Makala

Presha Gachagua aunge mkono Raila kuwa mwenyekiti wa AU

February 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

SHINIKIZO zimezidi kumwandama Naibu wa Rais Rigathi Gachagua aunge mkono hadharani azima ya Raila Odinga kuteuliwa kuwa mwenyekiti mpya wa tume ya muungano wa Bara Afrika (AUC).

Huku Rais William Ruto akiwa tayari ametangaza hadharani kwamba ari ya Bw Odinga ya kutwaa wadhifa huo sasa ni mradi wa serikali, Bw Gachagua amebakia kimya.

Kinara wa mawaziri Bw Musalia Mudavadi, Spika wa bunge la kitaifa Bw Moses Metang’ula na Spika wa bunge la Seneti Bw Amason Kingi tayari wametangaza kumuunga mkono Bw Odinga.

“Anangojea nini Gachagua? Amebeba uhasama wa kisiasa hadi Barani Afrika kiasi kwamba hawezi akamtakia Bw Odinga mema katika wadhifa ambao utaipa Kenya hadhi Barani na pia kimataifa? Cha busara kwake ni atangaze kwamba Kenya na pia Mlima Kenya kwa pamoja wanaunga mkono Bw Odinga,” asema Bw Zack Kinuthia ambaye alikuwa waziri msaidizi (CAS) wa Spoti na Elimu katika utawala wa Rais mstaafu, Uhuru Kenyatta.

Seneta wa Kiambu Bw Karungo Thang’wa ambaye ni mwandani wa Bw Gachagua tayari amesema kwamba haungi mkono Bw Odinga.

“Mimi sioni haja ya kuunga mkono mtu huyo (Bw Odinga) ilihali tulikuwa na mtoto wetu wa hapa mlimani na ambaye ni Kenyatta,” akasema.

Bw Thang’wa alimtaka Bw Gachagua azindue harakati za kubatilisha kuteuliwa kwa Bw Odinga na Kenya kuwania wadhifa huo na badala yake jina la Bw Kenyatta lipigiwe debe.

“Ni kama wengine wetu hata hatuelewi jinsi mambo haya yanaenda. Mtu anachukuliwa kama mgombezi wa wadhifa huo ikiwa ametuma ombi. Bw Odinga ndiye tu Mkenya ambaye ameomba hiyo kazi. Sasa tutaanza kuleta jina la Bw Kenyatta katika mjadala huo tukisaka nini hasa kwa siasa?” akawaza Seneta wa Murang’a Joe Nyutu.

Bw Nyutu aliwataka Wakenya wote kwa umoja “akiwemo Bw Gachagua tuunge mkono Bw Odinga kwa kuwa rais wetu ametangaza hadharani kwamba taifa la Kenya liko nyuma ya Odinga… Isiwe kana kwamba kuna wengine wetu ambao wana taifa lao pembeni”.

Waziri wa Utumishi wa Umma Bw Moses Kuria amesema kwamba “tunafaa kama serikali kujitokeza kwa sauti moja kukiri hadharani kwamba Bw Odinga ni mradi na fahari yetu katika harakati hizo za kutwaa uenyekiti wa AU.

“Utakosa kuunga mkono Mkenya namna gani? Odinga apate wadhifa huo ili hata tukifika katika kongamano za Barani Afrika tunaringa naye tukisema ni Mkenya. Sioni ni kinyongo kipi kitazuia yeyote hapa nchini kutomuunga mkono hadharani Bw Odinga,” akasema Bw Kuria.

Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Kirinyaga, Bi Njeri Maina alisema kwamba “hata uangalie suala hili kutoka upande gani wa kisiasa, hali itabakia tu kwamba Bw Odinga ndiye chaguo muafaka na hatuna budi kumuunga mkono tukiwa kama Wakenya”.

Alisema “kukosa kumuunga mkono ilhali ndiye tu ameelezea nia ya kuutwaa ni kinyongo kisicho na msingi wowote”.

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi amesema kwamba “tusiwe wa kuonekana kuwa watu wa dharau. Ni sawa kutounga mkono Bw Odinga katika uchaguzi wa hapa nchini lakini nje ya nchi ambapo hana Mkenya mwingine anayeshindana naye hatuna budi kumuunga mkono kama ishara ya uzalendo”.

Bw Ngugi alisema “ni mjinga tu wa mwisho ambaye atapinga Bw Odinga… Kwa kuwa taifa linapojipata katika ushindani na mataifa mengine, uzalendo hutushinikiza tujumuike nyuma ya bendera ya Kenya”.

Bw Ngugi alisema “Mlima Kenya unafaa kuwa katika mstari wa mbele kuunga Bw Odinga mkono na kwa sasa anayefaa kuwa ametutangulia kuunga harakati hizo sio mwingine bali ni Gachagua mwenyewe”.

 

[email protected]