Makala

Polisi wa Kisii wawapa mahabusu sherehe ya chang’aa ndani ya seli

January 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI

MAAFISA wawili wa polisi katika kaunti ya Kisii wako katika hatari ya kufutwa kazi baada ya kuandalia mahabusu sherehe ya chang’aa ndani ya seli.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Kaunti ya Kisii Bw Patrick Mukuria, kisa hicho cha kushangaza kilitokea mnamo Januari 25, 2024 katika kituo cha polisi cha Rioma.

“Uchunguzi umebaini kwamba maafisa wawili wanaohudumu katika kituo hicho cha polisi wakifahamika kama Konstebo Erick Mogoi na Konstebo Francis Ngugi walikuwa kazini rasmi na ndipo wakawazia kuwapa mahabusu sherehe ya mvinyo haramu,” akasema.

Bw Mukuria alisema kwamba katika seli hizo kulikuwa na washukiwa wawili wa mauaji ambao mahakama ilikuwa imeamrisha wazuiliwe hapo uchunguzi ukiendelea.

“Majina ya wafungwa hao ni Mathew Omanga na David Mboga. Maafisa hao waliwapelekea mgao wa chang’aa ambayo haijulikani maafisa hao walikuwa waliiagiza kutoka wapi na sherehe ikatanda,” akasema.

Haijulikani kama ni mahabusu hao waliomba kuburudika ama ni maafisa hao waliingiwa na roho ya ukarimu na wakaonelea kuwafaa mahabusu hao na ufadhili wa mvinyo.

Bw Mukuria alisema kwamba nyimbo za shangwe na furaha kutoka kwa maafisa hao pamoja na mahabusu wao ndizo ziliwavutia wakubwa wa stesheni hiyo na wakafika kujua nini kilikuwa kikiendelea.

“Ndipo maafisa hao wawili walipatikana wakiwa walevi chakari huku wakiimba nyimbo za ukombozi, nao mahabusu wakiwa katika hali iyo hiyo nao wakitandaza ngoma za kujituliza masaibu wakiwa hoi katika seli zao,” akasema.

Msako wa kujua kileo kilichokuwa kimewachangamsha hivyo ulitekelezwa na kibuyu kilichokuwa kimetumika kuingiza chang’aa hiyo kilipatikana ndani ya seli kikiwa kitupu.

“Ndipo uamuzi uliafikiwa wa kuwasafirisha washukiwa hao pamoja na maafisa hao wa polisi hadi katika kituo cha polisi cha Kisii na baada ya kufanyiwa uchunguzi wa alcoblow, wakapatikana walikuwa walevi kupindukia. Kibuyu pamoja na matokeo ya alcoblow yalihifadhiwa kama ushahidi huku hatua za kinidhamu zikianza kuwaziwa na wakubwa,” akasema.

[email protected]