Makala

Polisi wa kiume waonywa dhidi ya kufugwa na wahudumu wa biashara ya mahaba

April 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI 

KAMANDA wa Polisi eneo la Mwea, Chrispinus Omongini ameonya maafisa wake wa kiume dhidi ya kufugwa na wahudumu wa biashara ya mahaba.

Hii ni baada ya visa vya aibu kuchipuka katika Mji wa Makutano, Kaunti ya Embu ambapo umesheheni biashara ya ukahaba, vikihusisha maafisa wa polisi.

Katika kisa cha wikendi iliyopita, afisa wa polisi alishambuliwa na makahaba baada ya kuzua fujo katika chumba cha kahaba rafikiye.

“Afisa huyo alifika katika mtaa wa Kivuva na akaingia kwa chumba cha mwanamke kahaba na baada ya muda, kukazuka fujo,” ripoti ambayo Taifa Dijitali imeona inasema.

Afisa huyo alikuwa akiteta kwamba licha ya kujimudu kumpa mwanamke huyo pesa za matumizi kila siku, bado alikuwa akiuza mahaba badala ya kumhifadhia yawe yake binafsi.

“Afisa huyo alitumia pingu kama kufuli ya kufunga mlango kutoka ndani huku akimshambulia mwanamke huyo kwa makonde yaliyoishia nduru kutanda katika danguro hilo,” ripoti hiyo ya ujasusi inaelezea.

Afisa huyo alishinikizwa kufungua pingu zake baada ya makahaba kutisha kuvunja mlango.

Katika hali ya kuogopa pingu zisiharibike na aishie kuwa motoni kazini, alifungua mlango na ndipo akakabidhiwa kichapo cha mbwa na wanawake waliokuwa na ghadhabu.

“Kisha, makahaba hao walikimbia hadi katika Kituo cha Polisi cha Makutano, wakaripoti kisa hicho na ambapo Kamanda wa Stesheni (OCS) ndiye alichukua wajibu wa kupatanisha afisa wake na wanawake hao wahudumu wa biashara ya mahaba,” ripoti hiyo inaendelea kusema.

Ni katika msingi huo ambapo Bw Omongini ametoa onyo kwa maafisa wake wajiepushe na hali za uchumba na mitandao hiyo ya makahaba.

Amewataka maafisa hao, ikiwa watapendana na wanawake wa mtaa almaarufu vibiriti ngoma “basi muwachukue na muwaweke kwa ploti za upangaji ambapo mtawadhibiti kama wake wenu”.

Ameteta kwamba hata sio sifa za mwanamume anayejielewa “kuchukuliwa na mwanamke na kufugiwa kama mifugo ndani ya chumba ambacho mwanamke yuyo huyo hujiuzia kama kahaba”.

Alisema hata kuna maafisa ambao wametekwa hisia zao katika madanguro ya pombe za mauti na mihadarati, hata nao akiapa kuwaadhibu.

 

[email protected]