Polisi watia nguvuni mashabiki 148 waliozua ghasia jijini Paris baada ya PSG kupigwa na Bayern kwenye fainali ya UEFA
Na CHRIS ADUNGO
MAAFISA wa polisi nchini Ufaransa wamesema kwamba waliwatia nguvuni jumla ya mashabiki 148 walijitoma barabarani na kuanza kuandamana jijini Paris baada ya kikosi cha Paris Saint-Germain (PSG) kuzidiwa maarifa na Bayern Munich kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
Vita, vurugu, fujo na makabiliano makali kati ya waandamanaji na polisi yalianza katika eneo la Champs-Elysees karibu na uwanja wa Parc des Princes, Paris pindi baada ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kati ya PSG na Bayern kutoka Ujerumani kupulizwa.
Bayern ya kocha Hansi Flick iliibuka na ushindi wa 1-0 na kutawazwa wafalme wa bara Ulaya kwa mara ya sita katika historia.
Bao la miamba hao wa Ujerumani lilifumwa wavuni na chipukizi Kingsley Coman, 24, ambaye ni mzawa wa Ufaransa.
“Magari yalichomwa, maduka yakavunjwa, uporaji ukafanyika na madirisha ya vioo ya majengo mengi kuharibiwa na mashabiki waliokuwa wamekongamana nje ya uwanja wa Parc des Princes kutazama mechi kwenye runinga kubwa,” wakasema polisi.
PSG walikuwa wakilenga kunyanyua ubingwa wa taji la UEFA kwa mara ya kwanza katika historia.