• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Polisi wafichua sababu nyeti za kuua washukiwa

Polisi wafichua sababu nyeti za kuua washukiwa

NA MWANGI MUIRURI

VIKOSI vya polisi nchini mara kwa mara hushutumiwa kwa kuwekeza bidii za utekelezaji sheria katika njia ya mkato ya kuua washukiwa kikatili pasipo kuwawasilisha mahakamani.

Huku makundi ya haki za kibinadamu yakizidisha harakati za kulaani mauaji hayo, polisi wanashikilia kwamba mshukiwa akionyesha ukaidi zaidi, atakumbana na risasi na kuuawa.

Hali hii ndio ilishinikiza watunzi wa Katiba Mpya ya Mwaka 2010 wawazie kuweka Mamlaka Huru ya Kumulika Utendakazi wa Polisi (Ipoa) ili kuwawajibisha mkondo wa kisheria polisi wauaji.

“Hatupendi kuua watu. Maafisa wa polisi pia ni binadamu na wangependa kuokoa jamii kutokana na misiba isiyofaa. Lakini kila hali itafsiriwe kwa mazingara yake. Hakuna Mkenya aliye na ufahamu wa masuala ya nchi ambaye hajui kwamba hata sisi maafisa wa polisi huuawa na majambazi,” asema Inspekta Mkuu wa Polisi Japhet Koome.

Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome. PICHA | DENNIS ONSONGO

Bw Koome anasema kwamba polisi hujipata katika hali ya kujinusuru kwanza na ndipo hufyatulia washukiwa risasi.

“Katika hali kama hizi, mara nyingine mauti hutokea. Hali huwa ni nani atatwaa bunduki yake kwanza na awe na shabaha ya juu kati ya jambazi na polisi,” afafanua.

Bw Koome anaonya kwamba risasi zitazidi kutembea katika hali ya kuweka usalama “watu wapende wasipende kwa kuwa kuna baadhi ya washukiwa hata uwape mazingira mazuri ya wao kusalimu amri, watazidi tu kuomba mauti”.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki hivi majuzi alisema kwamba polisi hujipata kwa ulazima wa kuthibitisha kama kweli bunduki na risasi za Kenya hufanya kazi.

Waziri Kindiki alisema kwamba “bunduki si mwiko wa kusonga ugali na risasi si mahindi”.

“Bunduki na risasi huwa na kazi maalum katika vitengo mbalimbali vya idara ya usalama na huwa imekadiriwa kwamba silaha hizo zinaweza zikatumika dhidi ya binadamu anayefaa,” akasema Prof Kindiki.

Prof Kindiki anashikilia kwamba “sheria ya kuua washukiwa imeelezewa vizuri sana na sisi kama serikali kazi yetu ni kuhakikisha utawala bora”.

“Wale wanaostahili risasi watazidi kuzipokea kwa msingi wa kisheria lakini maafisa wetu ambao watatekeleza mikakati nje ya sheria hiyo watasakamwa na wafungwe,” akaweka wazi.

Kamanda wa polisi wa Ruiru Alexander Shikondi anashikilia kwamba kuonyesha moyo wa huruma kwa jambazi sugu ni sawa na kuchinja halaiki ya watu wasio na makosa.

“Hakuna jinsi ambavyo polisi aliyejihami atakumbana nawe ukiua watu kiholela na kuwapora ukitumia mabavu…wengine ukiwabaka na ufikirie haki za kibinadamu zitakusaidia. Utapigwa risasi na Mungu abakie akiwa Mungu tu,” akasema Bw Shikondi.

Bw Shikondi anaweka wazi kwamba haki za mshukiwa huishia pale haki za watiifu wa sheria zinaanzia.

“Hata katika changamoto hizi za baadhi ya maafisa wetu kushtakiwa pasipo haki yoyote, sioni vile wakubwa wetu watatuachilia sisi sote kama maafisa wadogo na wananchi kuteswa na majambazi ambao dawa yao tu ni kulazwa pema pale kwa barafu,” akasema.

Wakili wa Mahakama Kuu Timothy Mwangi anasema kwamba jamii huwa imegawanyika mara mbili kuhusu suala la polisi kuua washukiwa.

