Makala

RAEL MUKEKU: Mke wa wanaume wawili, na wanaishi kwa raha

September 3rd, 2018 Kusoma ni dakika: 3

Na PIUS MAUNDU

UKIKUTANA naye njiani akivalia nadhifu na kufuga nywele fupi asili, utadhani Bi Rael Mukeku, ni mwanamke wa kisasa, lakini sivyo.

Mwanamke huyu mwenye umri wa miaka 35 ni mama ya watoto 11 na mke wa wanaume wawili.

Anaishi katika nyumba ndogo ya matope iliyoezekwa nyasi nyuma ya soko la Kathekakai, karibu na mbuga ya wanyama pori ya Chyullu Hills, Kaunti ya Makueni.

Na asipokufahamisha hautaelewa kwamba ameolewa na wanaume wawili, maisha ambayo anasema anayafurahia.

“Niliolewa na mume wangu wa kwanza 1992 na tukapata mtoto wetu wa kwanza mwaka uliofuata. Nimezaa watoto wengine kumi,” Mukeku alifahamisha Taifa Leo na kusimulia alivyojipata katika mtindo wa maisha usiochukuliwa kuwa wa kawaida na jamii ya Wakamba na jamii nyingi nchini Kenya.

Wakati wa mahojiano, alikuwa aking’ang’ana kuwatuliza watoto watatu wadogo waliokuwa wakilia kwa njaa akiwa amempakata mwingine.

Alisema alisoma hadi darasa la pili katika shule ya msingi iliyo karibu na kwao na akafanya kazi ya yaya kwa majirani kabla ya kuolewa hapo kwao kijijini.

“Niliolewa na mume wa pili nikiwa na watoto saba. Hakutaka kuwatunza watoto hao bila kuzaa wake mwenyewe na hivi ndivyo tulipopata watoto zaidi,” alifichua.

Kwa wakati huu, Mukeku ni nyanya wa wajukuu wawili na anakiri kwamba aliacha uraibu wa kulewa, kutafuna miraa na kunusa tumbaku, hulka ambayo anasema alianza kuwa nayo akiwa mdogo kutokana na utukutu hadi aliposhauriwa na madaktari kuacha.

Hata hivyo, anasema hajuti kuolewa na wanaume wawili ambao wanafanya kazi ya vibarua.

“Makosa yangu ni kuwa niliolewa na wanaume ambao si matajiri lakini sijuti kwa sababu wananijali na kunipenda,” asema na kukumbuka kisa cha majuzi ambapo waume zake waliungana kumsaidia akiwa mgonjwa.

“Mmoja aliuza mbuzi wake wote watatu kunilipia bili ya hospitali na yule mwingine akatoa pesa za kukidhi mahitaji yetu ya kila siku,” alisema.

Bi Mukeku anasema kwamba kabla ya kuolewa na mume wa pili alimweleza mama yake kwamba hakuwa akitosheka na tendo la ndoa.

Uamuzi wa kuolewa na mume wa pili ambao ulikubaliwa na mumewe wa kwanza Muema Nguu, ulitokana na ukosefu wa pesa tofauti na dhana kwamba mtindo wa wanawake kuolewa na wanaume wawili huendelezwa na matajiri.

“Ulifika wakati ambapo alinishauri nitafute mwanamume mmoja ambaye ningemtambulisha kwake kwa sababu tunaishi enzi za maradhi hatari,” alisema.

Bw Nguu anasema haikuwa rahisi kufikia uamuzi huo. “Ulikuwa uamuzi mgumu sana kufanya. Ulitanguliwa na kipindi kigumu mno ambacho nilikuwa dhaifu baada ya kuugua kwa muda mrefu,” asema mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 50 huku akichunga mifugo wa mwajiri wake katika kijiji jirani.

Wanaume hao waliweka mkataba ulioshuhudiwa na mzee wa kijiji chao na mmoja wa wana wao wakubwa lakini mwanzoni, Bw Nguu alikuwa na wakati mgumu kuzoea ndoa ya kugawana mke.

“Nilipogundua kwamba alikuwa amemtunga mimba, nilikasirika na kuonya hilo lisitendeke tena,” alisema.

Hata hivyo, watoto watatu zaidi walizaliwa na Bw Nguu akamkumbatia mume mwenza ambaye wamepitia masaibu sawa maishani.

Wawili hao waliachwa mayatima wakiwa wa umri mdogo na wakaanza kufanya kazi za vibarua katika boma za majirani matajiri walipolazimika kuacha masomo kufuatia ukosefu wa karo.

“Jamaa zangu hawafurahii ndoa ya aina hii lakini kila wakati wakilalamika, huwa ninawakumbusha kwamba walikataa kunisaidia kulea wanangu,” alisema Bw Nguu akijuta kwamba watoto wake hawakuweza kupata elimu.

Anasema baadhi ya watoto wake wakubwa hawajakubali ndoa hiyo.

“Wasiwasi wetu ni kuwa huwa anapanda mbegu ya chuki miongoni mwa watoto kwa kuwatambua na baba zao. Tumekuwa tukimshauri asiwabague kwa kuwaambia kuwa ni wa mume huyu au yule,” asema jirani yao Timothy Mutua ambaye ni jamaa ya familia yao.

Mume mwenza wa Bw Nguu, Mutuku Muia, 45, anayefanya kazi katika mashamba ya majirani anasema hana tatizo na ndoa hiyo.

“Watoto wake huniita baba. Akishindwa kulipa karo, huwa ninamsaidia, naye huwa anarudisha mkono nikiwa na shida ya pesa akiwa nazo,” alisema.

Tofauti na Muia anayelala nyumbani kila siku, Bw Nguu hufika nyumbani mara mbili kwa mwezi.

Wanakijiji hao hawajumuiki pamoja wakihofia huenda baadhi yao wakawaripoti kwa serikali kwa kuingia katika mbuga ya wanyama kutafuta kuni na kuchuma miraa.

“Sio watu wengi waliofahamu kinachoendelea katika familia hii hadi juzi mwanamke huyo alipougua,” alisema Bw Japheth Musyoki, mhubiri katika kanisa la Centurion Gospel Ministries.