• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 2:49 PM
Priscilla wa Imani: Upigaji mbinja ulivyomletea mafanikio maishani

Priscilla wa Imani: Upigaji mbinja ulivyomletea mafanikio maishani

NA WANDERI KAMAU

JE, unafahamu kuwa upigaji mbinja pekee unaweza ukakuletea mafanikio?

Naam, upigaji mbinja tu!

Hiyo ndiyo simulizi ya Bi Priscilla Gakuru, maarufu kama ‘Priscilla wa Imani’.

Bi Gakuru alipata umaarufu mkubwa kupitia mitandao ya kijamii mwaka uliopita, 2023, kutokana na upigaji mbinja kwa njia ya kipekee.

Pia, hilo ni ikizingatiwa kuwa yeye ni mwamamke.

Mara nyingi, mtindo huo huwa unahusishwa na wanaume. Hivyo, watu wengi walishangazwa sana na uwezo wake wa kupiga mbinja kama wanaume wale wengine.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali, Bi Gakuru alisema kuwa upigaji mbinja ni uraibu ambao huwa unamsaidia kujituliza na kuondoa mawazo mengi ambayo huwa nayo.

“Kila mtu huwa na uraibu wake. Huu ndio uraibu wangu. Huwa ninapata tulizo la kipekee ninapopiga mbinja,” akasema kwenye mahojiano.

Bi Gakuru ameolewa na ni mfanyabiashara katika mji wa Nyahururu, Kaunti ya Laikipia.

Kinyume na matarajio ya watu wengi, anasema mumewe huwa anamuunga mkono kwenye uraibu wake huo wa kipekee.

“Mume wangu huwa hana tatizo nami kutokana na uraibu huu. Badala yake, huwa ananiunga mkono na nyakati nyingine hata kunifunza!” akasema.

Bi Gakuru ni mama wa watoto watatu; mvulana na wasichana wawili. Anasema hakuna mtoto wake hata mmoja ambaye ameonyesha kuvutiwa na uraibu wake.

Je, kando na kumpa umaarufu mkubwa mitandaoni na kote nchini, amepata mafanikio yapi?

Bi Gakuru anasema ijapokuwa baadhi ya watu humwona kama “mwendawazimu”, amepata mafanikio mengi kupitia upigaji mbinja.

Anasema hadhani ikiwa angejulikana na kujizolea umaarufu mkubwa, isingalikuwa ni video zilizosambaa mitandaoni zikmwonyesha akipiga mbinja.

“Nimepata mafanikio makubwa. Kutokana na umaarufu wangu, nimefanikiwa kuwa balozi wa kutangaza biashara za kampuni kadhaa za kuuza mashamba. Nilifanikiwa kutimiza hayo kupitia mikataba niliyotia saini katika kampuni hizo. Hilo limenisaidia kupata pesa ambazo nimewekeza katika biashara yangu,” akasema Bi Gakuru.

Vile vile, anasema kuwa, ikizingatiwa alijizolea umaarufu wake kwa njia ya kipekee, amekuwa akialikwa katika hafla tofauti nchini kuwatumbuiza wageni na watu mashuhuri.

“Katika hafla hizo, mimi huwa sialikwi kama msanii. Utumbuizaji wangu huwa wa kipekee. Huwa naalikwa kuwapigia watu mbinja!” akasema huku akiangua kicheko kikubwa.

Anasema amefanikiwa kutangamana na watu maarufu, kama vile  mawaziri na viongozi wengine wa ngazi za juu.

“Ni fahari kubwa mtu anapoalikwa kuwafurahisha watu kwa njia ambayo wengi huichukulia kuwa mzaha,” akasema.

Hata hivyo, anaeleza kuwa hajatumia umaarufu wake kujifaidi pekee. Anasema kwamba kama mwanamke, amekuwa akitumia umaarufu huo kuzisaidia jamii ambazo hazijajiweza, hasa zinazoishi katika mitaa ya mabanda maeneo ya mijini.

Baadhi ya maeneo ambayo amekuwa akiendesha mpango huo ni mtaa duni wa Mathare, jijini Nairobi.

“Nimekuwa nikichangisha pesa kupitia njia ya mtandao ili kuzisaidia familia zinazoishi katika eneo hilo kupata chakula. Imani yangu ni kwamba, kama mama, sifai kutumia umaarufu wangu kujisaidia tu, bali pia kuwasaidia watu wengine wasiojiweza katika jamii,” akasema.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Mcheshi Kiengei atangaza kuunga mkono Gachagua kukabili...

Uzinduzi wa vitabu vya Kibajuni kudumisha tamaduni  

T L