Makala

Polisi wawapa raia maua Valentino kutuliza mioyo yao

Na MERCY SIMIYU, DOMNIC OMBOK February 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAAFISA wa polisi kote nchini, walitenga muda kutoka majukumu yao ya utekelezaji wa sheria Siku ya Wapendanao ili kutoa maua kwa umma.

Mpango huo uliolenga kukuza uhusiano chanya kati ya idara za sheria na wananchi, ulishuhudia maafisa wakisambaza maua katika maeneo mbalimbali ikiwa ni ishara ya shukrani na kuonyesha nia njema.

Jijini Nairobi, Naibu Inspekta Jenerali Eliud Lagat (Huduma ya Polisi Kenya) na Gilbert Masengeli (Huduma ya Polisi wa Utawala) waliongoza mpango huo, wakisimama bila mpangilio katika mji mkuu ili kutoa maua na kutangamana na umma.

Maafisa hao walitaka kuonyesha wanajali ustawi wa Wakenya katika maisha yao ya kila siku huku pia wakiimarisha ari ya huduma ya polisi katika kudumisha usalama wa umma.

Mpango huu ulijiri wakati ambao umma umekuwa ukikosoa utekelezaji wa sheria, kuwalaumu utekaji nyara, kutoweshwa kwa wakosoaji wa serikali na mauaji ya kiholela.

Katika miezi ya hivi karibuni, mashirika ya haki za binadamu na familia za wahasiriwa wameibua wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa idadi ya watu waliopotea na visa vya ukatili wa polisi, wakitaka uwajibikaji na haki.

“Tunaungana na Wakenya wengine kusherehekea siku hii maalum kwa kuwapa maua kama ishara ya upendo  kutoka Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kwa watu. Asubuhi ya leo, tulipata fursa ya kutangamana na umma, na kuwaruhusu kuona upande wetu tofauti- hatua ambayo inaonyesha kwamba sisi pia tuna hisia na tunajali kwa dhati ustawi wao,” alisema Bw Lagat.

Kwa upande wake Bw Masengeli alisema hatua hiyo inatokana na moyo wa upendo.

“Zamani, watu wakiwaona polisi walikuwa wakikimbia na wengine kuwa na hofu, ukiangalia nyuma, hiyo ilikuwa ni ishara ya ukatili wa polisi, lakini leo askari polisi ni ndugu, dada, marafiki na familia, ujumbe wetu kwa umma ni kuwaombea na siku zote kumbuka kumjali jirani yako jinsi unavyojijali mwenyewe ili sote tuishi kwa maelewano,” alisema Bw Masengeli.

Roho ya upendo na shukrani waliyoonyesha polisi ilienea hadi Kisumu, ambapo Jane Atieno mwenye umri wa miaka 61 aliadhimisha Siku ya Wapendanao ambayo hatasahau kamwe.

Kwa mara ya kwanza maishani mwake, alipokea zawadi ya Valentino—ua mbichi na jekundu lililotolewa na afisa wa polisi kutoka Kituo cha Central, Kisumu.

“Kupokea ua langu la kwanza katika siku hii maalum, na kutoka kwa afisa wa polisi, kunaifanya kuwa ya ajabu zaidi,” Bi Atieno alisema.