Makala

Polisi, wanafunzi watajwa miongoni mwa washukiwa wa ‘kutoa lock’

January 31st, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

KILIO kimeongezeka katika mitaa ya Jua Kali, Grogan na steji ya Mukurwe-ini, ambapo wanaume hupanga foleni kuanzia saa kumi za asubuhi, wakiendea pombe ya ‘kutoa lock’, imefichuka.

Lakini ukiwafuata ujifahamishe zaidi, utagundua kwamba wanaume hao wamefika katika mangweni ya ulevi.

Ile pombe ya kipimo cha Sh10 ambayo katika lugha ya mitaa ilikuwa ikifahamika kama ‘Kumikumi’ kwa sasa imepanda bei na kubadili jina hadi ‘thirty thirty’ ikiuzwa kwa Sh30.

Kipimo hicho cha Sh30 ni kiwango cha thumuni ya lita, yaani huwa imegawanywa mara nane. Hiyo pombe ya vipimo kwa siku nyingi imedaiwa kuchangia vifo.

Wanafunzi wakiwa na sare rasmi za shule, wanataaluma wakiwemo matabibu na walimu, wahudumu wa mochari za mji huo, maafisa wa polisi na askari wa kanjo wa Murang’a, huonekana wakijumuika na vibarua sambamba na wahudumu wa matatu kupimiwa pombe.

Walio na uwezo kidogo huwa wanaotumia pombe za kupimwa kwa vikombe, kikubwa kikiwa cha Sh60 au Sh70 kulingana na brandi.

Walio na uwezo wa juu utawapata wamekamata vipimo vya kati ya Sh150 na Sh200 huku wengine wa kiwango cha masonko wakijipa za chupa.

“Ni hali ya kusikitisha ambapo walevi huamka saa tisa ili wafike katika mabaa kadha ambayo kupitia ushawishi wa wamiliki wayo kwa maafisa wa kiusalama, huwa wanafungua milango yao kuwapimia waraibu hao pombe,” akasema mwenyekiti wa muungano wa wakazi wa Murang’a mjini James Gitau.

Bw Gitau aliambia Taifa Leo kwamba sheria za uuzaji pombe huvunjwa pasipo kujali mjini Murang’a.

“Hapa polisi hushuhudia pasipo kujali kwa kuwa mlungula huwa umetembezwa,” akadai Bw Gitau.

Aliyekuwa Kamishna wa Murang’a Patrick Mukuria ambaye amehamishiwa Kaunti ya Kisii, alisema wiki jana kwamba ulevi ulikuwa umegeuka janga.

“Ni ukweli ulevi umepenya vibaya sana ambapo hata wafanyakazi wa umma wametekwa na pombe,” akasema Bw Mukuria.

Alisema ikizingatiwa kwamba polisi ni miongoni mwa washukiwa wakuu wa ulevi wa kiholela, “bila shaka kuna shida kubwa”.

Kamanda wa polisi Mary Wakuu alikataa kujadili suala hilo wakati Taifa Leo ilimfikia kutaka kauli yake.

Hata hivyo, Taifa Leo ilionyeshwa jumbe tano za ujasusi ambazo zimeandaliwa na kamati ya usalama ya Murang’a na kunakiliwa makao makuu ya Wizara ya Usalama wa Ndani jijini Nairobi.

Ujumbe mmoja unaelezea jinsi ambavyo maafisa wa polisi huokota mlungula wa Sh500 kwa kila baa kila Ijumaa ndipo ulevi kiholela utandazwe, nao hao wa kufungua saa kumi asubuhi kutoa walevi ‘lock’ wakihitajika kutoa hongo zaidi ya Sh300 kwa siku.

Huku hali hii ya kufedhehesha wenyeji ikiendelea kushuhudiwa mjini Murang’a, naye Naibu Rais Rigathi Gachagua anazidi kusema kwamba vita dhidi ya ulevi vinaendeshwa mashinani kwa ufanisi.

Kwa sasa, wamiliki wa baa na pia wanaonuia kujiunga upya na sekta hiyo ndio wako katika harakati za kujisajili kwa minajili ya leseni za 2024.

Licha ya Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata kutangaza kwamba leseni za 2023 zingepunguzwa kwa asilimia 60, hali hiyo haikutimia kwa kuwa hakuna iliyofutiliwa mbali, baa nyingine za ziada hata zikichipuka.

[email protected]