Makala

Polisi Mumias wachunguza visa vya watu kuporwa kila wanapotoka benki

Na SHABAN MAKOKHA April 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

POLISI mjini Mumias Kaunti ya Kakamega wanachunguza visa ambapo watu wanaotoa hela kwenye benki wamekuwa wakivamiwa kisha kuibiwa na magenge ya wahalifu wanaodaiwa wamejipanga vyema.

Tukio la hivi punde ni ambapo Roselida Akinyi kutoka kijiji cha Budonga, Navakhola aliibiwa Sh200,000 kisha kupigwa risasi hadi kufa.

Alikuwa ametoa hela kwenye benki moja mjini Mumias mnamo Alhamisi.

Bi Akinyi alikuwa mwalimu katika Shule ya Sekondari ya Nanderema na alipigwa risasi baada ya kuondoka kwenye barabara ya Kakamega-Mumias eneo la Eluche akielekea kwake.

Kumekuwa na ada ambapo watu wanaotoa zaidi ya Sh100,000 wamekuwa wakilengwa na wezi ambao huwafuata kwa kutumia magari aina ya Probox au hata pikipiki.

Wakazi sasa wanadai kuwa baadhi ya wafanyakazi wa benki ya KCB na Cooperative ambazo ndizo kubwa zaidi Mumias, wanashirikiana na wakora hao kuwaeleza kuhusu wateja ambao wanatoa kitita kikubwa cha pesa.

Baadhi ya wahalifu hao wamekuwa wakiwafuatilia wanaotoa pesa huku wengine wakiwalenga na kuvunja magari yao yakiwa yameegeshwa kwenye vituo vya petroli, supamaketi au hoteli kisha kuhepa na hela zao.

Kabla ya kesi ya wikendi, mwalimu ambaye alikuwa amestaafu na anatoka kijiji cha South Wanga alipoteza Sh500,000 kwa wezi ambao walikuwa wamemwandama kutoka Mumias.

Walikuwa kwenye gari aina ya Probox yenye vioo ambavyo mtu hawezi kuona ndani. Waligonga pikipiki yake, wakamwibia na wakaendesha gari kwa kasi ya juu huku wakimwelekezea bunduki.

Ruth Makamu kutoka kaunti ndogo ya Mayoni naye alipoteza Sh700,000 baada ya kuibiwa na watu waliokuwa na bunduki na walikuwa kwenye pikipiki.

Bi Makamu alipatwa na shinikizo la damu kutokana na kisa hicho akafa siku chache baadaye.

Mwalimu kutoka Nyakwaka naye alipoteza Sh250,000 baada ya watu wanaoshukiwa kuwa wahalifu kuvunja gari lake. Alikuwa ametoa pesa hizo kutoka benki mjini Mumias.

Awali, Ali Wawire, mumewe marehemu Roselida Akinya alitekwa nyara na baadaye akaachiliwa baada ya kutoa Sh600,000 benkini.

Wanandoa hao walikuwa wakiendesha biashara za Mpesa Mumias Mashariki na Navakholo.

Kamanda wa Polisi Mumias Mashariki Dorice Chemoss alisema matukio hayo yanaaibisha na huenda wanashirikiana na wafanyakazi wa benki au kufuatilia wanatoa pesa nyingi benkini kisha kuwavamia.

“Huwa wanaingia kwenye kumbi za benki na kufuatilia wale ambao wanatoa hela nyingi. Wakishamtambua aliyetoa hela nyingi, wanashirikiana na wenzao kuwaandama na kuwapora,” akasema Bi Chemoss.

Aliwaomba wale ambao wanatoa pesa nyingi watafute huduma za polisi ili kuhakikisha usalama wao.

Makachero kutoka Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) wameanza msako kuandama genge hilo kuzima visa hivyo wizi na mauaji.

“Angalau kwa sasa tumepiga hatua katika kuwaandama japo hakuna aliyekamatwa,” akasema.

Mnamo Jumamosi makachero waliwahoji wafanyakazi wa benki na kuangalia kanda za kamera za CCTV kwenye benki ya Cooperative mjini Mumias.