio umekuwa kizingiti kikuu kwenye juhudi za kukabiliana na maovu hayo,” akasema Bw Ikomol.
Je, ni mbinu zipi ambazo huwa zinamsaidia kutangamana na wananchi?
Bw Ikomol anasema kuwa kando na mafunzo kuhusu masuala ya usalama aliyopata, amesomea taaluma ya uanahabari.
“Kando na kuwa polisi, nilisomea taaluma ya uanahabari hadi katika kiwango cha chuo kikuu. Nilisomea katika Chuo Kikuu cha Egerton. Kwa kutumia masuala niliyofunzwa kuhusu mawasiliano, hilo limenisaidia sana kuingiliana na raia, kwa kuwadhihirishia kuwa polisi hawapaswi kuwa maadui, bali marafiki wao ili kuifanya iwe vigumu kwao kukabili visa vyovyote vya uhalifu,” akasema Bw Ikomol.
Anasema analenga kutumia mbinu hiyo katika maeneo yote ambayo atahudumu ili kuhakikisha Wakenya wamebadili dhana zao dhidi ya polisi.
Anasema kuwa ushirikiano huo ndiyo njia ya pekee inayoweza kuhakikisha hali ya usalama imeimarishwa katika jamii.