Anasema kwamba wale wote ambao ni watiifu huhofia tu maafisa kupewa uhuru kupita kiasi wa kuua kwa kuwa wanaweza wakawa wendawazimu wa kuua hata wasio na makosa.

“Lakini wale ambao wana misukumo ya uhalifu pamoja na jamii na marafiki zao, hupinga utumizi wa risasi dhidi ya washukiwa. Lakini bora tu sheria ifuatwe, washukiwa watazidi kuuawa na polisi. Letu tu ni kupiga msasa kila tukio na kuliweka wazi katika msingi wa kisheria,” akasema Bw Mwangi.

Aliyekuwa jambazi sugu wa wizi wa kujihami kabla ya kubadilika na akageukia uandishi wa vitabu, John Kiriamiti, anasema kwamba jambazi anayejielewa anajua kwamba akifumaniwa na polisi, hafai kufyatua bunduki yake.

“Usipozua fujo hakutakuwa na hali ya kushinikiza polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi yako. Ukifumaniwa peupe kubali, salimu amri, weka chini bunduki yako na uweke mikono yako juu ambapo viganja vyote vya mikono vinafaa kuonekana wazi na ikiwezekana, lala chini ukiwa umenyoosha mikono kama ishara ya amani tosha,”ashauri Bw Kiriamiti.

Bw Kiriamiti anasema kwamba kuanza vita vya risasi na polisi ni upumbavu wa kiwango cha kipekee kwa kuwa hao maafisa hawaogopi kukufyatulia na hawataishiwa na risasi pamoja na bunduki.

“Polisi wana uwezo na subira kukesha kwako kwa muda wowote ule wakiita vikosi vingine kukukabili wewe tu,” aonya.

Mwenzake Kiriamiti aliyebadili mienendo pia Bw Elias Mwaganu kutoka Kaunti ya Murang’a anasema kwamba polisi wakisikia mlio wa bunduki haramu, huwa wanaingiwa na ‘wazimu’ fulani na wanaweza wakaua hata wasio na makosa.

“Vita vya risasi huwa na milio ya kishetani na kila anayevishiriki huwa sio mtu wa kawaida tena na ndio madhara hata ya kisheria huzuka,” asema Bw Mwaganu.

Anasema kwamba uhalifu ni haramu lakini kuwa afisa wa polisi aliyejihami na anayefyatua risasi sio kinyume na sheria na ndiyo sababu jambazi yeyote anayetegemea haki za kibinadamu kuepuka mauti ako katika dunia telezi inayoweza ikammeza wakati wowote”.

Duru moja katika vitengo vya polisi imeelezea Taifa Leo kwamba “sio tu eti majambazi watazidi kuuawa katika makabiliano ya risasi na maafisa”.

“Kuna wengine tutazidi kuwaendea kule waliko, tuwateke nyara na hatimaye tuishie kuwaangamiza kwa kuwa wabunge wenu wamekataa kuimarisha sheria za kupambana na uhalifu suguk,”akasema.

Mdokezi wetu alisema kwamba “kuna majambazi sugu ambao wamesoma sheria na wanajua kwamba wakiwa hawajapatikana na ushahidi, wako salama…hao ni magaidi na wafuasi wa magenge mengine hatari ya kijamii ambao hushambulia na kuficha ushahidi kwamba tukiwapata, hawana cha kuwahusisha na ujambazi huo wa mauti”.

Aidha, wakishtakiwa huwa wanajipa huduma ya mawakili walio na uzoeefu na kuishia kuachiliwa huru.

“Sisi huwa tunakosa raia wa kutoa ushahidi wa kufunga majambazi hao,” akasikitika.

Katika hali hiyo, akasema, tegemeo la usalama ni risasi tu kwa njia yoyote ile.

Alisema kwamba “hao ndio tuko na haja nao zaidi”.

“Hakuna vile mtakubaliwa kutumia elimu na sheria kutukoroga akili eti kwa msingi wa haki za kibinadamu. Tutakuja uliko kama jambazi, tukuchukue na tuhepe nawe na utaenda kufuatilia haki zako huko kuzimuni,” akasema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Hofu biashara zenye hatari ya milipuko zikitapakaa mitaani

Elimu, kilimo kutengewa fedha zaidi kwenye bajeti ijayo

T L