Makala

Polisi waanza kumsaka mbwa wao aliyetoweka Meru

February 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

POLISI katika Kaunti ya Meru wameanza msako mkali dhidi ya mbwa wao aliyetoweka katika hali tatanishi mnamo Jumanne, kutoka Kituo cha Polisi cha Tigania.

Kulingana na ripoti ya polisi, mbwa huyo aina ya Belgian Malinois alipatikana akiwa hayupo kwenye chumba chake na mhudumu ambaye huwa anamlisha.

Mbwa huyo, anayeitwa ‘Jet’, ana umri wa miaka saba na ana rangi ya kijivu, ilisema ripoti hiyo.

“Mhudumu huyo aliripoti tukio hilo kwa Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Msimamizi Mkuu wa Mbwa wa Ukanda huo,” ikasema ripoti hiyo.

Polisi wamekuwa wakimtafuta mbwa huyo katika sehemu tofauti eneo hilo, tangu alipotoweka.

Idara za usalama katika eneo hilo zimetoa wito kwa wakazi kutoa habari yoyote inayoweza kuwasaidia polisi kumpata mbwa huyo.

“Mbwa huyo ni rafiki wetu wa karibu. Tunamwomba mtu yeyote mwenye habari kuhusu aliko aripoti kwenye kituo cha polisi kilicho karibu,”  akasema polisi mmoja wa kitengo cha kuhudumia mbwa.

Kulingana na Shirika la Kuwahudumia Mbwa nchini Amerika (AKC), Belgian Maliois ni miongoni mwa aina za mbwa wanaopendelewa sana na polisi kote duniani kutokana na ukakamavu wao.

“Ni mbwa wenye uwezo mkubwa sana katika kuwanasa washukiwa,” linaeleza shirika hilo.

Shirika hilo lilianzishwa mnamo 1884, na linaaminiwa sana kwenye ulezi, utoaji matibabu na ufunzaji wa mbwa.

Mbwa aina ya Belgian Malinois pia wanapendelewa sana na jeshi, likiwemo jeshi la Amerika.

Shirika pia linawataja mbwa aina hiyo kuwa “wenye nguvu, wanaojiamini, wenye urefu wa kati ya inchi 22 na 26.”

“Ni mbwa mwaminifu, mwerevu na mwenye urafiki mkubwa na binadamu,” linaeleza shirika kwenye tovuti yake.